Wazee wanapojitokeza kusema neno ni lazima kulitafakari na kulitendea kazi. Mzee Mkapa amesema
By Habel
Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz
Dodoma. Wakati Serikali
ikiendelea na mkakati wa kubadilisha mfumo wa elimu, Rais wa Awamu ya Tatu,
Benjamini Mkapa amesema maagizo na amri za viongozi zinazotolewa bila ya kuwa
na majadiliano, zitaitumbukiza shimoni elimu ya Tanzania.
Mbali na hilo,
Mkapa, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia,
amesema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa vyuo vikuu nchini, ni lazima iendane na
ubora wa miundombinu pamoja na bajeti ya Serikali badala ya kujaza wanafunzi
wakati hakuna fedha za kutosha na hivyo kuwa mzigo.
Mkapa alitoa
kauli hiyo jana wakati wa mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)
ambako alikuwa mgeni rasmi.
Mkuu huyo wa
Udom alisema maagizo peke yake, hayaondoi matatizo ambayo yamejitokeza katika
siku za hivi karibuni.
Alisema njia
bora ya kuboresha elimu nchini ni kwa wadau kukutana katika meza ya mazungumzo
ili wajadili changamoto zinazowakabili na kueleza nini kinatakiwa.
“Amini
nawaambia, maagizo peke yake hayaondoi matatizo tuliyonayo ndani ya elimu, bali
niwaombe wadau pamoja na wizara husika kuwa wakae meza ya mazungumzo ili
wazijadili changamoto hizo,” alisema Mkapa.
Alisema kama
maagizo yataendelea bila ya kuwepo na majadiliano elimu ya Tanzania itakuwa
imewekwa rehani na kwamba katika kipindi cha miaka michache nchi haitakuwa
kwenye ubora wa elimu kama ambavyo wengi wanadhania.
Alisema hayo
wakati kukiwa na malalamiko ya wanafunzi yanayotokana na kuondolewa kwenye
orodha ya wanaotakiwa kupata mikopo, huku wanafunzi waliokuwa wakisoma kozi
maalumu ya ualimu wa sayansi wakiondolewa na vyuo binafsi vya elimu ya juu
vikilalamikia kutopangiwa wanafunzi.
Pia serikali
ilitangaza kubadilisha upangaji wa madaraja ya matokeo ya elimu ya sekondari
kutoka mfumo wa kupanga kwa kutumia GPA na kurudisha mfumo wa divisheni.
Kwa kawaida
mgeni rasmi kwenye mahafali ya vyuo vya elimu ya juu huwa hahutubii, lakini
Udoma ilimuomba aseme machache baada ya kutunuku wahitimu.
“Katika
machache mliyotaka niseme ni pamoja na kuwataka Serikali waache kutegemea
wawekezaji, maana vyuo vyenyewe vimewekezwa. Bado nasisitiza kuwa wafanye
mikutano ya pamoja na waitane kwa haraka wazungumze bila ya kutegeana,”
alisema.
Awali
mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka alimweleza Mkapa kuwa Udom
inakabiliwa na kazi kubwa mbili ambazo ni kutopelekewa fedha kutoka Bodi ya
Mikopo pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi waliotoka Chuo Kikuu cha St Joseph
ambao wamefanya chuo kipate shida ya namna bora ya kuwasaidia kwani masomo
waliyokuwa wanasoma hayaeleweki.
Mwezi Februari,
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ilifuta hati ya usajili ya kampasi mbili za Chuo Kikuu
cha St Joseph za Sayansi ya Kilimo na Teknolojia na Chuo cha Tehama na kusema
wanafunzi 2,046 waliokuwa wakichukua shahada na stashahada wangehamishiwa vyuo
vingine.
Kuhusu
changamoto ya fedha, Mkapa alisema Bodi ya Mikopo imewakwamisha kwa kiasi
kikubwa kutokana na kutopeleka Sh6.5 bilioni ambazo ni ada ya wanafunzi katika
mwaka wa masomo 2015/16.
Mwenyekiti huyo
alisema deni hilo limeharibu taswira nzima ya Udom na kuwafanya wadau washindwe
kuwaamini katika utoaji wa huduma mbalimbali, kama kushindwa kuendelea na
mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi.
Makamu mkuu wa
chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alisema kulikuwa na jumla ya wahitimu 4,839
wa kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili, na
shahada ya uzamivu.
0 Comment to "Mkapa: Maagizo ya viongozi yanaua elimu"
Post a Comment
Post a Comment
1410