Bado taifa hili lina watu wanaofikiri vizuri kiasi cha
kuweza kutoa mawazo ya kuiendeleza nchi. Tunapaswa kujivunia watu hao wenye
vipawa vya kufikiri na wenye ujasiri wa kuweka mawazo yao wazi kwa maslahi
mapana ya nchi.
Mwandishi wa makala hii ni miongoni mwa watu hao.
Makala hii iliandikwa na mwanasafu maaru na mkongwe wa
gazeti la Raia Mwema,Gidion Shoo na kuchapishwa na gazeti hilo.
VIWANDA. Viwanda. Viwanda. Hilo ndilo neno kuu vinywani mwa
Watanzania. Hii ni ndoto nzuri. Kila mmoja aipendaye nchi hii anaipenda kuiota
na kila mmoja anachora taswira yake ya Tanzania ya viwanda.
Wapo wanaoiona Tanzania ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ya makundi ya wafanyakazi wakisubiri mabasi yaliyoandikwa Urafiki, Kiltex,
Sunguratex na kadhalika ili kwenda kazini kuingia shifti na kuwapatia wenzao
fursa ya kurejea nyumbani baada ya kumaliza ngwe yao ya uzalishaji kiwandani.
Ilikuwa Tanzania ya Azimio la Arusha. Azimio lililokuwa chachu ya mapinduzi
katika kila nyanja ya uzalishaji mali nchini.
Hali kadhalika wapo wanaoiona Tanzania ya viwanda vya kisasa
zaidi ambavyo havihitaji nguvu kazi kubwa sana lakini vinazalisha zaidi
kutokana na teknolojia ya kisasa ambayo imetawala katika uchumi wa viwanda kote
duniani.
Zote hizo ni ndoto nzuri na njema. Ni ndoto zinazolitakia
kheri taifa letu. Lakini wakati tukiwa katika kuota na kujitahidi kuchora picha
ta Tanzania mpya hatuna budi kujiuliza maswali ya msingi kama vile nini nafasi
ya vijana kama nguvu kazi katika Tanzania ya viwanda.
Tunaambiwa kwamba moja ya faida za viwanda ni kuongezeka kwa
ajira kwa nguvu kazi ya taifa letu. Hilo ni jambo jema. Lakini pamoja na uzuri
wake wote tunatakiwa kujiuliza swali moja la msingi kwamba hawa tunaodai kwamba
watapata ajira katika hivyo viwanda vitavyojengwa hapa nchini ni kweli watapata
ajira? Na kama bi kweli watapata ajira je, watapata ajira ya aina gani ni ajira
ya kiwango au ili mradi ajira?
Hatuna budi kama taifa kujiuliza maswali ya msingi na
kuyapatia majibu kwa sababu kama tutaimba ngonjera za kisiasa kwamba tunahitaji
kuwa na viwanda kwa ajili ya kutengeneza ajira kwa vijana lakini tusifanye
lolote katika maandalizi ya viwajana wenyewe basi tutakuwa tunatengeneza ajira
kwa ajili ya vijana wa mataifa mengine.
Viwanda vya kisasa vinahitaji elimu bora. Vinahitaji watu
wenye uelewa wa kutosha katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. Viwanda
vingi hivi sasa duniani vinaendeshwa kwa mitambo ya kisasa. Hata ujenzi wa
barabara unafanyika kwa kutumia mitambo ambayo inahitaji maopereta waliopatiwa
mafunzo maalum kwa ajili ya kuiendesha. Buldoza la siku hizi ni tofauti na la
zamani. Buldoza la siku hizi ni la kidijitali na linaendeshwa kwa kompyuta.
Ili kujiandaa na Tanzania na viwanda ni lazima kuhakikisha
kwamba vijana wetu wanapatiwa elimu bora ya kisasa inayoendana na mapinduzi ya
sayansi na teknolojia yanayoiongoza dunia hivi sasa.
Kwa mantiki hiyo basi mitaala ya elimu katika shule zetu
zote ni lazima iandaliwe kwa kuzingatia ukweli huo kwamba dunia tuliyopo hivi
sasa ni ya kidijitali. Si sahihi hata kidogo kuendelea na mitaala ya elimu
ambayo haitilii maanani mapinduzi ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kote
duniani. Hii maana yake nini?
Shule zetu za msingi hazina budi kuhakikisha kwamba mtoto
anaelekezwa katika kuijua dunia kwa kutumia nyenzo za kisasa ambazo ni za
kidijali zaidi kulinganisha na zile tulizotumia sisi wakati tunasoma. Mtoto wa
kisasa hawezi kutengwa na kompyuta kwani kompyuta ndiyo kila kitu kuanzia katika
kutumia maktaba za ndani na nje ya nchi hadi kufikia katika upishi wa keki na
chapati kutumia majiko ya kuoka kwa kutumia mionzi.
Kuingia kwa simu smati yaani smartphones ni ushahidi kwamba
tunakoelekea bila ya kujua kutumia mitambo ya kidijitali baisha yatakuwa ni
magumu sana.
Kwa maana hiyo ni kwamba kasi ya maendeleo katika sayansi na
teknolojia inafanya kiu ya Tanzania ya viwanda kuwa si kubwa tu bali kuwa ya
changamoto kubwa sana.
Ni wazi kwamba hata kama tungelitaka kurejesha viwanda vile
vilivyouawa wakati wa zama za Mwalimu Nyerere ukweli ni kwamba dunia
imekwishaachana na viwanda hivyo. Viwanda vingi duniani ni vya teknolojia ya
kisasa inayohitaji uelewa mkubwa wa jinsi ya kuendesha mitambo ya kisasa.
Kadri tunavyozidi kutafuta wawekezaji ndivyo tunavyokutana
na teknolojia ya kisasa. Hata kama tukisema tuwe na viwanda visivyokumbatia
teknolojia ya kisasa kwa kiasi kikubwa bado hicho kiasi kilichopo
kitatulazimisha sisi kuwa na watu wenye uelewa wa sayansi na teknolojia tofauti
na ilivyokuwa enzi za Kiltex, Mwatex na kadhalika.
Kama hatutaketi chini na kuangaliza mitaala yetu ya elimu na
kutoa kipaumbele katika masomo ya sayansi na teknolojia ya kisasa tutakuwa
katika hatari ya kuwa wafanyakazi wa daraja la chini katika viwanda
tutanavyopigia debe kuanzishwa kwa wingi hapa nchini. Maana yake ni kwamba
shule zetu hazina budi kutilia mkazo masomo yanayohusisha teknolojia ya
mawasiliano kama msingi na nguzo ya elimu yote kuanzia vidudu.
Tunatakiwa kuhakikisha kwamba mtoto wa Kitanzania anakuwa na
urafiki wa karibu na teknolojia ya mawasiliano kama msingi wa upatikanaji wa
elimu kwani vinginevyo tutakuwa tunajidanganya.
Mtoto asiyejua kompyuta hana lake katika uchumi wa viwanda
wa kisasa. Hata kama sisi tungelipenda kuwa na viwanda visivyokuwa vya kisasa
sana bado hivyo viwanda kwa kiwango kikubwa vitahitaji uelewa wa kiasi kikubwa
wa teknolojia mpya ya sayansi ya mawasiliano kwa sababu hata umeme unaoendesha
mitambo hiyo unatumia mita za LUKU na wala si zile za kuzunguka za karne
iliyopita. Huo ndio ukweli.
Ili kuhakikisha kwamba vijana wa nchi yetu wanaandaliwa kwa
ajili ya kuingia katika uchumi wa viwanda ni lazima shule wanazosoma ziwe na
viwango vya kisasa kuanzia msingi. Ina maana kwamba kila shule ni lazima iwe
walau na maabara ndogo ya kompyuta kama sehemu muhimu ya mafunzo yao. Ili shule
iwe kompyuta ni lazima iwe na umeme wa uhakika. Ni shule zetu ngapi za msingi
zina umeme?
Aidha, swali la kujiuliza ni waalimu wangapi wa shule za
msingi kote nchini wanao uelewa wa jinsi ya kutumia kompyuta? Wakati kompyuta
ni kifaa cha nyumbani katika takriban kila familia huko ughaibuni ambako ndiko
tunahangaika kuwaomba waje wawekeze kwenye viwanda, je, hapa nchini ni shule
ngapi za msingi zina kompyuta?
Shule zetu nyingi za msingi hazina umeme. Watoto wetu
wanamaliza elimu ya msingi bila ya uelewa wa kompyuta. Hiyo inawakwaza
wanapoingia katika masomo ya sekondari na hiyo inaendelea hadi wanafika mbele
ya safari.
Ninapomsikia waziri mwenye dhamana ya elimu anapiga kelele
kuhusu sayansi na teknolojia na hata kufikia hatua ya kutoa maelekezo kwamba
kila mtoto asome sayansi ninamuelewa kwa dhati kabisa japokuwa sikubaliani na
staili hiyo ya utoaji wa elimu. Hakuna sababu ya kuwalazimisha wasiotaka masomo
ya sayansi kuyasoma isipokuwa ni muhimu kuwalazimisha wote kutumia sayansi na
teknolojia kupata elimu.
Inamaanisha kwamba kila motto ni busara akajua jinsi ya
kutumia kompyuta kwani hivi sasa dunia inatafuta elimu katika mitandao ya
inteneti ambayo kimsingi ni utumiaji wa kompyuta kwa ajili ya kuhifadhi taarifa
ambazo ndani yake kuna elimu kubwa tu.
Mtoto asiyejua kutumia kompyuta ni wazi kwamba atakuwa
hawezi kushindana katika soko la ajira la zama hizi. Kompyuta ndiyo maktaba,
ndiyo vitabu vya ada na kiada, ndiyo mabuku ya rejea na kadhalika. Ili mradi
mtoto anayejua kutumia kompyuta kwa ajili ya kujipatia elimu atakuwa mbele ya
yule ambaye hana fursa hiyo.
Hatuna budi basi kuwaandaa vijana wetu kwa ujio wa viwanda
vya kisasa kwani tusipofanya hivyo tutajikuta katika wakati mgumu. Tutajengewa
viwanda lakini watakaohudumu humo watatoka kwa wale waliofanya maandalizi ya
kutosha kielimu kwa ajili ya ujio wa viwanda.
Ni wakati muafaka hivi sasa kwa wataalamu wetu wa mitaala ya
elimu kupitia upya taratibu za ufundishaji ili kuhakikisha kwamba vijana wetu
hawaishii kuwa ni watu wa kubofya tufe za simu tu bali wawe ni watu wanaojua
kwamba hiyo simu ya mkononi ni mwendelezo wa kompyuta na kwamba kompyuta ni
chombo muhimu sana katika maisha ya leo duniani.
0 Comment to "Tusipobadili mitaala vijana wetu watabaki vibarua"
Post a Comment
Post a Comment
1410