Wednesday, December 28, 2016

Hakuna elimu bora kwa wazazi wanaobweteka

Wanafunzi wengi wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo hawafanyi vizuri kitaaluma kwa sababu ya wazazi wao kutofuatilia maendeleo ya watoto wao. Wazazi wanafikiri majukumu yao ni kulipa ada na michango mengine pekee na kuwaachia walimu.


Wazazi wengi wana shauku kubwa ya kuona watoto wao wanafanya vizuri katika masomo, lakini hawako tayari kufuatilia maendeleo yao ya taaluma na hata nidhamu.

Jukumu hilo wameachiwa walimu peke yao. Na walimu wanapojaribu kuwanyoosha kinidhamu, jamii kwa upande mwingine inawanyooshea kidole na kuwalaumu.

Uzoefu unaonyesha, kwa sababu ya ugumu wa maisha wazazi wengi hawana muda wa kukagua daftari za watoto wao, kutembelea shuleni na kufanya mashauriano na walimu.

Kwa kutembelea shule, kuna mengi yanaweza kutafutiwa ufumbuzi kati ya mwalimu na mzazi, lakini hilo halifanyiki. Mzigo wote anaachiwa mwalimu ambaye hata hivyo hulaumiwa pindi matokeo yakiwa mabaya.

Tujiulize kosa la mwalimu huyu aliyeachiwa mzigo wa kusomesha na ule wa malezi ambao haumhusu. Wakati mwingine, ufaulu mdogo unatokana na wanafunzi kutokuwa na nidhamu, upi wajibu wa wazazi katika hili?

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwa Kiingereza: “It takes a village to raise a child” yaani ni jukumu la jamii au kijiji kumkuza mtoto.

Hii inamaanisha kuwa ikiwa jamii itaungana kwa pamoja kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu bora, ni dhahiri hakutakuwa na malalamiko kuhusu nidhamu mbovu na hata ufaulu usioridhisha.

Linapokuja suala la ushiriki wa jamii katika kutoa elimu iliyo bora, wazazi na walezi wanapaswa kuwa sehemu ya vikao vya maamuzi kuhusu maendeleo ya watoto wao katika shule za umma kama inavyokua katika shule binafsi.

Wazazi lazima watambue kwamba Serikali haiwezi kubeba majukumu yote kwa mwamvuli wa elimu bure, huku wakibweteka na kusubiri watoto wao wapate elimu itakayoleta mabadiliko katika maisha.

Wazazi wasiwe wapiga filimbi kuwalaumu walimu tu na kuzuia adhabu zinazotolewa na walimu kwa wanafunzi. Lazima wayaelewe mazingira wanayofanyia kazi walimu na aina ya wanafunzi walio nao.
Wanaposhindwa kutoa ushirikiano kuhusu suala zima la maendeleo ya wanafunzi, walimu nao wanakata tamaa na kuacha mambo yajiendee.

Wanasiasa na watu wenye ushawishi katika jamii lazima walielewe hili na wawe mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa wazazi wanashiriki kikamilifu katika nidhamu na maendeleo ya taaluma.

Fedha zinazotumika katika elimu bure zinatokana na makusanyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo wananchi wenyewe.

Huu ni uwekezaji usiokuwa na malengo ya kupata faida hauna maana hata kidogo. Lazima wananchi tuone kwamba fedha zetu zinazokwenda kugharimia elimu ya vijana wetu zinaleta faida.

Mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu lazima ihakikishe pamoja na mambo mengine inawajengea uwezo wakuu wa shule na walimu kuhusu njia bora za kuwashirikisha wazazi.

Tukiwaachia jukumu hili walimu na Serikali tunakua tumepoteza mwelekeo. Wazazi tuwajibike kwa kuhakikisha vijana wetu wanakua nguvukazi madhubuti kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili. Vinginevyo shule zetu zitakua vituo vya kulelea watoto kwa miaka kadhaa na baadaye watoto hao wasiwe na mchango wowote kwa maendeleo ya nchi yetu.

Wakati ni sasa kila mmoja atimize wajibu wake katika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata elimu bora.


Share this

0 Comment to "Hakuna elimu bora kwa wazazi wanaobweteka"

Post a Comment

New post Overview  Posts Pages Comments Stats Earnings Campaigns Layout Template Settings 1401 1409

Post a Comment

1410

1411 1412 1413 1414

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...