Makala hii ilichapishwa na gazeti la Mwananchi kama sehemu ya uchambuzi jinsi serikali ilivyofanikiwa na isivyofanikiwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha mwaka wakwanza. Mengi yamesemwa katika kuitathimini serikali ya awamu ya tano kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini naamini upande wa sekta ya elimu unahitaji mjadala mpana zaidi pia juhudi zinahitajika zaidi kuikomboa elimu.
Katika mwaka wake
wa kwanza madarakani, Rais John Magufuli amefanya jitihada kadhaa za kuboresha
sekta ya elimu nchini.
Miongoni mwa
jitihada hizo ni kutekeleza mpango wa utoaji wa elimu bure, unaotokana na Sera
ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotamka kuwa Serikali itahakikisha
elimumsingi (elimu ya awali hadi kidato cha nne) inakuwa ya lazima na ya bure
katika shule za umma.
Mwaka mmoja wa
Serikali ya Awamu ya Tano, mambo kadhaa yamejitokeza, huku yakihitaji uamuzi
mgumu kuyashughulikia.
Kampeni dhidi ya
ukosefu wa madawati
Kutokana na
mahitaji makubwa ya elimu bure, kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa
wanafunzi, hali iliyosababisha kuwapo kwa ukosefu mkubwa wa madawati.
Mwaka mmoja wa utawala wake, Rais Magufuli akashupalia upatikanaji wa madawati
shuleni.
Julai 13, Rais
alizindua mpango wa ugawaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari kwa
kupokea fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya kubana
matumizi katika bajeti yake.
Siku ya uzinduzi
alikabidhi madawati 537 kwa mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu kwa
niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Madawati hayo 537
yalikuwa sehemu ya madawati 61,385 ambayo yalitengenezwa katika awamu ya kwanza
yakifuatiwa na madawati mengine 60,000 ya awamu ya pili yakigharimu Sh4 bilioni
zilizotolewa na Bunge.
Mikoa iliyofadika
katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam,
Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa,
Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Rais Magufuli alisema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa
ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha
kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia
wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5.
Alisema hali hali
hiyo imesababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo
limetatuliwa kwa kiasi kikubwa na mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000
yametengenezwa.
Wanafunzi wasio na
sifa
Serikali ya Awamu
ya Tano na kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu, ilifanikiwa kubaini wanafunzi wasiokuwa
na sifa waliokuwa wakisomea kozi maalumu ya sayansi katika Chuo Kikuu cha
Dodoma. Wanafunzi wapatao 7,800 walisimamishwa masomo na kuzua mjadala mkubwa
wa kitaifa. Mwezi mmoja baadaye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Joyce Ndalichako alitoa orodha ya wanafunzi 382 aliodai kuwa ndiyo
wenye sifa.
Alisema kuwa
programu hiyo ilikuwa inahitaji walimu ambao watakwenda kufundisha shule za
sekondari lakini kulikuwa na wanafunzi 1,210 ambao walikuwa wanachukua
stashahada ya ualimu wa shule za msingi ambao ni kinyume na malengo na 6,595
wakichukua stashahada ya kufundisha shule za sekondari.
Utumbuaji majipu
taasisi za elimu
Kasi ya utumbuaji
majipu ya Serikali mpya ikaikumba Tume Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), baada
ya Waziri Ndalichako kuwasimamisha kazi mara moja viongozi wake
wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa.
Waliosimamishwa ni
pamoja na Katibu Mtendaji, Profesa Yunus Mgaya ambaye Profesa Ndalichako
alisema ameshindwa kusimamia kazi za Tume hiyo ikiwa na maana kwamba ameshindwa
kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi.
Mwingine
aliyesimamishwa ni Mkurugenzi wa Ithibati na Uhakiki Ubora, Dk Savinus Maronga
kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo
vikuu.
Mkurugenzi wa Udahili
na Nyaraka, Rose Kishweko naye alikumbwa katika kadhia hiyo akidaiwa kudahili
wanafunzi wasio na sifa. Pia aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Kimboka Istambuli
naye alisimamishwa.
Mbali ya viongozi
hao, Mwenyekiti wa bodi ya TCU, Awadhi Mawenya naye alisimamishwa kwa
kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kuwadahili
wanafunzi hao.
Kabla ya
mabadiliko ya TCU, Februari Profesa Ndalichako alisitisha mkataba wa
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega na
kuwasimamisha kazi wakurugenzi wengine watatu, kwa madai ya ukiukwaji wa utoaji
wa mikopo pamoja na ucheleweshaji usio na sababu za msingi.
Wanafunzi hewa
shuleni, vyuoni
Wakati Serikali
ikijihimu kupeleka fedha za ruzuku ya wanafunzi, ilibainika kuwa baadhi ya
walimu walikuwa na orodha ya wanafunzi bandia kwa minajili ya kufanya
ubadhirifu.
Kwa mfano,
Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Manispaa ya Arusha, zilibaini
udanganyifu huo na kuchukua hatua za awali kwa kusimamisha walimu wakuu wa shule
husika na pia kuziagiza mamlaka husika kuwavua uongozi walimu husika.
Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Ally Hapi alisema katika uhakiki huo walibaini wanafunzi hewa 3,462
kutoka shule 68 za msingi na wanafunzi 2,534 kutoka shule 22 za sekondari.
Katika Manispaa ya Arusha, wanafunzi 907 walibainika kutokuwapo shuleni. Mbali
na shule za msingi na sekondari, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza operesheni ya uhakiki wa
wanafunzi hewa wa vyuo vikuu.
Profesa Ndalichako
alisema kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao majina yao yamewasilishwa
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa
vitendo, yakiwamo majina ya wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa
chuo.
0 Comment to "Fagio la Serikali lilivyosafisha sekta ya elimu"
Post a Comment
Post a Comment
1410