Mwaka mmoja wa utawala wa serikali ya awamu ya tano hauwezi
kupita bila kufanyiwa tathimini ya kina jinsi alivyoenenda kadiri ya ahadi
alizoahidi, kadiri ya ilani ya chama chake katika uchaguzi na kadiri ya
alivyoshughulikia changamoto za wananchi.
Mafanikio na madhaifu
ya serikali hii yapimwe kwa kutathimini jinsi ilivyoshughulikia kero sugu za
wananchi, jinsi ilivyotekeleza ahadi na ilani yake ya uchaguzi, kadhalika
tathimini ijielekeze kwenye ubunifu na utayari wa serikali kushughulikia kero
mpya na za dharura.
Tathimini yangu juu ya serikali ya awamu ya tano, itajikita
katika kuitazama sekta ya elimu. Sera ya elimu bure ndiyo eneo ambalo jicho
langu litajikita zaidi. Sera ambayo imeipaisha sana serikali ya awamu ya tano
kiasi hatuwezi kutathimini mafanikio ya awamu ya tano bila kujadili mafanikio
ya utekelezaji wa sera ya elimu bure. Utekelezaji wa sera hii kwa vitendo
umechangia mafanikio yafuatayo kama Mr.Mwalimu Blog inavyofafanua:
Idadi ya wanafunzi kwa ngazi ya awali, msingi na sekondari
imeongezeka kwa kasi. Kwa kweli kama kuna mafanikio ya wazi ambayo serikali ya
awamu ya nne imepata basi ni kuongeza idadi ya wanafunzi mashuleni. Watoto
waliokosa elimu kwa sababu ya ufukara sasa wana matumaini ya kupata elimu.
Utengenezaji wa madawati umeboresha mazingira ya usomaji.
Rais Magufuli amejitahidi sana kushughulikia suala la wanafunzi kukaa chini
kutokana na ukosefu wa madawati. Ukosefu wa madawati umeathiri sana mazingira ya kujifunza na
kujifunzia kwa wanafunzi.
Mtoto anayekaa chini
wakati anafundishwa na watoto watano waliobanana kwenye dawati moja ambalo
hukaliwa na watoto wawili hawezi kuelewa vizuri anachofundishwa. Awamu ya tano imepigana vita na imeshinda
kiasi kikubwa sana vita hii dhidi ya watoto kukua chini. Eneo hili ni eneo
ambalo pia serikali inapaswa kupongezwa waziwazi.
Serikali ya awamu ya tano imerejesha uwajibikaji wa
watumishi wa umma. Si siri nchi imepita kwenye mpito cha uharibifu wa maadili
ya utumishi wa umma na sasa Rais Magufuli na serikali yake wapo kwenye kipindi
cha mpito cha kurejesha maadili na uwajibikaji wa watumishi wa umma.
Hili Rais pia kwa kiasi kikubwa amefanikiwa, watumishi
wanaheshimu kazi na wanawajibika hivyo walimu kama sehemu ya watumishi wa umma,
upepo huu wa matengenezo unawakumba pia. Walimu wengi sasa wanahudhuria katika
vituo vyao vya kazi na wanawajibika. Haya ni mafanikio ya kujivunia na
kupongezwa ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja.
Ulipaji wa posho za madaraka kwa wakuu wa shule, walimu
wakuu na waratibu wa elimu. Serikali imetekeleza moja ya dai la muda mrefu la
walimu kutaka kuwepo na posho ya madaraka. Katika kuanza kutekeleza dai hilo,
serikali imeanza kuwalipa wakuu wa shule posho ya madaraka ya shilingi 250000,
walimu wakuu shilingi 200000 na waratibu shilingi 250000. Haya ni mafanikio
yanayoweza kuchagiza kiwango cha elimu. Ni mafanikio kwa sababu wakuu hawa
watajituma zaidi na watawawajibisha zaidi walio chini yao.
Kama wasemavyo waswahili penye mafanikio hapakosi
changamoto, jitihada zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa ili kuboresha
elimu hazijafanikiwa kwa kwa asilimia mia. Hizo Mr.Mwalimu Blog, tunaziita
changamoto kwa sababu zinaweza kutatuliwa, si mambo yaliyoshindikana kabisa
bali ni mambo tu yanayohitaji dhamira ya kweli katika kuyashughulikia:
Changamoto kuu katika kipindi cha mwaka mmoja cha awamu ya
tano ni uhaba wa walimu. Uhaba wa elimu ni miongoni mwa sababu kubwa sana
inayodhoofisha elimu yetu. Mathalani katika shule ambayo nafundisha, shule
imeanza mwaka 2013 hivyo mwaka huu inatoa wanafunzi wa kwanza wa kidato cha nne
lakini Tangu imeanzishwa haijawahi kuwa na mwalimu wa somo la Fizikia!
Katika miaka minne ya
kuwepo kwake imekuwa na walimu wa Baiologia na Kemia kwa kipindi cha mwaka
mmoja na nusu pekee. Kutoajiri walimu. Licha ya changamoto walizo kabiliana
nazo, kitendo cha serikali ya tano kutoaajiri mwaka 2016 kimeathiri sana elimu.
Uhaba wa walimu uliopo ungepungua kama serikali ingeajiri walimu mapema mara tu baada ya kuhitimu vyuo badala ya
kuwaacha waranderande mtaani.
Sera ya elimu bure imetengeneza hali ya kubweteka kwa
wazazi, baada ya kutangazwa elimu bure wazazi wengi sasa wanafikiri kila kitu
kitafanywa na serikali. Wazazi wengi wasio na uelewa wamejitoa kwenye nafasi
zao za kuwawezesha vijana wao, kuwahamasisha kusoma, jukumu hilo wamewaachia
walimu. Hivyo elimu ni bure lakini watu hawana msisimko wa kusoma na kusomesha.
Ni kama sera hii ya elimu bure imewafanya baadhi ya wazazi kuwa kupe.
Sera ya elimu bure imeathiri utoaji wa elimu, ubora wa elimu
na uendeshaji wa shule hivyo kuathiri ubora wa elimu. Kila mwezi Serikali
inatoa kiasi fulani cha fedha kufidia ada ambayo ilikuwa inatozwa kwa
wanafunzi. Uendeshaji wa shule ambao ulikuwa ukitegemea sana michango ya
wanafunzi, sasa unategemea ruzuku na fidia ya ada. Kwa kiasi kikubwa elimu bure
imenufaisha wazazi au walezi lakini imeathiri uendeshaji washule na ubora wa
elimu.
Kupitia michango ya wanafunzi, shule ambazo hazina walimu wa
baadhi ya masomo hususani yale ya Sayansi ambayo yana uhaba mkubwa, shule
ilitumia fedha ya taaluma iliyokuwa ikichangwa na wanafunzi kuajiri walimu wa
muda. Hivyo pia shule nyingi za msing zilitumia walimu wengi wa kibarua cha muda
kufundisha madarasa ya juu na hata darasa la awali. Shule ziliweza kufanya
mitihani yenye ubora kwa kuwa fedha zilikuwepo.
Kwa sababu fedha za ruzuku na fidia ya ada hutolewa kwa
shule kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo au waliosajiliwa na shule husika,
shule nyingi zinakabiliwa na ukata kutokana na kuwa na idadi ndogo ya
wanafunzi. Fedha inayopatikana inaruhusu kufanya mahitaji madogo madogo ya
shule kama chaki, vitabu, na zana zingine za kujifunzia.
Hali ni mbaya sana
katika shule nyingi, baadhi ya shule zimefikia kushindwa kuchapa mitihani,
wanafunzi wanaandikiwa mitihani ubaoni. Hii
hali ambayo ipo na haisemwi sana lakini ina athari kubwa. Serikali
itizame upya kiwango cha fedha inachotoa mashule ili kiweze kukidhi mahitaji ya
uboreshaji wa elimu.
Kuweka vigezo vipya vya kujiunga na chuo kikuu kumeminya pia
mawanda ya elimu kukua. Nchi hii inawasomi wachache sana, sasa inapotokea
vinawekwa vigezo vya kubana zaidi ili watu wasipate elimu ya chuo kikuu lazima
ishangaze. Alama za kujiunga na chuo kikuu kwa wanafunzi waliotoka moja kwa
moja kidato cha sita ni wastani wa D mbili au alama nne kutoka E mbili au alama
tatu za awali.
Wizara ya elimu imetangaza vigezo hivyo mwaka huu na
imedahili wanafunzi wa mwaka huu kwa kutumia utaratibu huo. Kanuni hizi mpya,
ngumu na za ghafla zimeathiri ndoto za watu wengi kujiendeleza. Serikali
imechukua maamuzi haya haraka ilipaswa itoe maamuzi haya mwakani au ingetangaza
mwaka huu lakini yangeanza kutekelezwa mwakani ili watu wajiandae.
Ni hivyo pia watu wanaotaka kujiunga na chuo kikuu kwa cheti
cha stashahada, sasa itabidi angalau wawe na ufaulu wa kuanzia daraja la 3.
Bado maamuzi haya yanaathari hasi kwa watumishi waliopanga kujiendeleza mwaka
huu. Mathalani walimu na wauguzi ni wahanga zaidi kwani wengi kutokana na mfumo
wa elimu zao wengi huhitimu ngazi za stashahada wakiwa na chini ya daraja la
tatu.
Wanafunzi wa kidato cha nne nao hawako salama, sasa daraja C
linaanzia 45 kutoka 41 ya awali, daraja B linaanzia 65 kutoka 61 ya awali,
Daraja A limeshushwa sasa litaanzia 75 mpaka 100. Ni jambo jema kwa uboreshaji
wa elimu yetu lakini litaumiza watoto wetu hasa wanyonge. Watoto
waliopandishiwa madaraja tukumbuke ni hawa ambao hawana walimu, hawana maabara,
hawana maktaba, wanasoma kwa kukaa chini.
Kabla ya kupandisha madaraja serikali ilipaswa iboreshe
kwanza mazingira ya utoaji elimu na ufundishaji ndipo mabadiliko haya yangekuwa
na tija. Vinginevyo kuwapandishia madaraja wanafunzi ambao hawana walimu, maabara
wala maktaba kadhalika hawana vitabu ni dhuluma.
Wahanga zaidi wa mabadiliko
haya ni watoto wa shule za kata, ambao walikuwa wanapata 41,42,43,44 na hivyo
kujikuta wana daraja C leo wengi wanaoangukia hapo watajikuta wana D.
Kutoongeza mishahara kuna athari hasi. Licha Serikali ya
awamu ya tano kurejesha ni dhamu ya kazi kwa watumishi hususani walimu kwa
kiwango kikubwa, lakini kutowaongezea walimu mishahara kumenyong’onyeza sana
mioyo ya walimu na kumevunja moyo wa uwajibikaji wa dhati.
Uwajibikaji uliopo hivi sasa kwa walimu ni wa woga tu.
Walimu wengi wanawajibika kwa kuhofia kuchukuliwa hatua za kisheria lakini
uwajibikaji kutoka ndani ya moyo wa mwalimu umepungua. Hali hii imetokana na
mazoea ya walimu kuongezewa mishahara kila ifikapo mwezi wa saba kadhalika
walimu walikuwa na matumaini makubwa sana na Rais wao kuwa awamu hii kulingana
na ahadi zake angeboresha sana maslahi ya wafanyakazi. Kitendo cha kutoongezewa
mishahara mpaka sasa kina athari, hivyo hii ni moja ya kasoro ya serikali ya
awamu ya tano katika kuboresha walimu.
Mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu bado hali si shwari. Manung’uniko
ni mengi kutoka kwa vijana wa vyuo, kinachoendelea kinakinzana kabisa na ahadi
za Mh. Rais Magufuli wakati wa kampeni zake, ni kama ilikuwa ahadi ya kisiasa
tu ili kujipatia kura kama ilivyoada ya wanasiasa wengi kutoa ahadi nyingi
wasizoweza kutekeleza. Ubaguzi katika utoaji wa mikopo ni ukandamizaji wa
wanyonge kwa kuwa sehemu kubwa ya wanufaika wa mikopo hii ni wanyonge.
Ukitoa mikopo kwa ubaguzi maana unawanyima wanyonge nafasi
ya kujiendeleza, ukiwanyima nwanyonge nafasi ya kupata elimu basi unatengeneza
tabaka katika jamii. Tabaka la wenye nacho na wasionacho.
Mr.Mwalimu Blog tunasema, ELIMU KWANZA. Elimu
lazima kiwe kipaumbele cha kwanza katika nchi maskini kama Tanzania. Maendeleo
yote ya kimiundombinu, kimawasiliano lazima yatangulie na maendeleo ya kielimu.
Kuwa na nchi yenye barabara za lami mpaka uchochoroni lakini kuna watu wengi
wasiojua kusoma na kuandika na kasoro.
Kadiri ya tafiti zaidi ya asilimia ishirini humaliza shule
za msingi bila kujua kusoma na kuandika. Zaidi ya asilimia hamsini ya wanafunzi
wakidato cha nne humaliza shule wakipata madaraja dhaifu yasiyowawezesha
kuendelea. Pia walimu katika shule nyingi wanafundisha katika mlundikano mkubwa
wa wanafunzi .Hizi ni changamoto za msingi ambazo serikali hii inapaswa itatue.
0 Comment to "MWAKA MMOJA: JPM ALIVYOIPANDISHA NA KUISHUSHA ELIMU."
Post a Comment
Post a Comment
1410