Wednesday, December 28, 2016

Hakuna elimu bora kwa wazazi wanaobweteka

Wanafunzi wengi wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo hawafanyi vizuri kitaaluma kwa sababu ya wazazi wao kutofuatilia maendeleo ya watoto wao. Wazazi wanafikiri majukumu yao ni kulipa ada na michango mengine pekee na kuwaachia walimu.


Wazazi wengi wana shauku kubwa ya kuona watoto wao wanafanya vizuri katika masomo, lakini hawako tayari kufuatilia maendeleo yao ya taaluma na hata nidhamu.

Jukumu hilo wameachiwa walimu peke yao. Na walimu wanapojaribu kuwanyoosha kinidhamu, jamii kwa upande mwingine inawanyooshea kidole na kuwalaumu.

Uzoefu unaonyesha, kwa sababu ya ugumu wa maisha wazazi wengi hawana muda wa kukagua daftari za watoto wao, kutembelea shuleni na kufanya mashauriano na walimu.

Kwa kutembelea shule, kuna mengi yanaweza kutafutiwa ufumbuzi kati ya mwalimu na mzazi, lakini hilo halifanyiki. Mzigo wote anaachiwa mwalimu ambaye hata hivyo hulaumiwa pindi matokeo yakiwa mabaya.

Tujiulize kosa la mwalimu huyu aliyeachiwa mzigo wa kusomesha na ule wa malezi ambao haumhusu. Wakati mwingine, ufaulu mdogo unatokana na wanafunzi kutokuwa na nidhamu, upi wajibu wa wazazi katika hili?

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwa Kiingereza: “It takes a village to raise a child” yaani ni jukumu la jamii au kijiji kumkuza mtoto.

Hii inamaanisha kuwa ikiwa jamii itaungana kwa pamoja kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu bora, ni dhahiri hakutakuwa na malalamiko kuhusu nidhamu mbovu na hata ufaulu usioridhisha.

Linapokuja suala la ushiriki wa jamii katika kutoa elimu iliyo bora, wazazi na walezi wanapaswa kuwa sehemu ya vikao vya maamuzi kuhusu maendeleo ya watoto wao katika shule za umma kama inavyokua katika shule binafsi.

Wazazi lazima watambue kwamba Serikali haiwezi kubeba majukumu yote kwa mwamvuli wa elimu bure, huku wakibweteka na kusubiri watoto wao wapate elimu itakayoleta mabadiliko katika maisha.

Wazazi wasiwe wapiga filimbi kuwalaumu walimu tu na kuzuia adhabu zinazotolewa na walimu kwa wanafunzi. Lazima wayaelewe mazingira wanayofanyia kazi walimu na aina ya wanafunzi walio nao.
Wanaposhindwa kutoa ushirikiano kuhusu suala zima la maendeleo ya wanafunzi, walimu nao wanakata tamaa na kuacha mambo yajiendee.

Wanasiasa na watu wenye ushawishi katika jamii lazima walielewe hili na wawe mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa wazazi wanashiriki kikamilifu katika nidhamu na maendeleo ya taaluma.

Fedha zinazotumika katika elimu bure zinatokana na makusanyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo wananchi wenyewe.

Huu ni uwekezaji usiokuwa na malengo ya kupata faida hauna maana hata kidogo. Lazima wananchi tuone kwamba fedha zetu zinazokwenda kugharimia elimu ya vijana wetu zinaleta faida.

Mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu lazima ihakikishe pamoja na mambo mengine inawajengea uwezo wakuu wa shule na walimu kuhusu njia bora za kuwashirikisha wazazi.

Tukiwaachia jukumu hili walimu na Serikali tunakua tumepoteza mwelekeo. Wazazi tuwajibike kwa kuhakikisha vijana wetu wanakua nguvukazi madhubuti kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili. Vinginevyo shule zetu zitakua vituo vya kulelea watoto kwa miaka kadhaa na baadaye watoto hao wasiwe na mchango wowote kwa maendeleo ya nchi yetu.

Wakati ni sasa kila mmoja atimize wajibu wake katika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata elimu bora.


Sunday, December 25, 2016

SERIKALI Yapiga Marufuku Shule Binafsi Kufanya Mitihani ya Kuchuja Wanafunzi


Hiyo ni baada ya kutangaza kupiga marufuku utaratibu wa kuwachuja wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa uliokuwa unaofanywa na baadhi yao kwa lengo la kuonekana shule zao zinafaulisha vizuri.

Hivi karibuni, Nipashe iliripoti kuhusu hofu ya baadhi ya shule hizo; za msingi na sekondari ziko hatarini kubadilishwa matumizi kutokana na kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na kutoa elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikiwaumiza wananchi.

Huku udahili kwenye shule za serikali ukiongezeka na kuonekana kuwa tishio kwa ustawi wa shule za watu na taasisi binafsi, imewabana tena wamiliki wa shule binafsi kwa kuwazuia kufanya mchujo wa wanafunzi wanaoingia kwenye madarasa au vidato vyenye mitihani ya taifa.

Mmoja wa wazazi aliliambia Nipashe kuwa mwanawe anayesoma kidato cha tatu katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, amepangiwa kuhamishiwa shule nyingine ya mmiliki huyo huyo kutokana na kufaulu kwa daraja la tatu.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, kuna wanafunzi takribani 70 wa kidato cha tatu, wanatarajiwa kuhamishwa katika shule hiyo waliyosajiliwa tangu kidato cha kwanza, watahamishwa shule hiyo na kubaki wale waliofaulu kwa viwango vya madaraja ya kwanza na pili tu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, alisema ni marufuku shule kumkaririsha darasa, kumfukuza, kumhamishia shule nyingine au kumsajili kama mtahiniwa binafsi (PC) mwanafunzi kwa kigezo cha kutofanya vizuri katika mitihani ya shule husika.

"Ni marufuku kabisa kufanya hivyo. Mitihani tulionayo sisi (Wizara ya Elimu) ndiyo mchujo sahihi. Na mtihani ambao unamkaririsha mwanafunzi ni mtihani wa taifa wa kidato cha pili na mtihani wa darasa la nne tu," alisema.

"Wala siyo mtihani wa shule na madarasa mengine hayana mtihani wa kumkaririsha mtoto au kumfanya aondolewe shuleni au ahamishiwe shule nyingine, hatuna utaratibu huo na serikali haiwezi kukubaliana nao," aliongeza Dk. Akwilapo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongosco), Benjamin Nkonye, aliiambia Nipashe jana kuwa utaratibu wanaoutumia ni kushauriana na wazazi wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri shuleni ikiwamo kuwapeleka katika vyuo vya ufundi (Veta).

Alisema shule binafsi zinapaswa kupongezwa kwa kudahili hata wanafunzi hasa wa sekondari ambao shule za serikali huwa haziwachukui kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya shule za msingi.

“Hakuna shule ambazo zinapaswa kupongezwa kama za binafsi, serikali yenyewe imekuwa ikichagua wanafunzi wote. Inatuachia ‘vilaza’, lakini sisi kwa kujitoa kuwasaidia watoto wa Kitanzania, tunakubali kuwachukua hao hao wanaoonekana wabaya, tunawafundisha na mwisho wa siku wanakuwa wazuri kuliko hata hao wanaokuwa wamethaminiwa na serikali,” alisema Nkonya.

“Na sisi hatuchuji wala kumfukuza mwanafunzi, isipokuwa kinachofanyika kwa kuwa tunapokea wakati mwingine wanafunzi ambao ni ‘vilaza’ kabisa, huwa tunawagawanya katika makundi kulingana na uelewa wao, wenye uelewa wa kwanza, wa kati na wa mwisho. Na mwisho na tunawafundisha kulingana na ‘speed’ (kasi) ya uelewa wao na wanajikuta wanafanya vizuri.

“Lakini kwa sababu sisi tunakuwa na wanafunzi ambao ni wagumu sana, inapoonekana wakatokea wachache hawawezi kabisa huwa tunashauriana na wazazi wao, kuwapeleka Veta ili kule wanapokuwa wanaendelea kujifunza, wengine wanafanya vizuri hadi wanafika vyuo vikuu, hatuwaachi kama ilivyo katika shule za serikali na vyuo vya serikali, haya maneno mengine yanayozungumzwa ni ya kisiasa tu."

HALI ILIVYO

Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika hivi karibuni katika baadhi ya mikoa, ulibaini baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa na utaratibu wa kuchuja wanafunzi kila mwaka kwa lengo la kupata wenye uwezo mkubwa darasani.

Ilibainika kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanywa kwa nia ya kuwa na wanafunzi wenye uwezo mkubwa ili shule hizo zifanye vizuri katika mitihani ya taifa, hivyo kuvutia wazazi wengi zaidi kupeleka watoto wao.

Gazeti hili lilibaini kuwa, baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikiendesha utaratibu huo kipindi cha mitihani ya mwishoni mwa mwaka kwa kuwafukuza, kuwakaririsha darasa au kuwahamishia shule nyingine wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango kinachowekwa na shule husika kwenye mitihani ya kufunga mwaka.

Nipashe pia ilibaini baadhi ya shule hizo zimekuwa na utaratibu wa kuwachuja kwa kuwasajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) kwenye mitihani ya taifa wanafunzi wake wanaoshindwa kiwango kilichowekwa wanapofanya mitihani ya shule husika.

MTOTO WA PROFESA AKACHA KULA

Akizungumzia suala hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Allen Mushi, alisema haungi mkono utaratibu wa baadhi ya shule binafsi kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango cha alama zilizojiwekea.

Alisema: "Ni makosa kumfukuza shule mwanafunzi aliyekuwa amedahiliwa, anasoma halafu unamsitishia, unamwambia nenda katafute shule nyingine.

"Na ni kweli wana tabia hiyo. “Nina kijana wangu yuko ‘Form One’ (Kidato cha Kwanza) anasoma shule ... (anataja eneo ilipo shule hiyo), yaani anasoma kupindukia. Nilikuwa na wasiwasi hata akija likizo hawezi kula vizuri, anasoma tu."

Alisema kuwa katika shule hiyo ya jijini Dar es Salaam anayosoma mtoto wake, wameambiwa ni lazima awe na wastani wa kuanzia alama 50 katika mitihani ya shule ili aruhusiwe kuingia kidato kinachofuata, vinginevyo wakatafute shule nyingine.

"Katika utaratibu wa elimu, siyo sahihi kufanya hivyo, wewe kama wanafunzi wameshindwa, wewe siyo ndiyo mwalimu, ndiyo kazi yako ya kufanya wanafunzi waelewe," alisema na kufafanua zaidi:

“Sasa ukiwa unafanya hivyo, mwisho wa siku utakuwa unafelisha darasa zima na kujitamba kwamba unafaulisha kwa sababu umefukuza wengi na kubaki na wazuri wachache. Sasa hiyo ni biashara, siyo elimu tena. Wewe kama ni mwalimu, unatakiwa kufundisha wanafunzi wote.

“Kwa hiyo, wanasema shule za ‘private’ (binafsi) zinafaulisha wanafunzi wote, kumbe wengine mliowachuja. Mimi binafsi sikubaliani na hali hiyo kabisa."

Alisema ni muhimu wizara yenye dhamana ya elimu nchini iweke masharti kwamba ukishadahili wanafunzi, wasiondolewe shuleni kwa utaratibu wa viwango vya ufaulu katika mitihani ya shule husika isipokuwa kwa sababu za tabia mbaya na zisizofaa kwa mwanafunzi kwa mujibu wa sheria za nchi.

MAKUNDI YA UELEWA

Msomi huyo alisema wanafunzi wamegawanyika katika madaraja mawili kiuelewa darasani, la kwanza likiwa la wenye uelewa wa haraka (fast learners) na jingine likiwa la wenye uelewa hafifu (‘slow learners).

"Wote hao wanapaswa wazingatiwe katika elimu. Sasa hawa (shule binafsi) wenyewe wanaangalia 'fast learners' tu. Ni vema wote wakachukuliwa katika vigezo sawa, siyo unawachuja wengine halafu unasema unafaulisha wote," alisema Prof. Mushi.

BIASHARA

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na Nipashe jana kuhusu changamoto hiyo, alisema si vyema kumfukuza, kumkaririsha darasa au kumhamisha mwanafunzi aliyefanya vibaya katika mitihani ya shule.

"Mtihani wa Kidato cha Pili ni mchujo sahihi tu. Shule binafsi wanakosea. Ufundishaji wa kawaida huwezi kuwa na wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu," alisema.

"Hao shule binafsi kuna muda wanateleza kidogo, kwa sababu hakuna mwanafunzi asiyefundishika labda kwa sababu wao wanataka suala la biashara. Ni kuonea wanafunzi, bahati mbaya akishaanza shule ya 'private' (binafsi) kidato cha kwanza, hawezi kurudi kwenye mfumo wa serikali, kwa hiyo wanafunzi wanahangaika," alisema zaidi Mukoba.
Mr.Mwalimu blog




Friday, December 23, 2016

NCHI NANE KINARA WA KUWAKARIMU WANAFUNZI WA KIGENI



Fahamu kuwa si kwa sababu unataka kusoma nje ya nchi basi kila nchi ni salama kwako, hapana baadhi si salama kwako na baadhi ni salama kwako kutokana na vigezo na mazingira mbali mbali.

Kwa mtu ambaye una ndoto za kutafuta elimu nje ya nchi ya Tanzania, una kila sababu ya kusoma makala hii.Kadhalika mtu ambaye una shauku la mwanao au jamaa yako asome nje ya nchi taarifa hizi zawezakuwa za muhimu sana kwako.Chanzo cha makala hii ni gazeti la Mtanzania.

KILA mtu anatamani kusoma nje ya nchi hususan Ulaya ambako baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kuwa kusoma au kupata ujuzi kwenye vyuo hivyo  vya ng’ambo kutawawezesha kupata fursa zaidi za ajira ikilinganishwa na kusoma kwenye vyuo vya ndani.
Kumekuwapo baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwapata wanafunzi wa kigeni pindi wanapokuwa ng’ambo.

Hii inatokana kwamba nchi nyingi zimekuwa haziweki mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kigeni, hata inapotokea wamekumbwa na misukosuko serikali za nchi hiyo zimekuwa zikichelewa kuchukua uamuzi au  kuwatetea wanafunzi hao.
Hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya wanafunzi na wazazi  kuwa na hofu ya kwenda kusoma nje ya nchi zao.

Matukio kadhaa yasiyo ya kufurahisha yamewakumba wanafunzi wa kigeni, hali hiyo imekuwa ikitafasriwa kama ni kawaida kwa mataifa yaliyo na vyuo bora nje ya nchi jambo ambalo si kweli.

Kama ndoto zako au hata za mtoto wako ni kusoma na kupata ujuzi nje ya nchi kwenye vyuo vilivyoendelea na kujenga wasifu wake vizuri utakaomsaidia kupata kazi kirahisi ndani na nje ya nchi na bado hujajua ni nchi gani ambayo mwanao atasoma akiwa salama na kukarimiwa vizuri, makala hii itakupa mwanga.

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Ulaya EU miezi michache iliyopita, imeorodhesha nchi nane zinazoongoza kwenye kuwakarimu wanafunzi wa kigeni.

 Uingereza
Nchi hii imepata asilimia 0.7 ya kukarimu wageni huku ikinyakua asilimia 0.5 ya wanafunzi wanaohitimu kwenye vyuo vyake.

Licha ya kwamba nchi hii iliibuka kinara kwa kuwa na wanafunzi wengi wa kigeni kati ya nchi 35 za bara hilo lakini ilikuwa na asilimia 40 ya wanafunzi wake ambao walihitimu nje ya vyuo vya nchi hiyo kwa mwaka 2012-2013 jambo ambalo lilifanya ipunguziwe alama kwenye ripoti hiyo.

Mbali na ‘doa’ hilo, ni wazi kuwa Uingereza imekuwa ikisifika kwa kuwa na mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kigeni ikiwamo kuwapa msaada wa karibu na kuwashirikisha kwenye fursa mbalimbali za kiuchumi.

 Ubiligiji
Ina asilimia 2.4 ya ukarimu kwa wanafunzi huku kiwango cha wanafunzi wanaohitimu masomo yao nchini humo kikiwa ni asilimia 3.3 ambapo pia imekuwa ikisifika kwa kuwahamasisha wananchi wake juu ya watoto wao kujifunza lugha za kigeni walau 15 kwa mwaka.

Nchi hii haijapishana na Uingereza katika kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi sanjari na kuwawezesha kiuchumi ambapo katika kulitekeleza hilo imekuwa na mikakati mbalimbali ukiwamo ule wa ‘Flemish community’  wenye lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 inakuwa na asilimia 33 ya wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanaokwenda kusoma nchini humo.
Kwasasa asilimia 48 ya wanafunzi wa kigeni wanaosoma nchini humo ni kutoka Ufaransa.

 Denmark
Hii ina asilimia 1.3 ya ukarimu kwa wanafunzi huku ikiwa na asilimia 1.7 ya wanafunzi wa kigeni wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini humo.

Denmark ni miongoni mwa nchi chache za Ulaya zinazotoa msaada mkubwa zaidi kwa wanafunzi wa kigeni karibu wote wanaofika kuchukua masomo yao nchini humo, pia inatoa ushirikiano zikiwamo taarifa mbalimbali kwa wanafunzi.

Pamoja na mambo mengine imeweka mkazo wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anajifunza lugha mbili kwa wakati mmoja kwa kipindi cha walau miaka mitano huku akipata mkopo na msaada mkubwa kutoka serikalini.

Nchi nyingine ambazo zimekuwa na alama za juu zaidi ni pamoja na Ujerumani ambayo ina asilimia 3.9 ya kukarimu wanafunzi wa kigeni huku ikiwa na asilimia 54.1 ya wanafunzi wa kigeni wanaohitimu masomo yao nchini humo.

Lakini pia imekuwa ikitoa misaada ya hali na mali kwa wanafunzi wote wa kigeni wanaofika nchini humo. Nyingine ni Bulgaria yenye ukarimu wa asilimia 7.8 kwa wanafunzi wa kigeni na asilimi 6.6 ya wanaohitimu. Asilimi 52 ya wanafunzi wake wanatoka nchini Uturuki.

Nyingine ni Uholanzi, Luxembourg na Slovakiam. Chaguo ni lako mwanafunzi na mazazi kumpeleka mwanao nje au la kwani nchi hizo zote zina mazingira rafiki ya taaluma na hali ya juu

MRMWALIMU.BLOGSPOT.COM#ELIMU KWANZA


 MR.MWALIMU.BLOGSPOT.COM#ELIMU KWANZAM

Friday, December 16, 2016

Sitisho la ajira kwa walimu wa sanaa litazamwe upya.

Waziri wa elimu ametangaza kusitisha ajira kwa walimu wa sanaa, kwa mtazamo wangu nafikiri ni bado mapema kuchukua maamuzi hayo.Nchi hii inaupungufu wa walimu mkubwa bado.Upungufu mkubwa upo kwenye Sayansi lakini hata sanaa inaupungufu. Kuna shule hazina walimu wa Kiswahili, Kiingereza wala Jiografia.

Chanzo cha habari hii ni gazeti la Mtanzania.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku akisema Serikali haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa kutosha.

Akizungumza mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako, alisema Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa inataka kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao ni ndogo.

“Pamoja na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo ya sayansi nazo zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi na hisabati, wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.

“Kuhusu wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada ambao tutajaribu kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa shule moja. Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.

Akizungumzia suala la ubora wa elimu nchini, Profesa Ndalichako aliwataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu kwa kuwa wao ndio wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.

“Vilevile pelekeni takwimu sahihi za wanafunzi waliopo katika shule zenu kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa kuna kimbembe, yaani wakati mwingine huwa najifanya nimepoteza takwimu ya shule fulani, nikiziomba na kutumiwa, zinakuwa ni tofauti na zile za mwanzo.

“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti yenye tija,’’ alisema.
Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, waziri huyo alisema kwamba kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa vya maabara kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka vilikoagizwa.

Awali, akisoma risala ya walimu hao, Rais wa TAHOSSA, Bonus Nyimbo, aliiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka kwa ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi.

“Ili kuboresha elimu, tunaiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi tunazozikamata tunakuta mule hakuna taaluma,’’ alisema Nyimbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Molel, ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika kuendeleza elimu nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuiendeleza elimu ya Tanzania.

“Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu, wazazi, walezi na walimu, waambieni wanafunzi wasiwe na ‘expectation’ (matarajio) makubwa kwani wanapokuwa na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu wanakuwa wasumbufu,” alisema.

Wakati hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi na hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na sita na taaluma ya ualimu kwa uhakiki.

Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza kusitisha ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.

Sambamba na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa watumishi wa Serikali nazo zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa ambao walikuwa wakiingizia hasara serikali.

Visa vya ushirikina vinavyoweza kuiathari elimu Bunda


Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa wilaya zenye visa vingi vya kishirikina kiasi cha kuwaweka katika wasiwasi walimu wanao hudumu katika wilaya hiyo. Kama juhudi za dhati hazitachukuliwa Watumishi wengi wataiogopa Bunda na pengine kuihama. Viongozi wa dini,chama na serikali chukueni hatua kwa pamoja hali hii ikome. Chanzo cha Habari hii ni gazeti la Mtanzania.


WANAWAKE wanne katika Kijiji cha Kihumbu, Kata ya Hunyari wilayani Bunda, wamejeruhiwa kwa kupigwa na vitu vizito, zikiwamo fimbo, rungu, bapa za panga na katani, baada ya kutuhumiwa kumuua kwa uchawi, mwanafunzi Waryo Mseti (12).

Tukio hilo lilitokea juzi mchana katika kijiji hicho wakati mwili wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kihumbu ukisubiri kuzikwa.
Ilidaiwa kuwa baada ya Mseti kufariki dunia, wazazi wake kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hasha Hamisi, walikwenda kupiga ramli kwa mganga wa kienyeji wakidai mtoto huyo alikufa kifo cha ushirikina.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Chacha Warioba, alidai mganga huyo baada ya kufanya dawa zake, alieleza kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amechukuliwa kichawi na wanawake hao na alikuwa bado yuko hai ila walikuwa wamemficha sehemu.

“Nathibitisha ni kweli tukio hilo lipo, polisi walifika hapa kijijini na kuwachukuwa wanawake hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Bunda. Wakati tukio hilo linatokea mimi sikuwapo hapa kijijini,” alisema Warioba.

Inadaiwa kuwa Hamisi aliyewapeleka wazazi wa mwanafunzi huyo kwa mganga, aliwaeleza wenzake kuwa hata yeye aliwaona wachawi hao kwenye kioo cha maji ya mganga wa jadi.
Kauli hiyo ilithibitishwa kwa waombolezaji waliokuwapo nyumbani hapo wakati maiti ya mtoto huyo ikiwa ndani ikisubiri kuzikwa.

Baada ya kuelezwa hayo, baadhi ya waombolezaji walianza kuwasaka wanawake hao wanaotuhumiwa kwa uchawi.
Waliwakamata mmoja baada ya mwingine na kuwapeleka mlimani, huku wakiwa wamewafunga 

kamba na wakiwatishia kuwachinja. Waliwapiga na kuwataka   wamrudishe mtoto huyo.
Wanawake hao (majina tunayo), wote wakazi wa Kijiji cha Kihumbu, walisema  walifanyiwa unyama na ukatili huo unaohusisha imani za ushirikina, na hata nyumba ya mmoja wao ilimwagiwa mafuta   iweze kuteketezwa kwa moto.

“Walitupiga sana kwa fimbo, mabapa ya mapanga, rungu na katani, walituteka hadi milimani wakitulazimisha tumrudishe huyo mtoto waliodai tumemuua.
“Mimi walinilaza chini na wakaniwekea panga shingoni, eti wanichinje kama sitaki kusema ukweli. Lakini nilikataa kwamba sijui chochote,” alisema mmoja wa wanawake hao.

Wanawake hao waliokolewa na polisi waliofika katika eneo la tukio na kuwachukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi Bunda kabla yakuwapeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH).
Bado wamelazwa hospitalini hapo baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo na muuguzi wa zamu katika Wodi ya Wanawake, Daria John, alisema hali zao zinaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi, alisema wote waliohusika  kujichukulia sheria mkononi lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.


Mwalimu mmoja wanafunzi 126


Kuna upungufu mkubwa wa walimu bila kujali fani.Kuna upungufu wa walimu wa sanaa,wa biashara naSayansi pia.
Mapema Mwezi Septemba mwaka huu mkurugenzi mtendaji wa Twaweza alitangaza matokeo ya unaoeleza kuwa uwiano wa walimu na wanafunzi ni mbaya sana.Kiasi cha kufikia wanafunzi 126 kwa mwalimu mmoja.
Kwa kuwa nchi yetu bado ni maskini na elimu inatolewa katika mazingira haya bado kuna safari ndefu.Kunahitajika hatua za makusudi za kisiasa, kiuongozi, kijamii na kivitendo zaidi ili kuikomboa elimu.
Pia moja wapo ya kasumba mbaya inayoathiri elimu yetu ni kufanya mambo kisiasa zaidi badaala ya kuzingatia taaluma na tafiti.Wakati huu ilikuwa ni wakati wakutafuta majibu ya tatizo lililoibuliwa na tafiti hii.

Dar es Salaam.Taasisi ya Twaweza imefanya utafiti na kubaini kwamba mwaka 2014, mwalimu mmoja alikuwa anafundisha darasa lenye wastani wa wanafunzi 83 licha ya sera ya elimu na mafunzo kupendekeza mwalimu mmoja afundishe wanafunzi 45.
Akizindua ripoti leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema ripoti hiyo inaonyesha hali ni mbaya zaidi katika mkoa wa Manyara ambako wanafunzi 126 wanafundishwa na mwalimu mmoja.
Katika utafiti huo, amesema walitembelea shule za msingi za serikali 1,309, kaya 16,013, na kuwahoji na kuwapima wanafunzi 32,694.
Amesema katika utafiti huo, mikoa yenye wanafunzi wengi kwenye madarasa wanaofundishwa na mwalimu mmoja na idadi yao kwenye mabano ni Kigoma (108), Rukwa (100), Singida (99) na Tabora (98).
Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi (67), Lindi wanafunzi 63, Arusha wanafunzi 62, Kilimanjari 60, Iringa 59 na Pwani 56.
Eyakuze amesema katika darasa la tatu asilimia 54 tu ya wanafunzi wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.
Amesema asilimia 35 tu wanafunzi wa darasa la tatu wanaweza kufanya hesabu za darasa la pili


Fagio la Serikali lilivyosafisha sekta ya elimu

Makala hii ilichapishwa na gazeti la Mwananchi kama sehemu ya uchambuzi jinsi serikali ilivyofanikiwa na isivyofanikiwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha mwaka wakwanza. Mengi yamesemwa katika kuitathimini serikali ya awamu ya tano kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini naamini upande wa sekta ya elimu unahitaji mjadala mpana zaidi pia juhudi zinahitajika zaidi kuikomboa elimu.

Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, Rais John Magufuli amefanya jitihada kadhaa za kuboresha sekta ya elimu nchini.
Miongoni mwa jitihada hizo ni kutekeleza mpango wa utoaji wa elimu bure, unaotokana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotamka kuwa Serikali itahakikisha elimumsingi (elimu ya awali hadi kidato cha nne) inakuwa ya lazima na ya bure katika shule za umma.
Mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, mambo kadhaa yamejitokeza, huku yakihitaji uamuzi mgumu kuyashughulikia.
Kampeni dhidi ya ukosefu wa madawati
Kutokana na mahitaji makubwa ya  elimu bure, kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi, hali iliyosababisha kuwapo kwa ukosefu mkubwa wa madawati.  Mwaka mmoja wa utawala wake, Rais Magufuli akashupalia upatikanaji wa madawati shuleni.
Julai 13, Rais alizindua mpango wa ugawaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari kwa kupokea fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya kubana matumizi katika bajeti yake.
Siku ya uzinduzi alikabidhi madawati 537 kwa mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Madawati hayo 537 yalikuwa sehemu ya madawati 61,385 ambayo yalitengenezwa katika awamu ya kwanza yakifuatiwa na madawati mengine 60,000 ya awamu ya pili yakigharimu Sh4 bilioni zilizotolewa na Bunge.
Mikoa iliyofadika katika  awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5.
Alisema hali hali hiyo imesababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa na mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa.
Wanafunzi wasio na sifa
Serikali ya Awamu ya Tano na kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu, ilifanikiwa kubaini wanafunzi wasiokuwa na sifa waliokuwa wakisomea kozi maalumu ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Wanafunzi wapatao 7,800 walisimamishwa masomo na kuzua mjadala mkubwa wa kitaifa. Mwezi mmoja baadaye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitoa orodha ya wanafunzi 382 aliodai kuwa ndiyo wenye sifa.
Alisema kuwa programu hiyo ilikuwa inahitaji walimu ambao watakwenda kufundisha shule za sekondari lakini kulikuwa na wanafunzi 1,210 ambao walikuwa wanachukua stashahada ya ualimu wa shule za msingi ambao ni kinyume na malengo na 6,595 wakichukua stashahada ya kufundisha shule za sekondari.
Utumbuaji majipu taasisi za elimu
Kasi ya utumbuaji majipu ya Serikali mpya ikaikumba Tume  Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), baada ya Waziri  Ndalichako  kuwasimamisha kazi mara moja viongozi wake wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa.
Waliosimamishwa ni pamoja na Katibu Mtendaji, Profesa Yunus Mgaya ambaye Profesa Ndalichako alisema ameshindwa kusimamia kazi za Tume hiyo ikiwa na maana kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi.
Mwingine aliyesimamishwa ni Mkurugenzi wa Ithibati na Uhakiki Ubora, Dk Savinus Maronga kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu.
Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kishweko naye alikumbwa katika kadhia hiyo akidaiwa kudahili wanafunzi wasio na sifa. Pia aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Kimboka Istambuli naye alisimamishwa.
Mbali ya viongozi hao, Mwenyekiti wa  bodi ya TCU, Awadhi Mawenya naye alisimamishwa kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kuwadahili wanafunzi hao.
Kabla ya mabadiliko ya TCU, Februari  Profesa Ndalichako alisitisha mkataba wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega na kuwasimamisha kazi wakurugenzi wengine watatu, kwa madai ya ukiukwaji wa utoaji wa mikopo pamoja na ucheleweshaji usio na sababu za msingi.
Wanafunzi hewa shuleni, vyuoni
Wakati Serikali ikijihimu kupeleka fedha za ruzuku ya wanafunzi, ilibainika kuwa baadhi ya walimu walikuwa na orodha ya wanafunzi bandia kwa minajili ya kufanya ubadhirifu.
Kwa mfano,  Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Manispaa ya Arusha, zilibaini udanganyifu huo na kuchukua hatua za awali kwa kusimamisha walimu wakuu wa shule husika na pia kuziagiza mamlaka husika kuwavua uongozi walimu husika.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema katika uhakiki huo walibaini wanafunzi hewa 3,462 kutoka shule 68 za msingi na wanafunzi 2,534 kutoka shule 22 za sekondari. Katika Manispaa ya Arusha, wanafunzi 907 walibainika kutokuwapo shuleni. Mbali na shule za msingi na sekondari, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza operesheni ya uhakiki wa wanafunzi hewa wa vyuo vikuu.

Profesa Ndalichako alisema kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao majina yao yamewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, yakiwamo majina  ya wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa chuo. 
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...