Nov 23, 2013 ,gazeti la kila wiki Raia Mwema lilichapisha
makala hii, makala iliandikwa na Mrisho Gambo, miongoni mwa wanasiasa na
viongozi vijana wenye harakati nyingi chanya. Wakati anaandika alikuwa mkuu wa
wilaya ya Korogwe, huku alipigania sana maslahi ya walimu, baadaye alihamishiwa
Uvinza, Arusha na sasa ni mkuu wa mkoa wa Arusha. Ni mtu mwenye msimamo, mwenye
kukuiamini anachosema na kukiishi. Naomba niirejsehe makala yake kwa kuwa vingi
alivyosema vinasadifu changamoto za sasa za walimu kadhalika yeye ameendelea
kuwa mtetezi wa walimu.
LEO nimeona nami nianze kuweka mawazo yangu kwenye
maandishi. Japokuwa kwa sasa ni kiongozi wa serikali, naamini nafasi hiyo
haininyimi fursa ya kutoa mchango wangu wa mawazo kwa mustakabali wa taifa
langu.
Nimekuwa nakiandika kwenye mitandao ya kijamii kama facebook
pamoja na kutoa hotuba mbalimbali kwa watumishi na wananchi wilayani Korogwe.
Nimeona niandike baadhi tu ya changamoto zinazowakabili walimu kwa kuwa
nimekuwa nikijiuliza sana; mbona serikali inafanya mambo mengi kwa walimu
lakini bado kuna baadhi ya walimu wanaichukia serikali yao?
Ninaandika masuala ambayo naamini yangefanyiwa kazi walimu
wasingekuwa na manung’uniko makubwa. Sitazungumzia lile la kutaka kupandishwa
mshahara kwa asilimia 100 ambalo kwa sasa naamini halitekelezeki.
Baada ya kutafakari yote hayo nimeona niandike uchambuzi
ambao kwa kiasi kikubwa utazungumzia changamoto za kiutumishi za walimu wetu.
Kuwapandisha walimu madaraja
Hii ni changamoto inayowakabili walimu wetu Tanzania nzima.
Wakati mwingine inasababishwa na ufinyu wa bajeti ya serikali pamoja na uzembe
wa baadhi ya watendaji serikalini. Serikali mara nyingi imekuwa ikitoa
maelekezo ngazi za halmashauri lakini mara nyingi yamekuwa hayafanyiwi kazi kwa
uzito unaostahili.
Katika kipengele hiki nitatoa mfano hai, nina ushahidi
wa uzembe uliofanywa na Halimashauri ya Mji Korogwe kwenye bajeti ya mwaka
2012/2013. Walisahau kuwapandisha madaraja walimu zaidi ya 30 wa sekondari
walioajiriwa mwaka 2009.
Walimu hao walitakiwa kupanda daraja kwenye bajeti ya mwaka
2012/2013, lakini wakasahaulika kwa uzembe pamoja na serikali kutoa muongozo
kuwa watumishi wote wanaostahili kupanda daraja wapande wote.
Lakini wao wakawaweka kwenye bajeti ya 2013/2014 badala ya
2012/2013, nini tafsiri yake? Walimu hawa wataachwa nyuma kwa mwaka mmoja
kimaslahi na walimu wenzao walioanza kazi pamoja, ikiwa ni pamoja na kutolipwa
malimbikizo yao kwa sababu serikali ilikwishatoa muongozo kuwa wote wawekwe
kwenye bajeti.
Kitendo kama hiki cha uzembe wa watu wachache (mkurugenzi na
wenzake) kinawafanya walimu kuichukia serikali yao. Pia kuna malalamiko ya
walimu kushushwa madaraja bila hatia yoyote pamoja na wengine waliokuja baada
ya wao kuajiriwa, kupanda daraja na wa zamani kubaki pale pale.
Hii ni changamoto kubwa na jambo hili ni kilio cha walimu
wilayani Korogwe hadi leo. Halimashauri ya Korogwe Vijijini hawana tatizo hili
japokuwa wao wana eneo kubwa la utawala (Kilomita za mraba 3574 wakati za
halmashauri ya mji ni kilomita za mraba 212), wao walifanikiwa kuwapandisha
daraja walimu wote walioajiriwa mwaka 2009. Hili linawafanya walimu waichukie
serikali yao.
Malimbikizo ya madeni ya mshahara kwa walimu
Suala hili linahitaji kubadili mazoea katika utendaji. Kwa
mtazamo wangu serikali kuu na serikali za mtaa zote ni serikali za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Lazima halmashauri zetu zibadilike na kubeba jukumu hili
la malimbikizo ya madeni ya walimu ya mishahara na si kukusanya tu na kupeleka
serikali kuu.
Sasa umefika wakati watenge pesa kutokana na mapato ya ndani
ya halmashauri kwa ajili ya kumaliza madeni ya walimu.
Nimekuwa nikitoa mfano kuwa kama wameajiriwa walimu 30 wa
sekondari kwa ngazi ya shahada ambao mshahara wao ni 532,000 kwa mwezi
kwa kila mmoja kwa walimu wa shahada, jumla yake hapa ni shilingi 15,960,000.
Unakuta halmashauri wanalipeleka deni hilo serikali
kuu na inachukua zaidi ya miaka mitatu bila kulipwa, kumbe halmashauri
wangeweza kulipa kupitia mapato ya ndani na kama serikali kuu italeta,
halmashauri itawataka walimu walipe pole pole kwa kuwakata kwenye mishahara
yao.
Hii ni muhimu kwa kuwa utakuta mwalimu katoka Kigoma na
kupangiwa kazi Korogwe ambako hana ndugu na hakuna nyumba ya serikali ya
kufikia. Mwalimu huyu na wenzie utakuwa umewaharibu kisaikolojia na wataiona
serikali yote haina maana kwa sababu ya shilingi 15,960,000. Jambo hili lina
wafanya walimu waichukie serikali yao.
Kukosekana motisha kwa walimu wa sayansi
Kwanza naunga mkono agizo la Rais Jakaya Kikwete, pamoja na
jitihada za serikali na wananchi kujenga maabara kwa kila sekondari ya kata
nchini. Wilayani Korogwe tunaendelea kwa kasi na mchakato huu.
Jitihada hizi zitatuondolea changamoto ya upungufu wa walimu
wa sayansi mbele ya safari. Kwa sasa tunatakiwa kuwapa motisha walimu wa
sayansi kutokana na uchache wao unaosababisha kupangiwa vipindi vingi kuliko
wenzao wa masomo ya sanaa.
Mfano, kwa wiki mwalimu wa sanaa anakuwa na vipindi vinne
hadi saba, wakati mwalimu wa sayansi anakuwa na vipindi kati ya 22 hadi 30 bila
motisha yoyote. Mwalimu huyu lazima akate tamaa na ajione kama ananyonywa na
serikali yake.
Jambo hili pia linawafanya walimu wa sayansi waichukie
serikali yao. Lazima tutafakari namna ya kuwapa motisha walimu wetu wa masomo
ya sayansi. Ni dhahiri, jambo hili linawafanya walimu wa sayansi waichukie
serikali yao.
Aina ya wanafunzi wa kidato cha kwanza
Tunapeleka wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi waliopata
alama 70 chini ya 250 ambayo ni sawa na asilimia 28 ambayo ni alama D.
Mwaka huu kwenye Mock wamesema angalau alama 100 chini ya
250 ambayo ni sawa na asilimia 40 na yenyewe kwangu pia ni D, kwa sababu
nimezoea kuwa C inaanzia asilimia 41. Humu humu inasemekana wamo wasiojua
kusoma na kuandika, maana hata hesabu zenyewe ni za kuchagua, inakutosha
kuambia eti umefaulu.
Kwa mwanafunzi huyu pia mwalimu anawekewa Big Result Now
(BRN). Kama anaingia kidato cha kwanza amefeli maana kapata D, tunatarajia nini
kidato cha nne? Sisi tuliosoma teknolojia ya kompyuta tunasema kinachoingia
ndicho kinachotoka.
Tunahitaji kupitia upya utaratibu wetu wa kuwapata wanafunzi
wetu wa kidato cha kwanza. Lazima wizara iweke mikakati madhubuti kwenye jambo
hili, ili kumsaidia Rais wetu aache alama ya kukumbukwa na Watanzania kwenye
dhana ya BRN.
Mafunzo kwa walimu
Mafunzo kwa walimu ni muhimu sana. Kwenye vyuo vya ualimu
walimu hufundishwa mbinu za kufundishia, ambazo kwa mazingira ya sasa
zinahitaji kuboreshwa zaidi.
Ni vema serikali ikaliangalia vema jambo hili ili walimu
wetu waendane na mahitaji ya elimu yetu ya sasa.
Nyumba za walimu
Nyumba za walimu ni muhimu sana. Kuna maeneo mengine hata
nyumba za kupangisha walimu hakuna kutokana na mazingira yenyewe. Lazima halmashauri
itambue maeneo kama haya wakati wa kutekeleza jambo hili.
Kwenye bajeti ya mwaka huu kila halimashauri itapewa
shilingi milion 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. Fedha hizi lazima
zisimamiwe vizuri na tuachane na mambo ya wakandarasi ili tupate nyumba nyingi
zaidi jambo ambalo limechangia halmashauri zetu kuwa mchwa na shamba la bibi.
Walimu kusimamia mitihani
Kulikuwa na utaratibu uliozoeleka kwa kikundi fulani cha
walimu tu ndio waliokuwa wakisimamia mitihani. Kipindi fulani niliwahi kuuliza
hivi kuna walimu waliosomea somo la kusimamia mitihani kiasi ambacho wengine
wanakosa sifa hiyo?
Kama vigezo ni kuwa kazini miaka mitatu na kuwa na TSD namba
pamoja ma vigezo vingine, sasa kwa nini kila mwaka wajirudie hao hao? Jambo
hili linafanya walimu waichukie serikali yao.
Walimu kulipia vitambulisho vya kazi
Kumekuwa na utaratibu wa kuwalipisha walimu shilingi 2,000
kwa ajili ya vitambulisho, kitambulisho ni mali ya mwajiri ambaye ni serikali.
Kuwalipisha walimu ni kinyume cha utaratibu. Halimashauri zimekuwa
zikiwachangisha walimu wetu.
Nauliza, mbona vitambulisho vya taifa ni gharama zaidi
lakini serikali inatoa bure? Jambo hili linawafanya walimu waichukie serikali
yao.
Walimu kulipia ujazaji wa fomu za OPRAS
Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya halmashauri nchini
kuwataka walimu walipie gharama za photocopy za fomu za Opras. Fomu hizi ni
mali ya serikali kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa watumishi. Kumlipisha
mwalimu kwa ajili ya fomu hizi ni kinyume cha utaratibu. Jambo hili linawafanya
walimu waichukie serikali yao.
Uhaba wa vitendea kazi
Hapa serikali inastahili pongezi maana imefanya kazi kubwa
kwa upande wa vitabu. Jitihada zinatakiwa ziongezeke kwenye upande wa ofisi za
walimu na maeneo mengine.
Nimegundua mambo kama haya ambayo yapo ndani ya uwezo wa
serikali yanachangia kuongeza chuki kwa walimu dhidi ya serikali yao. Umefika
wakati sasa wa kuwachukulia hatua za makusudi watumishi wote wanaoikwamisha
serikali na watumishi wenzao, kwa sababu kila mwaka changamoto zimekuwa ni
zilezile.
Sasa kwenye elimu tunazungumzia (Big Results Now- BRN –
(Matokeo makubwa sasa), lakini kwa kweli bila kuangalia maslahi ya walimu
itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
BRN kwenye elimu ni zaidi ya mjadala wa daraja sifuri
(division 0) na daraja la tano (division 5) kwenye jamii yetu. BRN naikubali
kwa asilimia 100, baadhi ya watendaji wa serikali tusikubali kuipotosha dhana
hii nzuri kwa wananchi na kudhoofisha juhudi za serikali yetu, badala yake
tujielekeze kwenye matatizo ya msingi ya walimu wetu.
Mwandishi wa makala hii, Mrisho Gambo ni Mkuu wa Wilaya
Korogwe(sasa mkuu wa Mkoa wa Aruusha), mkoani Tanga na msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu:
+255766757575. barupepe; mrishogambo@gmail.c
)
0 Comment to "MRISHO GAMBO: KWA NINI WALIMU WANAICHUKIA SERIKALI"
Post a Comment
Post a Comment
1410