Sunday, October 30, 2016

MWAKA MMOJA: JPM ALIVOIPANDISHA NA KUISHUSHA ELIMU.



Mwaka mmoja wa utawala wa serikali ya awamu ya tano hauwezi kupita bila kufanyiwa tathimini ya kina jinsi alivyoenenda kadiri ya ahadi alizoahidi, kadiri ya ilani ya chama chake katika uchaguzi na kadiri ya alivyoshughulikia changamoto za wananchi.

Mafanikio na madhaifu ya serikali hii yapimwe kwa kutathimini jinsi ilivyoshughulikia kero sugu za wananchi, jinsi ilivyotekeleza ahadi na ilani yake ya uchaguzi, kadhalika tathimini ijielekeze kwenye ubunifu na utayari wa serikali kushughulikia kero mpya na za dharura.

Tathimini yangu juu ya serikali ya awamu ya tano, itajikita katika kuitazama sekta ya elimu. Sera ya elimu bure ndiyo eneo ambalo jicho langu litajikita zaidi. Sera ambayo imeipaisha sana serikali ya awamu ya tano kiasi hatuwezi kutathimini mafanikio ya awamu ya tano bila kujadili mafanikio ya utekelezaji wa sera ya elimu bure. Utekelezaji wa sera hii kwa vitendo umechangia mafanikio yafuatayo kama Mr.Mwalimu Blog inavyofafanua:

Idadi ya wanafunzi kwa ngazi ya awali, msingi na sekondari imeongezeka kwa kasi. Kwa kweli kama kuna mafanikio ya wazi ambayo serikali ya awamu ya nne imepata basi ni kuongeza idadi ya wanafunzi mashuleni. Watoto waliokosa elimu kwa sababu ya ufukara sasa wana matumaini ya kupata elimu.

Utengenezaji wa madawati umeboresha mazingira ya usomaji. Rais Magufuli amejitahidi sana kushughulikia suala la wanafunzi kukaa chini kutokana na ukosefu wa madawati. Ukosefu wa madawati  umeathiri sana mazingira ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi.

Mtoto anayekaa chini wakati anafundishwa na watoto watano waliobanana kwenye dawati moja ambalo hukaliwa na watoto wawili hawezi kuelewa vizuri anachofundishwa.  Awamu ya tano imepigana vita na imeshinda kiasi kikubwa sana vita hii dhidi ya watoto kukua chini. Eneo hili ni eneo ambalo pia serikali inapaswa kupongezwa waziwazi.

Serikali ya awamu ya tano imerejesha uwajibikaji wa watumishi wa umma. Si siri nchi imepita kwenye mpito cha uharibifu wa maadili ya utumishi wa umma na sasa Rais Magufuli na serikali yake wapo kwenye kipindi cha mpito cha kurejesha maadili na uwajibikaji wa watumishi wa umma.

Hili Rais pia kwa kiasi kikubwa amefanikiwa, watumishi wanaheshimu kazi na wanawajibika hivyo walimu kama sehemu ya watumishi wa umma, upepo huu wa matengenezo unawakumba pia. Walimu wengi sasa wanahudhuria katika vituo vyao vya kazi na wanawajibika. Haya ni mafanikio ya kujivunia na kupongezwa ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja.

Ulipaji wa posho za madaraka kwa wakuu wa shule, walimu wakuu na waratibu wa elimu. Serikali imetekeleza moja ya dai la muda mrefu la walimu kutaka kuwepo na posho ya madaraka. Katika kuanza kutekeleza dai hilo, serikali imeanza kuwalipa wakuu wa shule posho ya madaraka ya shilingi 250000, walimu wakuu shilingi 200000 na waratibu shilingi 250000. Haya ni mafanikio yanayoweza kuchagiza kiwango cha elimu. Ni mafanikio kwa sababu wakuu hawa watajituma zaidi na watawawajibisha zaidi walio chini yao.

Kama wasemavyo waswahili penye mafanikio hapakosi changamoto, jitihada zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa ili kuboresha elimu hazijafanikiwa kwa kwa asilimia mia. Hizo Mr.Mwalimu Blog, tunaziita changamoto kwa sababu zinaweza kutatuliwa, si mambo yaliyoshindikana kabisa bali ni mambo tu yanayohitaji dhamira ya kweli katika kuyashughulikia:

Changamoto kuu katika kipindi cha mwaka mmoja cha awamu ya tano ni uhaba wa walimu. Uhaba wa elimu ni miongoni mwa sababu kubwa sana inayodhoofisha elimu yetu. Mathalani katika shule ambayo nafundisha, shule imeanza mwaka 2013 hivyo mwaka huu inatoa wanafunzi wa kwanza wa kidato cha nne lakini Tangu imeanzishwa haijawahi kuwa na mwalimu wa somo la Fizikia!

 Katika miaka minne ya kuwepo kwake imekuwa na walimu wa Baiologia na Kemia kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu pekee. Kutoajiri walimu. Licha ya changamoto walizo kabiliana nazo, kitendo cha serikali ya tano kutoaajiri mwaka 2016 kimeathiri sana elimu. Uhaba wa walimu uliopo ungepungua kama serikali ingeajiri walimu mapema  mara tu baada ya kuhitimu vyuo badala ya kuwaacha waranderande mtaani.

Sera ya elimu bure imetengeneza hali ya kubweteka kwa wazazi, baada ya kutangazwa elimu bure wazazi wengi sasa wanafikiri kila kitu kitafanywa na serikali. Wazazi wengi wasio na uelewa wamejitoa kwenye nafasi zao za kuwawezesha vijana wao, kuwahamasisha kusoma, jukumu hilo wamewaachia walimu. Hivyo elimu ni bure lakini watu hawana msisimko wa kusoma na kusomesha. Ni kama sera hii ya elimu bure imewafanya baadhi ya wazazi kuwa kupe.

Sera ya elimu bure imeathiri utoaji wa elimu, ubora wa elimu na uendeshaji wa shule hivyo kuathiri ubora wa elimu. Kila mwezi Serikali inatoa kiasi fulani cha fedha kufidia ada ambayo ilikuwa inatozwa kwa wanafunzi. Uendeshaji wa shule ambao ulikuwa ukitegemea sana michango ya wanafunzi, sasa unategemea ruzuku na fidia ya ada. Kwa kiasi kikubwa elimu bure imenufaisha wazazi au walezi lakini imeathiri uendeshaji washule na ubora wa elimu.

Kupitia michango ya wanafunzi, shule ambazo hazina walimu wa baadhi ya masomo hususani yale ya Sayansi ambayo yana uhaba mkubwa, shule ilitumia fedha ya taaluma iliyokuwa ikichangwa na wanafunzi kuajiri walimu wa muda. Hivyo pia shule nyingi za msing  zilitumia walimu wengi wa kibarua cha muda kufundisha madarasa ya juu na hata darasa la awali. Shule ziliweza kufanya mitihani yenye ubora kwa kuwa fedha zilikuwepo.

Kwa sababu fedha za ruzuku na fidia ya ada hutolewa kwa shule kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo au waliosajiliwa na shule husika, shule nyingi zinakabiliwa na ukata kutokana na kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi. Fedha inayopatikana inaruhusu kufanya mahitaji madogo madogo ya shule kama chaki, vitabu, na zana zingine za kujifunzia.

 Hali ni mbaya sana katika shule nyingi, baadhi ya shule zimefikia kushindwa kuchapa mitihani, wanafunzi wanaandikiwa mitihani ubaoni. Hii  hali ambayo ipo na haisemwi sana lakini ina athari kubwa. Serikali itizame upya kiwango cha fedha inachotoa mashule ili kiweze kukidhi mahitaji ya uboreshaji wa elimu.

Kuweka vigezo vipya vya kujiunga na chuo kikuu kumeminya pia mawanda ya elimu kukua. Nchi hii inawasomi wachache sana, sasa inapotokea vinawekwa vigezo vya kubana zaidi ili watu wasipate elimu ya chuo kikuu lazima ishangaze. Alama za kujiunga na chuo kikuu kwa wanafunzi waliotoka moja kwa moja kidato cha sita ni wastani wa D mbili au alama nne kutoka E mbili au alama tatu za awali.

Wizara ya elimu imetangaza vigezo hivyo mwaka huu na imedahili wanafunzi wa mwaka huu kwa kutumia utaratibu huo. Kanuni hizi mpya, ngumu na za ghafla zimeathiri ndoto za watu wengi kujiendeleza. Serikali imechukua maamuzi haya haraka ilipaswa itoe maamuzi haya mwakani au ingetangaza mwaka huu lakini yangeanza kutekelezwa mwakani ili watu wajiandae.

Ni hivyo pia watu wanaotaka kujiunga na chuo kikuu kwa cheti cha stashahada, sasa itabidi angalau wawe na ufaulu wa kuanzia daraja la 3. Bado maamuzi haya yanaathari hasi kwa watumishi waliopanga kujiendeleza mwaka huu. Mathalani walimu na wauguzi ni wahanga zaidi kwani wengi kutokana na mfumo wa elimu zao wengi huhitimu ngazi za stashahada wakiwa na chini ya daraja la tatu.

Wanafunzi wa kidato cha nne nao hawako salama, sasa daraja C linaanzia 45 kutoka 41 ya awali, daraja B linaanzia 65 kutoka 61 ya awali, Daraja A limeshushwa sasa litaanzia 75 mpaka 100. Ni jambo jema kwa uboreshaji wa elimu yetu lakini litaumiza watoto wetu hasa wanyonge. Watoto waliopandishiwa madaraja tukumbuke ni hawa ambao hawana walimu, hawana maabara, hawana maktaba, wanasoma kwa kukaa chini.

Kabla ya kupandisha madaraja serikali ilipaswa iboreshe kwanza mazingira ya utoaji elimu na ufundishaji ndipo mabadiliko haya yangekuwa na tija. Vinginevyo kuwapandishia madaraja wanafunzi ambao hawana walimu, maabara wala maktaba kadhalika hawana vitabu ni dhuluma. 

Wahanga zaidi wa mabadiliko haya ni watoto wa shule za kata, ambao walikuwa wanapata 41,42,43,44 na hivyo kujikuta wana daraja C leo wengi wanaoangukia hapo watajikuta wana D.
Kutoongeza mishahara kuna athari hasi. Licha Serikali ya awamu ya tano kurejesha ni dhamu ya kazi kwa watumishi hususani walimu kwa kiwango kikubwa, lakini kutowaongezea walimu mishahara kumenyong’onyeza sana mioyo ya walimu na kumevunja moyo wa uwajibikaji wa dhati.

Uwajibikaji uliopo hivi sasa kwa walimu ni wa woga tu. Walimu wengi wanawajibika kwa kuhofia kuchukuliwa hatua za kisheria lakini uwajibikaji kutoka ndani ya moyo wa mwalimu umepungua. Hali hii imetokana na mazoea ya walimu kuongezewa mishahara kila ifikapo mwezi wa saba kadhalika walimu walikuwa na matumaini makubwa sana na Rais wao kuwa awamu hii kulingana na ahadi zake angeboresha sana maslahi ya wafanyakazi. Kitendo cha kutoongezewa mishahara mpaka sasa kina athari, hivyo hii ni moja ya kasoro ya serikali ya awamu ya tano katika kuboresha walimu.

Mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu bado hali si shwari. Manung’uniko ni mengi kutoka kwa vijana wa vyuo, kinachoendelea kinakinzana kabisa na ahadi za Mh. Rais Magufuli wakati wa kampeni zake, ni kama ilikuwa ahadi ya kisiasa tu ili kujipatia kura kama ilivyoada ya wanasiasa wengi kutoa ahadi nyingi wasizoweza kutekeleza. Ubaguzi katika utoaji wa mikopo ni ukandamizaji wa wanyonge kwa kuwa sehemu kubwa ya wanufaika wa mikopo hii ni wanyonge.

Ukitoa mikopo kwa ubaguzi maana unawanyima wanyonge nafasi ya kujiendeleza, ukiwanyima nwanyonge nafasi ya kupata elimu basi unatengeneza tabaka katika jamii. Tabaka la wenye nacho na wasionacho.

Mr.Mwalimu Blog tunasema, ELIMU KWANZA. Elimu lazima kiwe kipaumbele cha kwanza katika nchi maskini kama Tanzania. Maendeleo yote ya kimiundombinu, kimawasiliano lazima yatangulie na maendeleo ya kielimu. Kuwa na nchi yenye barabara za lami mpaka uchochoroni lakini kuna watu wengi wasiojua kusoma na kuandika na kasoro.

Kadiri ya tafiti zaidi ya asilimia ishirini humaliza shule za msingi bila kujua kusoma na kuandika. Zaidi ya asilimia hamsini ya wanafunzi wakidato cha nne humaliza shule wakipata madaraja dhaifu yasiyowawezesha kuendelea. Pia walimu katika shule nyingi wanafundisha katika mlundikano mkubwa wa wanafunzi .Hizi ni changamoto za msingi ambazo serikali hii inapaswa itatue.

Share this

0 Comment to "MWAKA MMOJA: JPM ALIVOIPANDISHA NA KUISHUSHA ELIMU."

Post a Comment

New post Overview  Posts Pages Comments Stats Earnings Campaigns Layout Template Settings 1401 1409

Post a Comment

1410

1411 1412 1413 1414

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...