Mountain View

Wednesday, December 28, 2016

Hakuna elimu bora kwa wazazi wanaobweteka

Wanafunzi wengi wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo hawafanyi vizuri kitaaluma kwa sababu ya wazazi wao kutofuatilia maendeleo ya watoto wao. Wazazi wanafikiri majukumu yao ni kulipa ada na michango mengine pekee na kuwaachia walimu.


Wazazi wengi wana shauku kubwa ya kuona watoto wao wanafanya vizuri katika masomo, lakini hawako tayari kufuatilia maendeleo yao ya taaluma na hata nidhamu.

Jukumu hilo wameachiwa walimu peke yao. Na walimu wanapojaribu kuwanyoosha kinidhamu, jamii kwa upande mwingine inawanyooshea kidole na kuwalaumu.

Uzoefu unaonyesha, kwa sababu ya ugumu wa maisha wazazi wengi hawana muda wa kukagua daftari za watoto wao, kutembelea shuleni na kufanya mashauriano na walimu.

Kwa kutembelea shule, kuna mengi yanaweza kutafutiwa ufumbuzi kati ya mwalimu na mzazi, lakini hilo halifanyiki. Mzigo wote anaachiwa mwalimu ambaye hata hivyo hulaumiwa pindi matokeo yakiwa mabaya.

Tujiulize kosa la mwalimu huyu aliyeachiwa mzigo wa kusomesha na ule wa malezi ambao haumhusu. Wakati mwingine, ufaulu mdogo unatokana na wanafunzi kutokuwa na nidhamu, upi wajibu wa wazazi katika hili?

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwa Kiingereza: “It takes a village to raise a child” yaani ni jukumu la jamii au kijiji kumkuza mtoto.

Hii inamaanisha kuwa ikiwa jamii itaungana kwa pamoja kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu bora, ni dhahiri hakutakuwa na malalamiko kuhusu nidhamu mbovu na hata ufaulu usioridhisha.

Linapokuja suala la ushiriki wa jamii katika kutoa elimu iliyo bora, wazazi na walezi wanapaswa kuwa sehemu ya vikao vya maamuzi kuhusu maendeleo ya watoto wao katika shule za umma kama inavyokua katika shule binafsi.

Wazazi lazima watambue kwamba Serikali haiwezi kubeba majukumu yote kwa mwamvuli wa elimu bure, huku wakibweteka na kusubiri watoto wao wapate elimu itakayoleta mabadiliko katika maisha.

Wazazi wasiwe wapiga filimbi kuwalaumu walimu tu na kuzuia adhabu zinazotolewa na walimu kwa wanafunzi. Lazima wayaelewe mazingira wanayofanyia kazi walimu na aina ya wanafunzi walio nao.
Wanaposhindwa kutoa ushirikiano kuhusu suala zima la maendeleo ya wanafunzi, walimu nao wanakata tamaa na kuacha mambo yajiendee.

Wanasiasa na watu wenye ushawishi katika jamii lazima walielewe hili na wawe mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa wazazi wanashiriki kikamilifu katika nidhamu na maendeleo ya taaluma.

Fedha zinazotumika katika elimu bure zinatokana na makusanyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo wananchi wenyewe.

Huu ni uwekezaji usiokuwa na malengo ya kupata faida hauna maana hata kidogo. Lazima wananchi tuone kwamba fedha zetu zinazokwenda kugharimia elimu ya vijana wetu zinaleta faida.

Mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu lazima ihakikishe pamoja na mambo mengine inawajengea uwezo wakuu wa shule na walimu kuhusu njia bora za kuwashirikisha wazazi.

Tukiwaachia jukumu hili walimu na Serikali tunakua tumepoteza mwelekeo. Wazazi tuwajibike kwa kuhakikisha vijana wetu wanakua nguvukazi madhubuti kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili. Vinginevyo shule zetu zitakua vituo vya kulelea watoto kwa miaka kadhaa na baadaye watoto hao wasiwe na mchango wowote kwa maendeleo ya nchi yetu.

Wakati ni sasa kila mmoja atimize wajibu wake katika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata elimu bora.


Sunday, December 25, 2016

SERIKALI Yapiga Marufuku Shule Binafsi Kufanya Mitihani ya Kuchuja Wanafunzi


Hiyo ni baada ya kutangaza kupiga marufuku utaratibu wa kuwachuja wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa uliokuwa unaofanywa na baadhi yao kwa lengo la kuonekana shule zao zinafaulisha vizuri.

Hivi karibuni, Nipashe iliripoti kuhusu hofu ya baadhi ya shule hizo; za msingi na sekondari ziko hatarini kubadilishwa matumizi kutokana na kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na kutoa elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikiwaumiza wananchi.

Huku udahili kwenye shule za serikali ukiongezeka na kuonekana kuwa tishio kwa ustawi wa shule za watu na taasisi binafsi, imewabana tena wamiliki wa shule binafsi kwa kuwazuia kufanya mchujo wa wanafunzi wanaoingia kwenye madarasa au vidato vyenye mitihani ya taifa.

Mmoja wa wazazi aliliambia Nipashe kuwa mwanawe anayesoma kidato cha tatu katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, amepangiwa kuhamishiwa shule nyingine ya mmiliki huyo huyo kutokana na kufaulu kwa daraja la tatu.

Kwa mujibu wa mzazi huyo, kuna wanafunzi takribani 70 wa kidato cha tatu, wanatarajiwa kuhamishwa katika shule hiyo waliyosajiliwa tangu kidato cha kwanza, watahamishwa shule hiyo na kubaki wale waliofaulu kwa viwango vya madaraja ya kwanza na pili tu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, alisema ni marufuku shule kumkaririsha darasa, kumfukuza, kumhamishia shule nyingine au kumsajili kama mtahiniwa binafsi (PC) mwanafunzi kwa kigezo cha kutofanya vizuri katika mitihani ya shule husika.

"Ni marufuku kabisa kufanya hivyo. Mitihani tulionayo sisi (Wizara ya Elimu) ndiyo mchujo sahihi. Na mtihani ambao unamkaririsha mwanafunzi ni mtihani wa taifa wa kidato cha pili na mtihani wa darasa la nne tu," alisema.

"Wala siyo mtihani wa shule na madarasa mengine hayana mtihani wa kumkaririsha mtoto au kumfanya aondolewe shuleni au ahamishiwe shule nyingine, hatuna utaratibu huo na serikali haiwezi kukubaliana nao," aliongeza Dk. Akwilapo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongosco), Benjamin Nkonye, aliiambia Nipashe jana kuwa utaratibu wanaoutumia ni kushauriana na wazazi wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri shuleni ikiwamo kuwapeleka katika vyuo vya ufundi (Veta).

Alisema shule binafsi zinapaswa kupongezwa kwa kudahili hata wanafunzi hasa wa sekondari ambao shule za serikali huwa haziwachukui kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya shule za msingi.

“Hakuna shule ambazo zinapaswa kupongezwa kama za binafsi, serikali yenyewe imekuwa ikichagua wanafunzi wote. Inatuachia ‘vilaza’, lakini sisi kwa kujitoa kuwasaidia watoto wa Kitanzania, tunakubali kuwachukua hao hao wanaoonekana wabaya, tunawafundisha na mwisho wa siku wanakuwa wazuri kuliko hata hao wanaokuwa wamethaminiwa na serikali,” alisema Nkonya.

“Na sisi hatuchuji wala kumfukuza mwanafunzi, isipokuwa kinachofanyika kwa kuwa tunapokea wakati mwingine wanafunzi ambao ni ‘vilaza’ kabisa, huwa tunawagawanya katika makundi kulingana na uelewa wao, wenye uelewa wa kwanza, wa kati na wa mwisho. Na mwisho na tunawafundisha kulingana na ‘speed’ (kasi) ya uelewa wao na wanajikuta wanafanya vizuri.

“Lakini kwa sababu sisi tunakuwa na wanafunzi ambao ni wagumu sana, inapoonekana wakatokea wachache hawawezi kabisa huwa tunashauriana na wazazi wao, kuwapeleka Veta ili kule wanapokuwa wanaendelea kujifunza, wengine wanafanya vizuri hadi wanafika vyuo vikuu, hatuwaachi kama ilivyo katika shule za serikali na vyuo vya serikali, haya maneno mengine yanayozungumzwa ni ya kisiasa tu."

HALI ILIVYO

Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika hivi karibuni katika baadhi ya mikoa, ulibaini baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa na utaratibu wa kuchuja wanafunzi kila mwaka kwa lengo la kupata wenye uwezo mkubwa darasani.

Ilibainika kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanywa kwa nia ya kuwa na wanafunzi wenye uwezo mkubwa ili shule hizo zifanye vizuri katika mitihani ya taifa, hivyo kuvutia wazazi wengi zaidi kupeleka watoto wao.

Gazeti hili lilibaini kuwa, baadhi ya shule binafsi zimekuwa zikiendesha utaratibu huo kipindi cha mitihani ya mwishoni mwa mwaka kwa kuwafukuza, kuwakaririsha darasa au kuwahamishia shule nyingine wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango kinachowekwa na shule husika kwenye mitihani ya kufunga mwaka.

Nipashe pia ilibaini baadhi ya shule hizo zimekuwa na utaratibu wa kuwachuja kwa kuwasajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) kwenye mitihani ya taifa wanafunzi wake wanaoshindwa kiwango kilichowekwa wanapofanya mitihani ya shule husika.

MTOTO WA PROFESA AKACHA KULA

Akizungumzia suala hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Allen Mushi, alisema haungi mkono utaratibu wa baadhi ya shule binafsi kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango cha alama zilizojiwekea.

Alisema: "Ni makosa kumfukuza shule mwanafunzi aliyekuwa amedahiliwa, anasoma halafu unamsitishia, unamwambia nenda katafute shule nyingine.

"Na ni kweli wana tabia hiyo. “Nina kijana wangu yuko ‘Form One’ (Kidato cha Kwanza) anasoma shule ... (anataja eneo ilipo shule hiyo), yaani anasoma kupindukia. Nilikuwa na wasiwasi hata akija likizo hawezi kula vizuri, anasoma tu."

Alisema kuwa katika shule hiyo ya jijini Dar es Salaam anayosoma mtoto wake, wameambiwa ni lazima awe na wastani wa kuanzia alama 50 katika mitihani ya shule ili aruhusiwe kuingia kidato kinachofuata, vinginevyo wakatafute shule nyingine.

"Katika utaratibu wa elimu, siyo sahihi kufanya hivyo, wewe kama wanafunzi wameshindwa, wewe siyo ndiyo mwalimu, ndiyo kazi yako ya kufanya wanafunzi waelewe," alisema na kufafanua zaidi:

“Sasa ukiwa unafanya hivyo, mwisho wa siku utakuwa unafelisha darasa zima na kujitamba kwamba unafaulisha kwa sababu umefukuza wengi na kubaki na wazuri wachache. Sasa hiyo ni biashara, siyo elimu tena. Wewe kama ni mwalimu, unatakiwa kufundisha wanafunzi wote.

“Kwa hiyo, wanasema shule za ‘private’ (binafsi) zinafaulisha wanafunzi wote, kumbe wengine mliowachuja. Mimi binafsi sikubaliani na hali hiyo kabisa."

Alisema ni muhimu wizara yenye dhamana ya elimu nchini iweke masharti kwamba ukishadahili wanafunzi, wasiondolewe shuleni kwa utaratibu wa viwango vya ufaulu katika mitihani ya shule husika isipokuwa kwa sababu za tabia mbaya na zisizofaa kwa mwanafunzi kwa mujibu wa sheria za nchi.

MAKUNDI YA UELEWA

Msomi huyo alisema wanafunzi wamegawanyika katika madaraja mawili kiuelewa darasani, la kwanza likiwa la wenye uelewa wa haraka (fast learners) na jingine likiwa la wenye uelewa hafifu (‘slow learners).

"Wote hao wanapaswa wazingatiwe katika elimu. Sasa hawa (shule binafsi) wenyewe wanaangalia 'fast learners' tu. Ni vema wote wakachukuliwa katika vigezo sawa, siyo unawachuja wengine halafu unasema unafaulisha wote," alisema Prof. Mushi.

BIASHARA

Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba, akizungumza na Nipashe jana kuhusu changamoto hiyo, alisema si vyema kumfukuza, kumkaririsha darasa au kumhamisha mwanafunzi aliyefanya vibaya katika mitihani ya shule.

"Mtihani wa Kidato cha Pili ni mchujo sahihi tu. Shule binafsi wanakosea. Ufundishaji wa kawaida huwezi kuwa na wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu," alisema.

"Hao shule binafsi kuna muda wanateleza kidogo, kwa sababu hakuna mwanafunzi asiyefundishika labda kwa sababu wao wanataka suala la biashara. Ni kuonea wanafunzi, bahati mbaya akishaanza shule ya 'private' (binafsi) kidato cha kwanza, hawezi kurudi kwenye mfumo wa serikali, kwa hiyo wanafunzi wanahangaika," alisema zaidi Mukoba.
Mr.Mwalimu blog




Friday, December 23, 2016

NCHI NANE KINARA WA KUWAKARIMU WANAFUNZI WA KIGENI



Fahamu kuwa si kwa sababu unataka kusoma nje ya nchi basi kila nchi ni salama kwako, hapana baadhi si salama kwako na baadhi ni salama kwako kutokana na vigezo na mazingira mbali mbali.

Kwa mtu ambaye una ndoto za kutafuta elimu nje ya nchi ya Tanzania, una kila sababu ya kusoma makala hii.Kadhalika mtu ambaye una shauku la mwanao au jamaa yako asome nje ya nchi taarifa hizi zawezakuwa za muhimu sana kwako.Chanzo cha makala hii ni gazeti la Mtanzania.

KILA mtu anatamani kusoma nje ya nchi hususan Ulaya ambako baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kuwa kusoma au kupata ujuzi kwenye vyuo hivyo  vya ng’ambo kutawawezesha kupata fursa zaidi za ajira ikilinganishwa na kusoma kwenye vyuo vya ndani.
Kumekuwapo baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwapata wanafunzi wa kigeni pindi wanapokuwa ng’ambo.

Hii inatokana kwamba nchi nyingi zimekuwa haziweki mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kigeni, hata inapotokea wamekumbwa na misukosuko serikali za nchi hiyo zimekuwa zikichelewa kuchukua uamuzi au  kuwatetea wanafunzi hao.
Hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya wanafunzi na wazazi  kuwa na hofu ya kwenda kusoma nje ya nchi zao.

Matukio kadhaa yasiyo ya kufurahisha yamewakumba wanafunzi wa kigeni, hali hiyo imekuwa ikitafasriwa kama ni kawaida kwa mataifa yaliyo na vyuo bora nje ya nchi jambo ambalo si kweli.

Kama ndoto zako au hata za mtoto wako ni kusoma na kupata ujuzi nje ya nchi kwenye vyuo vilivyoendelea na kujenga wasifu wake vizuri utakaomsaidia kupata kazi kirahisi ndani na nje ya nchi na bado hujajua ni nchi gani ambayo mwanao atasoma akiwa salama na kukarimiwa vizuri, makala hii itakupa mwanga.

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Ulaya EU miezi michache iliyopita, imeorodhesha nchi nane zinazoongoza kwenye kuwakarimu wanafunzi wa kigeni.

 Uingereza
Nchi hii imepata asilimia 0.7 ya kukarimu wageni huku ikinyakua asilimia 0.5 ya wanafunzi wanaohitimu kwenye vyuo vyake.

Licha ya kwamba nchi hii iliibuka kinara kwa kuwa na wanafunzi wengi wa kigeni kati ya nchi 35 za bara hilo lakini ilikuwa na asilimia 40 ya wanafunzi wake ambao walihitimu nje ya vyuo vya nchi hiyo kwa mwaka 2012-2013 jambo ambalo lilifanya ipunguziwe alama kwenye ripoti hiyo.

Mbali na ‘doa’ hilo, ni wazi kuwa Uingereza imekuwa ikisifika kwa kuwa na mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kigeni ikiwamo kuwapa msaada wa karibu na kuwashirikisha kwenye fursa mbalimbali za kiuchumi.

 Ubiligiji
Ina asilimia 2.4 ya ukarimu kwa wanafunzi huku kiwango cha wanafunzi wanaohitimu masomo yao nchini humo kikiwa ni asilimia 3.3 ambapo pia imekuwa ikisifika kwa kuwahamasisha wananchi wake juu ya watoto wao kujifunza lugha za kigeni walau 15 kwa mwaka.

Nchi hii haijapishana na Uingereza katika kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi sanjari na kuwawezesha kiuchumi ambapo katika kulitekeleza hilo imekuwa na mikakati mbalimbali ukiwamo ule wa ‘Flemish community’  wenye lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 inakuwa na asilimia 33 ya wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanaokwenda kusoma nchini humo.
Kwasasa asilimia 48 ya wanafunzi wa kigeni wanaosoma nchini humo ni kutoka Ufaransa.

 Denmark
Hii ina asilimia 1.3 ya ukarimu kwa wanafunzi huku ikiwa na asilimia 1.7 ya wanafunzi wa kigeni wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini humo.

Denmark ni miongoni mwa nchi chache za Ulaya zinazotoa msaada mkubwa zaidi kwa wanafunzi wa kigeni karibu wote wanaofika kuchukua masomo yao nchini humo, pia inatoa ushirikiano zikiwamo taarifa mbalimbali kwa wanafunzi.

Pamoja na mambo mengine imeweka mkazo wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anajifunza lugha mbili kwa wakati mmoja kwa kipindi cha walau miaka mitano huku akipata mkopo na msaada mkubwa kutoka serikalini.

Nchi nyingine ambazo zimekuwa na alama za juu zaidi ni pamoja na Ujerumani ambayo ina asilimia 3.9 ya kukarimu wanafunzi wa kigeni huku ikiwa na asilimia 54.1 ya wanafunzi wa kigeni wanaohitimu masomo yao nchini humo.

Lakini pia imekuwa ikitoa misaada ya hali na mali kwa wanafunzi wote wa kigeni wanaofika nchini humo. Nyingine ni Bulgaria yenye ukarimu wa asilimia 7.8 kwa wanafunzi wa kigeni na asilimi 6.6 ya wanaohitimu. Asilimi 52 ya wanafunzi wake wanatoka nchini Uturuki.

Nyingine ni Uholanzi, Luxembourg na Slovakiam. Chaguo ni lako mwanafunzi na mazazi kumpeleka mwanao nje au la kwani nchi hizo zote zina mazingira rafiki ya taaluma na hali ya juu

MRMWALIMU.BLOGSPOT.COM#ELIMU KWANZA


 MR.MWALIMU.BLOGSPOT.COM#ELIMU KWANZAM

Friday, December 16, 2016

Sitisho la ajira kwa walimu wa sanaa litazamwe upya.

Waziri wa elimu ametangaza kusitisha ajira kwa walimu wa sanaa, kwa mtazamo wangu nafikiri ni bado mapema kuchukua maamuzi hayo.Nchi hii inaupungufu wa walimu mkubwa bado.Upungufu mkubwa upo kwenye Sayansi lakini hata sanaa inaupungufu. Kuna shule hazina walimu wa Kiswahili, Kiingereza wala Jiografia.

Chanzo cha habari hii ni gazeti la Mtanzania.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku akisema Serikali haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa kutosha.

Akizungumza mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako, alisema Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa inataka kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao ni ndogo.

“Pamoja na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo ya sayansi nazo zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi na hisabati, wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.

“Kuhusu wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada ambao tutajaribu kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa shule moja. Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.

Akizungumzia suala la ubora wa elimu nchini, Profesa Ndalichako aliwataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu kwa kuwa wao ndio wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.

“Vilevile pelekeni takwimu sahihi za wanafunzi waliopo katika shule zenu kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa kuna kimbembe, yaani wakati mwingine huwa najifanya nimepoteza takwimu ya shule fulani, nikiziomba na kutumiwa, zinakuwa ni tofauti na zile za mwanzo.

“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti yenye tija,’’ alisema.
Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, waziri huyo alisema kwamba kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa vya maabara kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka vilikoagizwa.

Awali, akisoma risala ya walimu hao, Rais wa TAHOSSA, Bonus Nyimbo, aliiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka kwa ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi.

“Ili kuboresha elimu, tunaiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi tunazozikamata tunakuta mule hakuna taaluma,’’ alisema Nyimbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Molel, ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika kuendeleza elimu nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuiendeleza elimu ya Tanzania.

“Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu, wazazi, walezi na walimu, waambieni wanafunzi wasiwe na ‘expectation’ (matarajio) makubwa kwani wanapokuwa na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu wanakuwa wasumbufu,” alisema.

Wakati hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi na hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na sita na taaluma ya ualimu kwa uhakiki.

Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza kusitisha ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.

Sambamba na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa watumishi wa Serikali nazo zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa ambao walikuwa wakiingizia hasara serikali.

Visa vya ushirikina vinavyoweza kuiathari elimu Bunda


Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa wilaya zenye visa vingi vya kishirikina kiasi cha kuwaweka katika wasiwasi walimu wanao hudumu katika wilaya hiyo. Kama juhudi za dhati hazitachukuliwa Watumishi wengi wataiogopa Bunda na pengine kuihama. Viongozi wa dini,chama na serikali chukueni hatua kwa pamoja hali hii ikome. Chanzo cha Habari hii ni gazeti la Mtanzania.


WANAWAKE wanne katika Kijiji cha Kihumbu, Kata ya Hunyari wilayani Bunda, wamejeruhiwa kwa kupigwa na vitu vizito, zikiwamo fimbo, rungu, bapa za panga na katani, baada ya kutuhumiwa kumuua kwa uchawi, mwanafunzi Waryo Mseti (12).

Tukio hilo lilitokea juzi mchana katika kijiji hicho wakati mwili wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kihumbu ukisubiri kuzikwa.
Ilidaiwa kuwa baada ya Mseti kufariki dunia, wazazi wake kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hasha Hamisi, walikwenda kupiga ramli kwa mganga wa kienyeji wakidai mtoto huyo alikufa kifo cha ushirikina.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Chacha Warioba, alidai mganga huyo baada ya kufanya dawa zake, alieleza kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amechukuliwa kichawi na wanawake hao na alikuwa bado yuko hai ila walikuwa wamemficha sehemu.

“Nathibitisha ni kweli tukio hilo lipo, polisi walifika hapa kijijini na kuwachukuwa wanawake hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Bunda. Wakati tukio hilo linatokea mimi sikuwapo hapa kijijini,” alisema Warioba.

Inadaiwa kuwa Hamisi aliyewapeleka wazazi wa mwanafunzi huyo kwa mganga, aliwaeleza wenzake kuwa hata yeye aliwaona wachawi hao kwenye kioo cha maji ya mganga wa jadi.
Kauli hiyo ilithibitishwa kwa waombolezaji waliokuwapo nyumbani hapo wakati maiti ya mtoto huyo ikiwa ndani ikisubiri kuzikwa.

Baada ya kuelezwa hayo, baadhi ya waombolezaji walianza kuwasaka wanawake hao wanaotuhumiwa kwa uchawi.
Waliwakamata mmoja baada ya mwingine na kuwapeleka mlimani, huku wakiwa wamewafunga 

kamba na wakiwatishia kuwachinja. Waliwapiga na kuwataka   wamrudishe mtoto huyo.
Wanawake hao (majina tunayo), wote wakazi wa Kijiji cha Kihumbu, walisema  walifanyiwa unyama na ukatili huo unaohusisha imani za ushirikina, na hata nyumba ya mmoja wao ilimwagiwa mafuta   iweze kuteketezwa kwa moto.

“Walitupiga sana kwa fimbo, mabapa ya mapanga, rungu na katani, walituteka hadi milimani wakitulazimisha tumrudishe huyo mtoto waliodai tumemuua.
“Mimi walinilaza chini na wakaniwekea panga shingoni, eti wanichinje kama sitaki kusema ukweli. Lakini nilikataa kwamba sijui chochote,” alisema mmoja wa wanawake hao.

Wanawake hao waliokolewa na polisi waliofika katika eneo la tukio na kuwachukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi Bunda kabla yakuwapeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH).
Bado wamelazwa hospitalini hapo baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo na muuguzi wa zamu katika Wodi ya Wanawake, Daria John, alisema hali zao zinaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi, alisema wote waliohusika  kujichukulia sheria mkononi lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.


Mwalimu mmoja wanafunzi 126


Kuna upungufu mkubwa wa walimu bila kujali fani.Kuna upungufu wa walimu wa sanaa,wa biashara naSayansi pia.
Mapema Mwezi Septemba mwaka huu mkurugenzi mtendaji wa Twaweza alitangaza matokeo ya unaoeleza kuwa uwiano wa walimu na wanafunzi ni mbaya sana.Kiasi cha kufikia wanafunzi 126 kwa mwalimu mmoja.
Kwa kuwa nchi yetu bado ni maskini na elimu inatolewa katika mazingira haya bado kuna safari ndefu.Kunahitajika hatua za makusudi za kisiasa, kiuongozi, kijamii na kivitendo zaidi ili kuikomboa elimu.
Pia moja wapo ya kasumba mbaya inayoathiri elimu yetu ni kufanya mambo kisiasa zaidi badaala ya kuzingatia taaluma na tafiti.Wakati huu ilikuwa ni wakati wakutafuta majibu ya tatizo lililoibuliwa na tafiti hii.

Dar es Salaam.Taasisi ya Twaweza imefanya utafiti na kubaini kwamba mwaka 2014, mwalimu mmoja alikuwa anafundisha darasa lenye wastani wa wanafunzi 83 licha ya sera ya elimu na mafunzo kupendekeza mwalimu mmoja afundishe wanafunzi 45.
Akizindua ripoti leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema ripoti hiyo inaonyesha hali ni mbaya zaidi katika mkoa wa Manyara ambako wanafunzi 126 wanafundishwa na mwalimu mmoja.
Katika utafiti huo, amesema walitembelea shule za msingi za serikali 1,309, kaya 16,013, na kuwahoji na kuwapima wanafunzi 32,694.
Amesema katika utafiti huo, mikoa yenye wanafunzi wengi kwenye madarasa wanaofundishwa na mwalimu mmoja na idadi yao kwenye mabano ni Kigoma (108), Rukwa (100), Singida (99) na Tabora (98).
Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi (67), Lindi wanafunzi 63, Arusha wanafunzi 62, Kilimanjari 60, Iringa 59 na Pwani 56.
Eyakuze amesema katika darasa la tatu asilimia 54 tu ya wanafunzi wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili.
Amesema asilimia 35 tu wanafunzi wa darasa la tatu wanaweza kufanya hesabu za darasa la pili


Fagio la Serikali lilivyosafisha sekta ya elimu

Makala hii ilichapishwa na gazeti la Mwananchi kama sehemu ya uchambuzi jinsi serikali ilivyofanikiwa na isivyofanikiwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha mwaka wakwanza. Mengi yamesemwa katika kuitathimini serikali ya awamu ya tano kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini naamini upande wa sekta ya elimu unahitaji mjadala mpana zaidi pia juhudi zinahitajika zaidi kuikomboa elimu.

Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, Rais John Magufuli amefanya jitihada kadhaa za kuboresha sekta ya elimu nchini.
Miongoni mwa jitihada hizo ni kutekeleza mpango wa utoaji wa elimu bure, unaotokana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotamka kuwa Serikali itahakikisha elimumsingi (elimu ya awali hadi kidato cha nne) inakuwa ya lazima na ya bure katika shule za umma.
Mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, mambo kadhaa yamejitokeza, huku yakihitaji uamuzi mgumu kuyashughulikia.
Kampeni dhidi ya ukosefu wa madawati
Kutokana na mahitaji makubwa ya  elimu bure, kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi, hali iliyosababisha kuwapo kwa ukosefu mkubwa wa madawati.  Mwaka mmoja wa utawala wake, Rais Magufuli akashupalia upatikanaji wa madawati shuleni.
Julai 13, Rais alizindua mpango wa ugawaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari kwa kupokea fedha zilizotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya kubana matumizi katika bajeti yake.
Siku ya uzinduzi alikabidhi madawati 537 kwa mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu kwa niaba ya wabunge wa majimbo yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Madawati hayo 537 yalikuwa sehemu ya madawati 61,385 ambayo yalitengenezwa katika awamu ya kwanza yakifuatiwa na madawati mengine 60,000 ya awamu ya pili yakigharimu Sh4 bilioni zilizotolewa na Bunge.
Mikoa iliyofadika katika  awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5.
Alisema hali hali hiyo imesababisha upungufu wa madawati 1,400,000 lakini tatizo hilo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa na mpaka sasa zaidi ya madawati 1,000,000 yametengenezwa.
Wanafunzi wasio na sifa
Serikali ya Awamu ya Tano na kaulimbiu yake ya Hapa Kazi Tu, ilifanikiwa kubaini wanafunzi wasiokuwa na sifa waliokuwa wakisomea kozi maalumu ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Wanafunzi wapatao 7,800 walisimamishwa masomo na kuzua mjadala mkubwa wa kitaifa. Mwezi mmoja baadaye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitoa orodha ya wanafunzi 382 aliodai kuwa ndiyo wenye sifa.
Alisema kuwa programu hiyo ilikuwa inahitaji walimu ambao watakwenda kufundisha shule za sekondari lakini kulikuwa na wanafunzi 1,210 ambao walikuwa wanachukua stashahada ya ualimu wa shule za msingi ambao ni kinyume na malengo na 6,595 wakichukua stashahada ya kufundisha shule za sekondari.
Utumbuaji majipu taasisi za elimu
Kasi ya utumbuaji majipu ya Serikali mpya ikaikumba Tume  Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), baada ya Waziri  Ndalichako  kuwasimamisha kazi mara moja viongozi wake wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa.
Waliosimamishwa ni pamoja na Katibu Mtendaji, Profesa Yunus Mgaya ambaye Profesa Ndalichako alisema ameshindwa kusimamia kazi za Tume hiyo ikiwa na maana kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi.
Mwingine aliyesimamishwa ni Mkurugenzi wa Ithibati na Uhakiki Ubora, Dk Savinus Maronga kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu.
Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kishweko naye alikumbwa katika kadhia hiyo akidaiwa kudahili wanafunzi wasio na sifa. Pia aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Kimboka Istambuli naye alisimamishwa.
Mbali ya viongozi hao, Mwenyekiti wa  bodi ya TCU, Awadhi Mawenya naye alisimamishwa kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kuwadahili wanafunzi hao.
Kabla ya mabadiliko ya TCU, Februari  Profesa Ndalichako alisitisha mkataba wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega na kuwasimamisha kazi wakurugenzi wengine watatu, kwa madai ya ukiukwaji wa utoaji wa mikopo pamoja na ucheleweshaji usio na sababu za msingi.
Wanafunzi hewa shuleni, vyuoni
Wakati Serikali ikijihimu kupeleka fedha za ruzuku ya wanafunzi, ilibainika kuwa baadhi ya walimu walikuwa na orodha ya wanafunzi bandia kwa minajili ya kufanya ubadhirifu.
Kwa mfano,  Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Manispaa ya Arusha, zilibaini udanganyifu huo na kuchukua hatua za awali kwa kusimamisha walimu wakuu wa shule husika na pia kuziagiza mamlaka husika kuwavua uongozi walimu husika.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema katika uhakiki huo walibaini wanafunzi hewa 3,462 kutoka shule 68 za msingi na wanafunzi 2,534 kutoka shule 22 za sekondari. Katika Manispaa ya Arusha, wanafunzi 907 walibainika kutokuwapo shuleni. Mbali na shule za msingi na sekondari, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza operesheni ya uhakiki wa wanafunzi hewa wa vyuo vikuu.

Profesa Ndalichako alisema kuwa kuna zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao majina yao yamewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa vitendo, yakiwamo majina  ya wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa chuo. 

Friday, November 25, 2016

Utafiti: Elimu bure imeongeza ubora wa elimu

Matokeo ya utafiti yaliotangazwa na taasisi ya Twaweza yanahitaji utafiti zaidi ili kuthibitisha.Kwa macho ya kawaida haionyeshi kuwa ubora wa elimu umeongezeka bali idadi ya wanafunzi imeongezeka. Tumeongeza idadi ya wanaohudhuria shule lakini hatujaongeza ubora. Habari hii imeandikwa na gazeti la Mwanachi.



By Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Dar es Salaam. Taasisi ya Twaweza imefanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 50 ya wananchi waliohojiwa wanasema ubora wa elimu umeongezeka tangu mfumo wa elimu bila ada ulipoanzishwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza,Aidan Eyakuze amesema idadi hiyo ya wananchi ni kati ya 1806 waliohojiwa Tanzania Bara.

Amesema asimilia 35 wamesema ubora umebaki palepale na wengine asilimia 15 wamesema ubora umeshuka.
Utafiti huo umefanyika kati ya Agosti 7 na 14 mwaka huu.
Hata hivyo baadhi ya wasomi wamesema  kiwango cha elimu hakiwezi kuboreshwa katika kipindi kisichofikia mwaka mmoja.

Mkapa: Maagizo ya viongozi yanaua elimu

Wazee wanapojitokeza kusema neno ni lazima kulitafakari na kulitendea kazi. Mzee Mkapa amesema
By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz
Dodoma. Wakati Serikali ikiendelea na mkakati wa kubadilisha mfumo wa elimu, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa amesema maagizo na amri za viongozi zinazotolewa bila ya kuwa na majadiliano, zitaitumbukiza shimoni elimu ya Tanzania.

Mbali na hilo, Mkapa, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, amesema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa vyuo vikuu nchini, ni lazima iendane na ubora wa miundombinu pamoja na bajeti ya Serikali badala ya kujaza wanafunzi wakati hakuna fedha za kutosha na hivyo kuwa mzigo.
Mkapa alitoa kauli hiyo jana wakati wa mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambako alikuwa mgeni rasmi.
Mkuu huyo wa Udom alisema maagizo peke yake, hayaondoi matatizo ambayo yamejitokeza katika siku za hivi karibuni.
Alisema njia bora ya kuboresha elimu nchini ni kwa wadau kukutana katika meza ya mazungumzo ili wajadili changamoto zinazowakabili na kueleza nini kinatakiwa.
“Amini nawaambia, maagizo peke yake hayaondoi matatizo tuliyonayo ndani ya elimu, bali niwaombe wadau pamoja na wizara husika kuwa wakae meza ya mazungumzo ili wazijadili changamoto hizo,” alisema Mkapa.
Alisema kama maagizo yataendelea bila ya kuwepo na majadiliano elimu ya Tanzania itakuwa imewekwa rehani na kwamba katika kipindi cha miaka michache nchi haitakuwa kwenye ubora wa elimu kama ambavyo wengi wanadhania.
Alisema hayo wakati kukiwa na malalamiko ya wanafunzi yanayotokana na kuondolewa kwenye orodha ya wanaotakiwa kupata mikopo, huku wanafunzi waliokuwa wakisoma kozi maalumu ya ualimu wa sayansi wakiondolewa na vyuo binafsi vya elimu ya juu vikilalamikia kutopangiwa wanafunzi.
Pia serikali ilitangaza kubadilisha upangaji wa madaraja ya matokeo ya elimu ya sekondari kutoka mfumo wa kupanga kwa kutumia GPA na kurudisha mfumo wa divisheni.
Kwa kawaida mgeni rasmi kwenye mahafali ya vyuo vya elimu ya juu huwa hahutubii, lakini Udoma ilimuomba aseme machache baada ya kutunuku wahitimu.
“Katika machache mliyotaka niseme ni pamoja na kuwataka Serikali waache kutegemea wawekezaji, maana vyuo vyenyewe vimewekezwa. Bado nasisitiza kuwa wafanye mikutano ya pamoja na waitane kwa haraka wazungumze bila ya kutegeana,” alisema.
Awali mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka alimweleza Mkapa kuwa Udom inakabiliwa na kazi kubwa mbili ambazo ni kutopelekewa fedha kutoka Bodi ya Mikopo pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi waliotoka Chuo Kikuu cha St Joseph ambao wamefanya chuo kipate shida ya namna bora ya kuwasaidia kwani masomo waliyokuwa wanasoma hayaeleweki.
Mwezi Februari, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ilifuta hati ya usajili ya kampasi mbili za Chuo Kikuu cha St Joseph za Sayansi ya Kilimo na Teknolojia na Chuo cha Tehama na kusema wanafunzi 2,046 waliokuwa wakichukua shahada na stashahada wangehamishiwa vyuo vingine.
Kuhusu changamoto ya fedha, Mkapa alisema Bodi ya Mikopo imewakwamisha kwa kiasi kikubwa kutokana na kutopeleka Sh6.5 bilioni ambazo ni ada ya wanafunzi katika mwaka wa masomo 2015/16.
Mwenyekiti huyo alisema deni hilo limeharibu taswira nzima ya Udom na kuwafanya wadau washindwe kuwaamini katika utoaji wa huduma mbalimbali, kama kushindwa kuendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi.
Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alisema kulikuwa na jumla ya wahitimu 4,839 wa kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili, na shahada ya uzamivu.


Friday, November 11, 2016

Mwalimu Mkuu ampiga mwanafunzi ngumi za uso.



Mwalimu una nafasi ya kuzuia matukio ya aina hii yasiendelee. Ni kweli kuwa kuna wakati wanafunzi wanaudhi kupindukia lakini imetupasa kujizuia hasira zinapokuwa juu dhidi ya wanafunzi. Matukio ya namna hii yakiendelea taswira ya taaluma ya ualimu itachafuka na kuonekana kama genge la watesaji wa wanafunzi.Chanzo cha habari hii ni gazeti la Mtanzania.


MWALIMU Mkuu wa Shule ya Sekondari Ridhwaa Seminary iliyopo wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Yusuph Kivugo, amemshambulia mwanafunzi wake, Mbaraka Mwalimu, kwa kumpiga ngumi usoni na kumsababishia maumivu makali.

Mwanafunzi huyo anayesoma kidato cha nne katika shule hiyo iliyopo Kinondoni Mkwajuni, alikutwa na mkasa huo Novemba 3, mwaka huu wakati akijiandaa na mtihani wa Historia.
Kwa mujibu wa ratiba ya mitihani ya taifa ya kidato cha nne inayoendelea nchini, mtihani huo ulikuwa unafanyika mchana, lakini hata hivyo hakufanya kutokana na maumivu aliyokuwa nayo.

“Tulikuwa msikitini na wenzangu tunasoma, ilikuwa ni saa mbili asubuhi kabla ya mtihani wa Historia kuanza, mwalimu alikuja akauliza kwanini tunapiga kelele na kuanza kutupiga.

“Upande wa pili kulikuwa na wanafunzi wa pre-form one ndio waliokuwa wakipiga kelele, nilishangaa kamkunja mwenzangu anaitwa Mohamed akawa anampiga mangumi, mimi nilijua labda kuna kosa amefanya.

“Katika kujitetea akina Mudy walikimbia, mara akaja kwangu akanishika akaanza kunishambulia, amenipiga ngumi nyingi za usoni, kwenye taya na nyingine jichoni kiasi kwamba sikuweza kufanya mtihani kwani jicho lilivimba sana,” alisema.

Mwalimu wa nidhamu shuleni hapo, Omary Ikome, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema jukumu lake ni kusimamia nidhamu kwa wanafunzi na kwamba suala hilo lipo juu ya uwezo wake.

“Nilimkuta Mbaraka analia na jicho la kushoto limevimba, nilimuuliza akasema amepigwa na mkuu. Mimi nasimamia nidhamu kwa wanafunzi, lakini kwa kuwa kitendo hiki kimefanywa na bosi wangu, siwezi kuzungumzia zaidi kwani lipo juu ya uwezo wangu,” alisema.

Mwalimu mkuu huyo alipoulizwa kiini cha tatizo, hakuweza kutoa ushirikiano na kumfukuza mwandishi ofisini kwake.


Sunday, November 6, 2016

Ushirikina kikwazo kingine cha maendeleo ya elimu yetu

IMANI ZA KISHIRIKIKINA KIKWAZO MOJA WAPO CHA MAENDELEO YA ELIMU
Kumekuwa na visa vingi vya vitendo vya kishirikina dhidi ya walimu, zipo shule zimekosa hata walimu baada ya walimu kukimbia kwa kuhofia ushirikiana. Baadhi ya maeneo yanaogopeka sana kwa ushirikina kiasi kwamba walimu wakipangiwa wanaogopa kwenda. Jamii inapaswa kubadilika maana suala la vitendo vya kishirikina si la kusema serikali itashughulikia bali ni la jamii yenyewe.Chanzo cha habari hii ni gazeti la mwananchi.
Kumekuwa na matukio mengi ya vitendo vya ushirikiana ambavyo huwalenga walimu.Baadhi ya maeneo walimu wakipangiwa hawakai kwa sababu ya vitendo vya kishirikina. Ni jambo la kusikitisha sana maana linaathiri sana walimu na elimu kwa ujumla maana ni wanafunzi ndiyo wanakosa elimu.Hatuwezi sema serikali ipambane na vitendo hivi bali tunasema jamii ibadilike.Chanzo cha habari hii ni gazeti la Mwananchi.

Kumekuwa na visa vingi vya vitendo vya kishirikina dhidi ya walimu, zipo shule zimekosa hata walimu baada ya walimu kukimbia kwa kuhofia ushirikiana. Baadhi ya maeneo yanaogopeka sana kwa ushirikina kiasi kwamba walimu wakipangiwa wanaogopa kwenda. Jamii inapaswa kubadilika maana suala la vitendo vya kishirikina si la kusema serikali itashughulikia bali ni la jamii yenyewe.Chanzo cha habari hii ni gazeti la mwananchi.
Ukerewe. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Frank Bahati amesema wafanyakazi 46 wa wamewasilisha maombi ya kuhamishwa kwa kuhofia ushirikina.
Bahati amesema kuwa maombi hayo yamewasilishwa kwa miezi kumi tangu mwaka huu uanze.
“Tunaendelea na uchunguzi kuhusu sababu za maombi haya, hatua za kisheria zitachukuliwa iwapo itabainika kuwa watumishi hawa wanatumia madai ya vitendo vya ushirikina kwa ajili ya kupata uhamisho nje ya wilaya,” ameonya Bahati.
Amefafanua kuwa katika uchunguzi wa awali imebainika kuwapo kwa baadhi ya wazazi wilayani humo kutumia vitisho vya ushirikina dhidi ya watumishi wanaowabana kwa makosa mbalimbali ikiwamo utoro.
Hivi karibuni Shule ya Msingi Uhuru ilifungwa baada ya walimu kuacha kuingia darasani wakishinikiza kuhamishwa kutokana na hofu ya ushirikina.
Walimu hao walidai mwalimu mwenzao,  Obadia Bwatwa alianguka ghafla na kufa wakati akirejea nyumbani kutoka shuleni.
Tangu kifo hicho kitokee Oktoba 23, mwaka huu, walimu hawajaingia darasani kufundisha baada ya kuingiwa hofu wakiamini kifo cha mwenzao kilitokana na  ushirikina.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amekanusha kifo hicho kutokana na ushirikina akisema uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa mwalimu Bwatwa alikuwa na ugonjwa wa moyo.

Thursday, November 3, 2016

Tusipobadili mitaala vijana wetu watabaki vibarua



Bado taifa hili lina watu wanaofikiri vizuri kiasi cha kuweza kutoa mawazo ya kuiendeleza nchi. Tunapaswa kujivunia watu hao wenye vipawa vya kufikiri na wenye ujasiri wa kuweka mawazo yao wazi kwa maslahi mapana ya nchi. 

Mwandishi wa makala hii ni miongoni mwa watu hao.
Makala hii iliandikwa na mwanasafu maaru na mkongwe wa gazeti la Raia Mwema,Gidion Shoo na kuchapishwa na gazeti hilo.

VIWANDA. Viwanda. Viwanda. Hilo ndilo neno kuu vinywani mwa Watanzania. Hii ni ndoto nzuri. Kila mmoja aipendaye nchi hii anaipenda kuiota na kila mmoja anachora taswira yake ya Tanzania ya viwanda.

Wapo wanaoiona Tanzania ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya makundi ya wafanyakazi wakisubiri mabasi yaliyoandikwa Urafiki, Kiltex, Sunguratex na kadhalika ili kwenda kazini kuingia shifti na kuwapatia wenzao fursa ya kurejea nyumbani baada ya kumaliza ngwe yao ya uzalishaji kiwandani. Ilikuwa Tanzania ya Azimio la Arusha. Azimio lililokuwa chachu ya mapinduzi katika kila nyanja ya uzalishaji mali nchini.

Hali kadhalika wapo wanaoiona Tanzania ya viwanda vya kisasa zaidi ambavyo havihitaji nguvu kazi kubwa sana lakini vinazalisha zaidi kutokana na teknolojia ya kisasa ambayo imetawala katika uchumi wa viwanda kote duniani.

Zote hizo ni ndoto nzuri na njema. Ni ndoto zinazolitakia kheri taifa letu. Lakini wakati tukiwa katika kuota na kujitahidi kuchora picha ta Tanzania mpya hatuna budi kujiuliza maswali ya msingi kama vile nini nafasi ya vijana kama nguvu kazi katika Tanzania ya viwanda.

Tunaambiwa kwamba moja ya faida za viwanda ni kuongezeka kwa ajira kwa nguvu kazi ya taifa letu. Hilo ni jambo jema. Lakini pamoja na uzuri wake wote tunatakiwa kujiuliza swali moja la msingi kwamba hawa tunaodai kwamba watapata ajira katika hivyo viwanda vitavyojengwa hapa nchini ni kweli watapata ajira? Na kama bi kweli watapata ajira je, watapata ajira ya aina gani ni ajira ya kiwango au ili mradi ajira?

Hatuna budi kama taifa kujiuliza maswali ya msingi na kuyapatia majibu kwa sababu kama tutaimba ngonjera za kisiasa kwamba tunahitaji kuwa na viwanda kwa ajili ya kutengeneza ajira kwa vijana lakini tusifanye lolote katika maandalizi ya viwajana wenyewe basi tutakuwa tunatengeneza ajira kwa ajili ya vijana wa mataifa mengine.

Viwanda vya kisasa vinahitaji elimu bora. Vinahitaji watu wenye uelewa wa kutosha katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. Viwanda vingi hivi sasa duniani vinaendeshwa kwa mitambo ya kisasa. Hata ujenzi wa barabara unafanyika kwa kutumia mitambo ambayo inahitaji maopereta waliopatiwa mafunzo maalum kwa ajili ya kuiendesha. Buldoza la siku hizi ni tofauti na la zamani. Buldoza la siku hizi ni la kidijitali na linaendeshwa kwa kompyuta.

Ili kujiandaa na Tanzania na viwanda ni lazima kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapatiwa elimu bora ya kisasa inayoendana na mapinduzi ya sayansi na teknolojia yanayoiongoza dunia hivi sasa.

Kwa mantiki hiyo basi mitaala ya elimu katika shule zetu zote ni lazima iandaliwe kwa kuzingatia ukweli huo kwamba dunia tuliyopo hivi sasa ni ya kidijitali. Si sahihi hata kidogo kuendelea na mitaala ya elimu ambayo haitilii maanani mapinduzi ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kote duniani. Hii maana yake nini?

Shule zetu za msingi hazina budi kuhakikisha kwamba mtoto anaelekezwa katika kuijua dunia kwa kutumia nyenzo za kisasa ambazo ni za kidijali zaidi kulinganisha na zile tulizotumia sisi wakati tunasoma. Mtoto wa kisasa hawezi kutengwa na kompyuta kwani kompyuta ndiyo kila kitu kuanzia katika kutumia maktaba za ndani na nje ya nchi hadi kufikia katika upishi wa keki na chapati kutumia majiko ya kuoka kwa kutumia mionzi.

Kuingia kwa simu smati yaani smartphones ni ushahidi kwamba tunakoelekea bila ya kujua kutumia mitambo ya kidijitali baisha yatakuwa ni magumu sana.
Kwa maana hiyo ni kwamba kasi ya maendeleo katika sayansi na teknolojia inafanya kiu ya Tanzania ya viwanda kuwa si kubwa tu bali kuwa ya changamoto kubwa sana.

Ni wazi kwamba hata kama tungelitaka kurejesha viwanda vile vilivyouawa wakati wa zama za Mwalimu Nyerere ukweli ni kwamba dunia imekwishaachana na viwanda hivyo. Viwanda vingi duniani ni vya teknolojia ya kisasa inayohitaji uelewa mkubwa wa jinsi ya kuendesha mitambo ya kisasa.

Kadri tunavyozidi kutafuta wawekezaji ndivyo tunavyokutana na teknolojia ya kisasa. Hata kama tukisema tuwe na viwanda visivyokumbatia teknolojia ya kisasa kwa kiasi kikubwa bado hicho kiasi kilichopo kitatulazimisha sisi kuwa na watu wenye uelewa wa sayansi na teknolojia tofauti na ilivyokuwa enzi za Kiltex, Mwatex na kadhalika.

Kama hatutaketi chini na kuangaliza mitaala yetu ya elimu na kutoa kipaumbele katika masomo ya sayansi na teknolojia ya kisasa tutakuwa katika hatari ya kuwa wafanyakazi wa daraja la chini katika viwanda tutanavyopigia debe kuanzishwa kwa wingi hapa nchini. Maana yake ni kwamba shule zetu hazina budi kutilia mkazo masomo yanayohusisha teknolojia ya mawasiliano kama msingi na nguzo ya elimu yote kuanzia vidudu.

Tunatakiwa kuhakikisha kwamba mtoto wa Kitanzania anakuwa na urafiki wa karibu na teknolojia ya mawasiliano kama msingi wa upatikanaji wa elimu kwani vinginevyo tutakuwa tunajidanganya.

Mtoto asiyejua kompyuta hana lake katika uchumi wa viwanda wa kisasa. Hata kama sisi tungelipenda kuwa na viwanda visivyokuwa vya kisasa sana bado hivyo viwanda kwa kiwango kikubwa vitahitaji uelewa wa kiasi kikubwa wa teknolojia mpya ya sayansi ya mawasiliano kwa sababu hata umeme unaoendesha mitambo hiyo unatumia mita za LUKU na wala si zile za kuzunguka za karne iliyopita. Huo ndio ukweli.

Ili kuhakikisha kwamba vijana wa nchi yetu wanaandaliwa kwa ajili ya kuingia katika uchumi wa viwanda ni lazima shule wanazosoma ziwe na viwango vya kisasa kuanzia msingi. Ina maana kwamba kila shule ni lazima iwe walau na maabara ndogo ya kompyuta kama sehemu muhimu ya mafunzo yao. Ili shule iwe kompyuta ni lazima iwe na umeme wa uhakika. Ni shule zetu ngapi za msingi zina umeme?

Aidha, swali la kujiuliza ni waalimu wangapi wa shule za msingi kote nchini wanao uelewa wa jinsi ya kutumia kompyuta? Wakati kompyuta ni kifaa cha nyumbani katika takriban kila familia huko ughaibuni ambako ndiko tunahangaika kuwaomba waje wawekeze kwenye viwanda, je, hapa nchini ni shule ngapi za msingi zina kompyuta?

Shule zetu nyingi za msingi hazina umeme. Watoto wetu wanamaliza elimu ya msingi bila ya uelewa wa kompyuta. Hiyo inawakwaza wanapoingia katika masomo ya sekondari na hiyo inaendelea hadi wanafika mbele ya safari.

Ninapomsikia waziri mwenye dhamana ya elimu anapiga kelele kuhusu sayansi na teknolojia na hata kufikia hatua ya kutoa maelekezo kwamba kila mtoto asome sayansi ninamuelewa kwa dhati kabisa japokuwa sikubaliani na staili hiyo ya utoaji wa elimu. Hakuna sababu ya kuwalazimisha wasiotaka masomo ya sayansi kuyasoma isipokuwa ni muhimu kuwalazimisha wote kutumia sayansi na teknolojia kupata elimu.

Inamaanisha kwamba kila motto ni busara akajua jinsi ya kutumia kompyuta kwani hivi sasa dunia inatafuta elimu katika mitandao ya inteneti ambayo kimsingi ni utumiaji wa kompyuta kwa ajili ya kuhifadhi taarifa ambazo ndani yake kuna elimu kubwa tu.

Mtoto asiyejua kutumia kompyuta ni wazi kwamba atakuwa hawezi kushindana katika soko la ajira la zama hizi. Kompyuta ndiyo maktaba, ndiyo vitabu vya ada na kiada, ndiyo mabuku ya rejea na kadhalika. Ili mradi mtoto anayejua kutumia kompyuta kwa ajili ya kujipatia elimu atakuwa mbele ya yule ambaye hana fursa hiyo.

Hatuna budi basi kuwaandaa vijana wetu kwa ujio wa viwanda vya kisasa kwani tusipofanya hivyo tutajikuta katika wakati mgumu. Tutajengewa viwanda lakini watakaohudumu humo watatoka kwa wale waliofanya maandalizi ya kutosha kielimu kwa ajili ya ujio wa viwanda.

Ni wakati muafaka hivi sasa kwa wataalamu wetu wa mitaala ya elimu kupitia upya taratibu za ufundishaji ili kuhakikisha kwamba vijana wetu hawaishii kuwa ni watu wa kubofya tufe za simu tu bali wawe ni watu wanaojua kwamba hiyo simu ya mkononi ni mwendelezo wa kompyuta na kwamba kompyuta ni chombo muhimu sana katika maisha ya leo duniani.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...