Katika kuboresha na kurasmisha
elimu Baraza la Mitihani limetangaza kutumia namba moja ya mtihani kwa ngazi
zote za elimu. Ni babadiliko yenye tija. Chanzo ni Gazeti la Mwananchi
Kuanzishwa kwa mfumo wa namba maalumu ya
usajili itakayotumiwa na wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi chuo ngazi ya
diploma, kutasaidia kupunguza tatizo la wanafunzi hewa.
Hayo yalitangazwa
jana na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mitihani wa
Necta, Khalifan Kabiki alisema utaratibu huo unafuta uliokuwa unatumika zamani
ambapo mwanafunzi alipewa namba mpya kila alipofanya mtihani.
Mfumo mpya,
utamtambua mwanafunzi kwa namba atakayosajiliwa nayo darasa la kwanza ambayo
ataitumia katika maisha yake yote ya shule na taarifa zake zote zitakuwa humo.
Kabiki alisema
mfumo huo ambao utakuwa wa kielektroniki, utasaidia uandikishaji wa wanafunzi
wa darasa la kwanza kwa kutoa namba maalumu itakayomtambulisha mwanafunzi
katika ngazi mbalimbali za mafunzo.
“Mfumo huu
utasadia katika uandaaji na utoaji wa takwimu za wanafunzi katika ngazi ya shule,
wilaya, mkoa na Taifa. Pia utarahisisha ufuatiliaji wa taarifa za matokeo ya
kila mwanafunzi ili kuhakikisha wadau wa elimu wanapata ufahamu wa kutosha
kuhusu ufundishaji na ujifunzaji,” alisema Kabiki.
Pia, mfumo huo
utasaidia katika uhamisho wa mwanafunzi ndani na nje ya mkoa, kwani namba hiyo
itakuwa ina taarifa zake zote muhimu na hakutakuwa na haja ya vielelezo
vingine.
Kabiki alisema
tayari mfumo huo umeanza kujaribiwa katika mikoa ya Mwanza na Ruvuma, na
ifikapo Desemba utaimarishwa zaidi ili kuanzia Januari uanze kutumika nchi
nzima.
Katika hatua
nyingine, ofisa habari wa baraza hilo, John Nchimbi alisema Necta imeboresha
mfumo wa usahihishaji mitihani ya Taifa kwa kuweka wasahihishaji kulingana na
idadi ya maswali kwa kila somo.
Pia, Necta walisema
wameimarisha udhibiti wa wizi wa mitihani na udanganyifu kwa kipindi cha miaka
minne, kuanzia mwaka 2011 hadi 2015.
“Usahihishaji wa
sasa unatumia mfumo wa mnyororo kuepuka baadhi ya wasahihishaji kumkosesha
mwanafunzi swali ambalo amelijibu kwa ufasaha kwa kuwa tu maswali
yaliyotangulia alikuwa hajayajibu vizuri,” alisema.
Alisema mfumo wa
kudhibiti wizi wa mitihani na udanganyifu umeimarishwa kutoka watahiniwa
wadanganyifu 9,736 mwaka 2011 mpaka sifuri mwaka 2015 kwa elimu ya msingi.
Kwa kidato cha nne
wanafunzi 3,303 walifanya wizi na udanganyifu huo kwa mwaka 2011 lakini idadi
hiyo imepungua mpaka wanafunzi 87 mwaka 2015.
Nchimbi alisema
mfumo huo umepunguza wizi na udanganyifu kwa wanafunzi wa kidato cha sita
kutoka 11 mwaka 2011 mpaka tano mwaka 2015.
0 Comment to "Wanafunzi kutumia namba moja ya mtihani katika kila ngazi ya elimu"
Post a Comment
Post a Comment
1410