Kama nilivyodokeza awali kila mwaka
mitihani ya kitaifa inapofanyika lazima kuwepo na viashiria vya wizi wa mtihani
huo. Hii ni matokeo ya kuwa na walimu,wanafunzi ,wazazi na jamii ambayo
inaamini kuna njia ya mkato ya mafanikio katika maisha na katika elimu.
Tunapaswa kubadili mtazamo na
kutambua kuwa sasa ni wakati wa kufanya kila kitu kwa njia sahihi bila mawaa.
Wanafunzi asome kwa bidii asitegemee kuwa atafaulu kwa kuvujisha mtihani.
Hivyo mwalimu asitegemee kufaulisha
kwa kuvujisha mtihani bali afanye kazi kwa bidii sifa ije kwa haki. Watu
wafanye kazi za haki na halali ili kujipatia kipato na si kubumba mitihani feki
ili wapate fedha. Wazazi wawasaidie watoto kusoma kwa bidii si kuwasaidia kuiba
mitihani.
Habari ifuatayo imeripotiwa na
Gazeti la Mtanzania, tukumbuke watu hawa wanatuhumiwa kuvujisha mtihani feki
,ni watuhumiwa bali haijathibitishwa na vyombo vya usalama kuwa ni wao kweli
walitenda kosa. Mr.Mwalimu Blog inaibandika hapa habari hii kama onyo na kama
sehemu ya kuwa kumbusha wasimamizi wa mitihani kuwa wawe makini.
MWALIMU wa Shule ya Sekondari
Hasanga, iliyopo wilayani Mbozi mkoani Songwe na wafanyabiashara wawili,
wanahojiwa na vyombo vya usalama mkoani Mbeya kwa tuhuma za kuhusika na
utengenezaji wa mitihani feki ya kidato cha nne.
Watuhumiwa hao, James Kapinga (36)
ambaye anadaiwa kufanya kazi Shule ya Sekondari ya Hasanga pia anajitolea
kufundisha Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Sangu, Baraka Mwazambe (28),
mfanyabiashara na mkazi wa Tunduma na mtaalamu wa masuala ya Tehama (IT), Alex
Mochi.
Watu hao kwa pamoja inadaiwa
walikamatwa juzi usiku baada ya mwanafunzi mmoja ambaye jina lake na la shule
vimehifadhiwa kukutwa na mtihani wa somo la Kiingereza na alipobanwa, inadaiwa
aliwataja wahusika hao.
“Mwanafunzi huyu ni wa shule
nyingine tena si ya Mbeya, alikutwa na mtihani feki wa somo la Kiingereza,
alipohojiwa alieleza mtihani huo ulitoka Mbeya na Serikali ilipofuatilia
iliwabaini wahusika ambao walikuwa wanasambaza mitihani feki,” kilisema chanzo
kimoja cha habari hii.
Akizungumzia sakata hilo, Katibu
Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alikiri ofisi yake kupokea taarifa
juu ya uvujaji wa mitihani na walipofuatilia walibaini mitihani hiyo ni feki.
“Mbeya hakuna mitihani iliyovuja
kama inavyoelezwa katika mitandao, ukweli ni kwamba suala hilo lilifuatiliwa
ilibainika mitihani inayosambazwa si ile iliyochapishwa na Baraza la Mitihani
la Taifa, ni feki na baadhi ya wahusika wanahojiwa na vyombo vya dola,”
alisema.
Naye Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa
Mbeya, Benedict Sandy, alisema hakuna mitihani iliyovuja.
“Mitandao imekuwa ikitoa taarifa za
upotoshaji eti mitihani imevuja, mitihani iliyosambaa na kukutwa na baadhi ya
wanafunzi tena si wa Mkoa wa Mbeya ni feki na wahusika wanaodaiwa kuisambaza
wamekamatwa.
“Nawaomba wanafunzi wazingatie yale
waliyofundishwa, mitihani hiyo inakuja kwa lengo baya la kuwapotezea muda wao
na mwisho wa siku kuishia kufeli, watu wanaofanya kazi hiyo wapo kimasilahi,”
alisema.
MTANZANIA lilizungumza na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, ambaye alisema msemaji wa taarifa
hiyo ni ofisi ya elimu mkoa.
“Hili ni suala la elimu na msemaji
ni ofisa elimu mkoa, polisi hatuwezi kulisemea neno lolote, ninawashauri
mumtafute ofisa elimu alitolee ufafanuzi suala hilo,” alisema.
0 Comment to "Watuhumiwa kuvujisha mtihani kidato cha nne"
Post a Comment
Post a Comment
1410