Mr.Mwalimu Blog
Kero ya maji katika kanda ya Ziwa ni jambo la kustaajabisha
sana kwa watu ambao hawajawahikufika ukanda wa ziwa, kwa sababu wao picha
walioyonayo kichani ni tofauti na hali halisi. Wengi tunaposema kanda ya ziwa
kuna shida ya maji hawaamini lakini ndiyo ukweli.
Mikoa ya Mwanza, Geita, Mara na Simiyu ni moja ya mikoa
yenye uhaba mkubwa wa maji licha ya kulizunguka ziwa Victori ambalo lingeweza
kuwa chanzo mbadala cha maji. Wakazi wengi wa maeneo haya wanatumia maji yasiyo
salama na machafu. Mathalani, Mkoa wa Mara ambao umepitiwa na Ziwa victori una
kero kubwa ya maji hata kwa wakazi wanaoishi jirani na ziwa hilo.
Mkoa wa Mara na
wilaya zake kama Rorya, Tarime, Bunda, na Serengeti bado hawajanufaika na uwepo
wa Ziwa Victoria kama chanzo cha maji. Mkoa huu ambao pia una chanzo kingine
kikubwa cha maji kama kingewekewa mikakati mizuri ambacho ni Mto Mara, wakazi
wake hawana uhakika wa kupata huduma ya maji!
Inashangaza kama Mufindi ilivyoshangaza kuwa miongoni mwa
wilaya ambazo wanafunzi wanakaa chini kutokana na ukosefu wa madawati licha ya
kwamba Mufindi ndiyo wilaya inayoongoza kwa kuzalisha miti, mbao na kusambaza
kwa nchi nzima! Na kanda ya ziwa ni hivyo maji ya Ziwa victori yamepelekwa mkoa
wa Shinyanga, ambako ni mbali sana na ziwa lilipo lakini Geita, Mara, Simiyu
ambako ndiko ziwa liliko hakuna maji.
Kama ilivyo mikoa mingine ambayo haina mito wala maziwa,
wakazi wa kanda ya ziwa wanasumbuliwa na kero ya maji kama wao. Mathalani
Maeneo ya jirani na Shirati, na kata kadhaa za wilaya ya Rorya, Komaswa kwa
upande wa Tarime, maji yanauzwa mapaka shilingi mia 400 na 500 kwa lita
ishirini. Na maji yanayonunuliwa kwa bei hiyo bado si salama.
Mikoa ya kanda ya ziwa ambayo wakazi wake wengi ni wafugaji,
wanategemea maji ya mvua, maji yaliyovunwa kupitia mvua yakiisha, wakazi wa
kanda ya ziwa wanatumia maji ya kwenye malambo ambayo pia yanatumika kunyweshea
mifugo.
Ukosefu huu wa
maji unaathiri mfumo mzima wa maisha ya
wakazi wa kanda ya ziwa kwa sababu bila maji hakuna uhai, hakuna afya bora,
hakuna furaha ya maisha. Fikiri baadhi ya maeneo ya mikoa ya kanda ya Ziwa
wakazi wake wanatumia zaidi ya saa nne ili kupata maji toka umbali wa
kilometa zaidi ya kumi.
Uhaba wa maji unaathari kubwa sana katika sekta ya elimu,
wanafunzi wa mikoa ya kanda ya ziwa wanaumizwa zaidi na hali hii, kwa kweli ni
wahanga wa kuu wa kero ya ukosefu wa maji.
Penye ukosefu wa maji safi na salama, hapana afya bora.
Magonjwa ya tumbo ni moja ya changamoto kubwa sana kwa afya ya wanafunzi wa
kanda ya ziwa. Wanafunzi wengi huugua magonjwa ya tumbo hivyo kushindwa
kuhudhuria masomo. Katika siku 192 za masomo kwa mwaka, zaidi ya siku
thelathini zinapotea bila kuhudhuria masomo kutokana na kusumbuliwa na magonjwa
ya tumbo!
Kero ya maji inasabisha mahangaiko makubwa kwa wanafunzi,
hii ni kwa sababu shule nyingi hazina visima wala mabomba ya maji. Katika shule
hizi wanafunzi hulazimika kubeba vidumu vya maji kutoka nyumbani ili kumwagilia
maua na miti ya mazingira ya shule pia kwa ajili ya huduma ya choo. Wakati
mwingine wanafunzi wanatumia muda mrefu kwenda kufuata maji mara baada ya
kuripoti shule kiasi wanakosa vipindi vyote vya asubuhi.
Ukosefu wa maji unaathiri pia ratiba ya wanafunzi kujisomea
nyumbani mara baada ya kurejea kutoka shule. Ili mwanafunzi afanye vizuri
katika masomo lazima apate muda wakutosha kujisomea baada ya saa za shule.
Wanafunzi wengi wa
kanda ya ziwa hawana muda wa kujisomea, maana mara tu wanaporejea kutoka shule
wanafanya safari nyingine ndefu na yenye mikiki mikiki mingi kwenda kufuata
maji. Huko licha ya kusafiri umbali mrefu hukutana pia na foleni kubwa kiasi
hupoteza saa nyingi zaidi ambazo wangeweza kuzitumia katika masomo.
Kero hii ya maji inaathiri pia walimu, walimu waliopelekwa
na serikali maeneo haya ya kanda ya ziwa, wanakatishwa tamaa pia na hali ya
ukosefu wa maji. Gharama kubwa ya kupata maji, muda mwingi unaotumika ili
kupata maji vinaathiri ufundishaji wa walimu katika shule zao.
Wanafunzi wanakosa
masomo kwa sababu walimu wanatumia muda mwingi kufuata maji. Hali hii pamoja na
maji yenyewe kuwa si masafi na salama imechangia walimu wengi kutopendelea
kufanya kazi katika vijiji ambavyo vinashida ya maji. Baadhi wamelazimika
kuhama haraka au hata kuacha kazi.
Usafi binafsi wa wanafunzi kama vile kuoga, kufua na
kadhalika vinakuwa vigumu kwa wanafunzi kwa sababu ya ukosefu wa maji.
Mwanafunzi anatakiwa pia kujifunza kujiweka nadhifu, ufundishaji unadhifu kwa
vitendo kwa vijana wetu unakuwa mgumu kwa sababu ya shida ya maji. Kuna wakati
mwanafunzi anavaa ngua chafu inabidi tu mwalimu uvunge maana unajua
kinachomsibu.
Ushauri wangu kwa viongozi wa mikoa ya kanda ya Ziwa na
wilaya zake, wakuu wa halmashauri na madiwani, wabunge wote bila kujali wajimbo
ama wa kuteuliwa suala la ukosefu wa maji liwe ajenda kuu katika vikao na
litekelezwe kwa vitendo.Ni aibu na uzembe kanda ya ziwa kukosa maji.\
Pia wananchi wa kanda
ya ziwa ni wakati wakudai maji bila kusita bila uitikadi wa vyama, katika kila
kikao tunachokaa na viongozi wetu tuwaambie MAJI KWANZA.MR.MWALIMU.BLOGSPOT.COM, ELIMU KWANZA.


0 Comment to "Kanda ya Ziwa bila maji: Ukosefu wa maji unavyoathiri elimu"
Post a Comment
New post Overview Posts Pages Comments Stats Earnings Campaigns Layout Template Settings 1401 1409Post a Comment
1410
1411 1412 1413 1414