Mr.Mwalimu. Blogspot.Com
Si dhambi, si kosa la jinai wala si utovu wa nidhamu kwa
mtumishi wa umma au mwalimu kugoma kutii maagizo ya muajiri au mkuu wake wa
kazi pale maagizo hayo yanapokuwa yamekiuka sheria za kazi, haki za binadamu au
yanapokuwa na dalili za udhalilishaji.
Ni wajibu na ni lazima kwa kwa mtumishi wa umma kutii
maagizo ya muajiri au mkuu wake wa kazi, lakini hayo maagizo lazima yawe
hayakinzani na sheria na taratimu za kazi na utumishi wa umma. Si haki wala
vema kwa muajiri au mkuu wa kazi kutumia madaraka yake vibaya kwa kutoa maagizo
au maalekezo ambayo yanakinzana na haki na taratimu za kazi.
Muajiri au mkuu wa kazi hayupo juu ya sheria za nchi, hana
kibali cha kuvunja sheria za kazi, haruhusiwi kusigina sheria za utumishi wa
umma wala hana ruhusa ya kukiuka haki za binadamu. Cheo ni dhamana, hakimpi mtu
ruhusa wala mamlaka ya kumdhalilisha mtu wa chini yake, hakimpi mtu haki ya
kudhalilisha utu wa binadamu.
Niliposoma kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna mwalimu
ameamuriwa kudeki darasa na mkurugenzi wa halmashauri mbele ya wanafunzi,
nilikataa kuamini, nilisema huu utakuwa ni uzushi tu au utani wa mitandaoni.
Mpaka nilipojitahidi kuwasiliana na mtu mmoja wa halmashauri husika
nikahakikishiwa kuwa ni ukweli.
Nikaketi chini kutafakari, nikakumbuka tukio la mkuu wa
wilaya mmoja kanda ya ziwa hiyo hiyo kuwacharaza viboko walimu, nikakumbuka
matukio kadhaa ya walimu kupigwa vibao na wakuu wake wa kazi likiwemo la
mwishoni mwa mwaka jana mkoani Dodoma.
Nikakumbuka shuhuda
za baadhi ya walimu jinsi wanavyoshambuliwa kwa lugha chafu na maneno ya kuudhi
na wakuu wao wa kazi katika halmashauri, nikatafakari madai ya walimu
yanavyopuuzwa, kisha nikatafakari wanaofanya hivyo nao walifundishwa na walimu
hawa hawa wanaowadhalilisha leo. Nikahitimisha kwa huzuni nyingi kuwa ni kweli
tenda wema nenda zako.
Nikiri kauli ya Rais
wa chama cha walimu ,Gration Mkoba, wakati akihojiwa na gazeti la Raia mwema
katika siku ya mwalimu duniani, alisema ualimu ni “kazi ya kitume”.Ni kazi ya
kutenda wema na kwenda zako usingoje shukrani, fundisha kwa moyo lakini
usitegemee malipo sawia wala heshima sawia. Wengine utawafundisha watakudekisha
kesho na wengine watakukumbuka kwa wema na baadhi utafundisha watalitumikia
taifa vizuri hata utajivunia.
Kwa kweli baada ya kutafakari sana nikajikuta inanijia picha
ya walimu wakiwa wamepigishwa magoti na mkuu wao wa kazi! Usishangae, ndiyo
kitu ambacho nakiona kikimtokea mwalimu huko tuendako. Kama mwalimu anachapwa
viboko, anapigishwa magoti na anapewa adhabu ya kusafisha darasa basi mwalimu
ajiandae kupigishwa magoti ofisini kwa afisa elimu, mkurugenzi au kwa mkuu wa
wilaya!Wasomaji wa Mr.Mwalimu.blogspot.com ,hadhi ya walimu iko mashakani!
Vitendo tunavyovishuhudia sasa kutokana na kukua kwa
teknolojia ya mawasiliano na habari ni vichache kati ya vingi ambavyo walimu
wanatendewa hasa maeneo ya ndani ndani. Mengi hayaripotiwi lakini yanatokea, ukihoji
walimu utasimuliwa mengi ambayo hutaamini.
Ni kwa bahati mbaya sana vitendo vya kidhalilishaji kama
kuchapwa viboko, kupigwa makofi, kutamkiwa maneno machafu na
kudekishwa,wanatendewa walimu tu, walimu ambao ndiyo asilimia zaidi ya sabini
ya watumishi wa umma ndiyo wahanga wakuu wa vitendo vya udhalilishaji. Na ni
walimu ndiyo waliofundisha hao wanaodhalilisha walimu sasa.
Kwa kuwa vitendo vya kudhalilisha walimu vinaongezeka,
vinazoeleka, vinaanza kuwa ni vya kawaida kiasi kwamba mwalimu anaanza kupewa
hadhi ya mwanafunzi kwamba ni mtu wa kuadhibiwa pale anapokosa. Na kwa kuwa
Chama cha walimu hakina hatua za zaidi za kuchukua dhidi ya vitendo hivi zaidi
ya kumtaka mdhalilishaji aombe msamaha na kutoa tamko la kimaneno la kupinga
vitendo hivi.
Kadhalika kwa kuwa vitendo hivi havijawahi kukemewa
hadharani na waziri yoyote anayehusika na elimu au hata katibu mkuu wa wizara
inayohusika na elimu, naomba mwalimu achukue hatua. Pamoja na hilo niviombe
vyama vya walimu kote nchini, viache
ukasuku, visiishie tu kudai madai ya walimu, visihishie tu kudai nyongeza,
visiishie tu kukata asilimia mbili ya mishahara ya walimu. Vitoe elimu ya
kujitambua kwa walimu. Vifundishe walimu haki zao kama watumishi wa umma na kama
wafanyakazi. Hivi kuna faida gani kuwa mwalimu ambaye unalipwa vizuri lakini
huna hadhi, unadhalilishwa kila siku?
Heshima ya mtu inalindwa na mtu mwenyewe, hadhi ya mwalimu
italindwa kutetewa na mwalimu mwenyewe. Mwalimu usingoje CWT wakutetee haki
yako unao uwezo wa kujitetea mwenyewe. Simama imara na jiamini. Nasema mbele za
Mungu ingekuwa ni mimi mkurugenzi amenipa amri ya kudeki ningesimama kumtaza
usoni tu bila kumjibu kitu.
Hata angerudia amri hiyo mara kumi nisingetii, bali
ningebaki kumtiza bila wasiwasi wala kuogoba, ningemtazama usoni kwa heshima
zote kwa kuwa ni mkuu wangu wa kazi , nisingemuonyesha sura ya dharau, wala
nisingekimbia lakini nisingetafuata ndoo ya maji wala tambala la kudekia
liliko. Kutii kila maagizo unaweza jikuta una tii maagizo ya mtu aliyelewa, alafu
wewe ukabaki kudhalilika na akili zako timamu.
Binafsi najiuliza maswali mengi sana, Nchi hii imepita
mikononi mwa marais wa tano mpaka sasa, sijawahi sikia marais hao katika zama
zao waliwahi kumdhalilisha mkuu wa mkoa, mkurugenzi wa shirika la umma , mkuu
wa wilaya, mkurugenzi wa halmashuri wala mkuu yoyote wa idara fulani. Sasa hawa
wanaodhalilisha walimu wanatoa wapi ujasiri huo wa kufanya mambo ambayo hata
Rais mwenyewe hafanyi?
Kuna wakati na mazingira ambayo mtu ukitendewa udhalilishaji,
wewe uliyedhalilishwa ndiye unakuwa unastaahili kulaumiwa. Kukubali kuonewa si
utii, ni nidhamu ya woga ambayo haina faida. Fikiri kama yule mwalimu angegoma
kudeki lile darasa na akaripoti ngazi za juu ingetokea nini.
Nasema wazi mwalimu
aliyekubali kudekishwa mbele ya wanafunzi alikosea sana na ni dalili kuwa
wafanya kazi wengi wa umma hasa walimu hatujui haki zetu. Ndiyo maana hatusikii
wauguzi, madaktari, maaskari, maafisa maendeleo, mabwanamifugo wala wahasibu
wakifanyiwa hivyo vitendo hivyo bali walimu tu ndo wanaofanyiwa hivyo.
Mwalimu una haki ya
kukataa kutii maagizo ya mkuu wako wa kazi au muajiri wako kama unaona
amekusudia kukudhalilisha. Mwalimu
fahamu una sheria zinazokulindwa, usikubali kupelekwa pelekwa kama roboti.
Kuonewa au kudhalilishwa mara moja si mbaya ile kuendelea
kudhalilishwa ni uzembe. Mtetezi wa kwanza wa taaluma ya ualimu, utu wa
mwalimu, na haki za mwalimu ni mwalimu mwenyewe. Kinyume chake naweza sema adui
wa kwanza wa utu na hadhi ya mwalimu ni mwalimu
mwenyewe, taaluma ya ualimu itetewe na walimu wenyewe.
Mwalimu lazima utambue kuwa hakuna mtu kutoka nje ambaye
atakutetea kwa kiwango kikubwa kama ambavyo unaweza kujitetea wewe mwenyewe.
Bila kujitetea wenyewe hadhi ya walimu na ualimu itashuka kila leo na visa vya
udhalilishaji vitaongezeka kama tunavyosikia kiasi cha kuanza kuzoeleka kuwa
walimu ni kawaida kutendewa vibaya.
MZIZI WA ELIMU NI MWALIMU. MWALIMU KATAA KUDHALILISHWA.MR.MWALIMU.BLOGSPOT.COM ELIMU KWANZA.
0 Comment to "BAADA YA BAKORA, KUPIGWA VIBAO NA KUDEKISHWA ,MWALIMU AJIANDAE KUPIGISHWA MAGOTI!"
Post a Comment
Post a Comment
1410