Kama kuna mfupa ambao Baraza la mtihani chini wizara ya
elimu imeushindwa kuutafuna kwa miongo kadhaa sasa basi ni uvujaji wa mitihani
ya kitaifa. Mitihani ya kitaifa kuanzia darasa la nne, darasa la saba, kidato
cha pili, cha nne hivyo mpaka cha sita haikosi dalili za kuvuja kila
inapofanyika.
Bado wizara ya
elimu haijafanikiwa kudhibiti kasumba hii mbaya na yenye athari nyingi mbaya
kwenye elimu. Kadiri siku zinavyozidi kwenda inataka kuonekana kama ni jambo la
kawaida kuvujisha mitihani.
Kwa kweli uvujaji wa mitihani unaelekea kuwa sehemu ya
utamaduni wa taifa letu. Kila mwaka matokeo yanapotangazwa au mitihani
inapofanyika lazima visa vya wizi wa mitihani visikike.Yaani kuvuja kwa
mitihani kungekuwa kigezo cha kumuondoa waziri wa elimu au katibu wa baraza la
mitihani basi hakuna ambaye angedumu kwenye hizo nafasi kwa zaidi ya mwaka
mmoja. Ingekuwa kila mitihani wa kitaifa unaenda na waziri na katibu wake wa
baraza la mitihani.
Kwa kiasi kikubwa wahusika wa kuu wa kuvujisha mitihani ni
wasimamizi wa mitihani. Visa vingi vya uvujaji mitihani vinavyoripotiwa
vinaonyesha wazi wasimamizi wa mitihani kuhusika. Kwa kweli kwa asilimia nyingi
mtihani hauwezi kuvuja kama msimamizi hataamua uvuje.
Watawala wa elimu katika wilaya, Walimu wakuu, wamiliki wa
shule na wakati mwingine wana bodi ya shule ndiyo wamekuwa wakijihusisha na
uvujaji wa mitihani ili kuzipatia shule zao majina. Walimu wakuu wanaojihusisha
na vitendo hivi huwahonga wasimamizi wa mitihani kiasi fulani cha fedha ili
wakiuke kanuni za usimamizi wa mitihani.
Mathalani kwa mujibu wa baadhi ya walimu waliowahi kuwa
wasimamizi katika shule kadhaa, wanasema kuna shule ambazo huandaa kabisa fungu
la fedha kwa ajili ya kumpooza msimamizi ili wizi wa mitihani ufanyike.
Kwa hiyo ukosefu wa maadili na uaminifu ni moja ya sababu
kubwa sana ya uvujaji wa mitihani, baadhi ya wasimamizi wanageuza kazi ya
kusimamia kama sehemu ya kujipatia faida mara mbili, kwa sababu wanalipwa na
baraza lakini pia wanalipwa rushwa na wakuu wa shule au wamiliki wa shule.
Uko ujingi hata wa wazazi kuchangisha fedha za kuibia
mitihani katika baadhi ya maeneo. Ukweli ni dawa ,tukikaa kimya Taifa
litaangamia. Leo hii watoto wanafaulu kwenda kidato cha kwanza huku hawajui
hata kusoma na kuandika, unajiuliza mtihani wao walifaulu vipi kama si wizi!
Wasimamizi wa mitihani waliohongwa huwa hufanya ya fuatayo,
kwanza hutumia muda mwingi nje ya chumba cha mtihani. Hufanya hivyo ili kutoa
nafasi kwa wanafunnzi kuigiliziana majibu na kupeana majibu.
Wakati mwingine msimamizi wa mitihani wakishahakikishiwa
donge nono, hushirikiana na askari wasiowaaminifu kufungua mitihani kabla ya
muda, kisha huitafutia majibu na kisha majibu hayo hupewa wanafunzi kabla ya
mtihani. Hapa ndiyo kama mlivyosikia hivi karibuni wanafunzi walikutwa
wameingia na majibu yaliyoaandikwa kwenye sare zao za shule.
Wapo wasimamizi ambao hutumia mbinu ya kuchukua karatasi ya
maswali na kuitoa nje , huko nje walimu wa shule husika hujichimbia kutafuta
majibu ya maswali husika, Ambapo majibu hayo hupewa msimamizi awasambazie
watoto.
Kadhalika shule
inaweza kuyaweka majibu hayo chooni ili wanafunzi wanaofanya mtihani wakiomba
ruhusa kwenda chooni hujue wanarudi na majibu. Wanafunzi wawili watatu wanaweza
hata kujifanya wanaharisha, wakaenda chooni mara kwa mara kumbe wanaenda
kuchukua majibu.
Mr.Mwalimu Blog inashauri upekuzi wakina ufanyike na inapotokea
wanafunzi au shule imaiba mtihani kupitia njia hii askari aliyekuwa anasimamia
awajibishwe vikali.
Hii inawezekana tu kama askari ambaye anawajibu wakukagua
vyoo kabla ya kuanza mtihani, ana wajibu wakumpeleka mwanafunzi chooni na
kukikagua choo mara kwa mara atazembea au kama nae atakuwa ametembezewa mlungula.
Uvujishaji wa mitihani ni janga kwa sababu, unaharibu
watoto, watoto wanakuwa wazembe kujisomea, wakitegemea mitihani itavuja. Pia
inaharibu maadili ya watoto. Fikiri kuhusu mwalimu anaekaa chini na mwanafunzi
wakapanga mipango ya kuiba mtihani, akifaulu baada ya myaka akawa mwalimu
atakuwa mwalimu wa namna gani.
Janga la wizi wa mitihani linafundisha watoto
kutokuwajibika, linafundisha watoto wizi na ndiyo hawa wanakuwa watumishi wa
umma alafu haachi kuiba kwa sababu ndiyo njia iliyowatoa.
Mtihani wa kidato cha nne inayoaanza leo, ina nafasi kubwa
ya kuibiwa kutokana na hali na mwenendo wa ukali wa serikali ya sasa. Wakuu
wengi wa shule za umma wanahofia kupoteza nafasi zao kama watoto watafanya
vibaya hivyo baadhi watalinda nafasi zao hata kwa kuiba mtihani. Wakuu wa shule
binafsi watafanya ili kulinda soko la shule zao.
Wito wangu kwa serikali , ili kukomesha tabia hii mbaya
hatua kali na za wazi zichukuliwe dhidi ya wakuu wa shule, wasimamizi, wazazi, wanafunzi
na bodi za shule zitakazojihusisha na wizi wa mtihani. Bado sijasikia hatua
kali zinazolenga kukomesha jambo hili kabisa, ni kama serikali inawalea
waharibifu wa elimu yetu na taifa letu.
Walimu tulinde maslahi mapana ya nchi, tusiwe wepesi
wakununuliwa na vijihela vya mchuzi wakati tunaangamiza taifa, wakati
tunajishushia hadhi. Walimu ni chumvi ikiharibika haifai. Watu wa usalama,
walinzi na mgambo nao wasimamie kazi hii kwa uaminifu. Niliwahi kupita shule
moja siku ya mtihani wa darasa la saba nikakuta mgambo anayelinda usalma wa
ufanyaji wa mitihani yuko mtaa wa pili toka shule yake anayosimamia.
Wasimamizi mjitahidi kuvishinda vishawishi. Mathalani kuna
mwalimu mmoja alinipa ushuhuda, alienda kusimamia mtihani wa kidato cha nne, baada
ya kushawishiwa apokee rushwa ya kuvujisha mtihani na kukataa, alifuatwa na
wazee maarufu wa hicho kijii na wazee wabodi kumshawishi ili akubali. Hali ilikuwa
ngumu kwake kiasi hata wanafunzi aliokuwa anawasimamia hawakuwa wanamsalimia ni
hivyo pia wanakijiji. Hii ni jinsi gani wizi wa mitihani ulivyoota mizizi!
Serikali kwa namna ya pekee ifikiri zaidi namna ya kukomesha
jambo hili, na namna moja wapo ni kuboresha maslahi ya walimu na wasimamizi wa
mitihani.Yote kwa yote ninachojiuliza ni kwamba je mtihani wakidato cha nne
utavuja tena mwka huu? Wakati utatoa jibu. Mr.Mwalimu Blog; Elimu Kwanza.
KILA LA KHERI KIDATO CHA NNE
Nini unafikiri kifanye kuzuia uvujaji wa mitihani?Toa maoni yako tafadhali na karibu
ReplyDelete