Joseph Mungai ni moja ya wanasiasa wakongwe wasioweza kusahaulika katika nchi hii, amewahi kuwa waziri katika wizara mbali mbali tangu serikali ya awamu ya pili mpaka ya nne. Ni mmoja kati ya mawaziri wa elimu wa Taifa hili ambaye alifanya kazi kubwa ya kuboresha elimu, pia anashutumia kwa kuharibu mfumo wa elimu nchini.Makala hii ilichapishwa na gazeti la Mwananchi, fuatilia mahojiano haya ufahamu kiundani.
Kwa ufupi
Mungai, ambaye
alikuwa ajibu tuhuma zilizoelekezwa kwake baada ya kustaafu siasa, amesema hata
kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete hakutaka kumteua kuendelea
kuongoza elimu kwa kuwa alitaka kufurahisha walimu waliokuwa wakimchukia
kutokana na kuwabana.
Joseph Mungai,
ambaye alikuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni wa Serikali ya Awamu ya Tatu,
amepinga vikali shutuma kuwa alishusha kiwango cha elimu, badala yake
akairushia lawama awamu iliyofuata kuwa ilifanya maamuzi yaliyozorotesha sekta
hiyo.
Mungai, ambaye
alikuwa ajibu tuhuma zilizoelekezwa kwake baada ya kustaafu siasa, amesema hata
kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete hakutaka kumteua kuendelea
kuongoza elimu kwa kuwa alitaka kufurahisha walimu waliokuwa wakimchukia
kutokana na kuwabana.
Mwanasiasa huyo mstaafu
pia alipinga shutuma dhidi yake kuwa alifuta michezo shuleni, akisema hahusiki
na suala hilo na alichokifanya ni kufuta michango ya mashindano ya Umiseta na
Umitashumta na kutoa maelekezo michezo ifanyike nje ya muda wa masomo au
mwishoni mwa wiki.
Mungai aliamua
kuweka bayana masuala hayo wakati alipofanya mahojiano na mwandishi Luqman
Maloto kuhusu mabadiliko makubwa ya elimu ambayo Serikali ya Awamu ya Tatu
iliyafanya, lakini akaelekezewa lawama kuwa ndiye aliyeyafanya bila
kushirikisha wadau na kusababisha kuanguka kwa elimu.
“Kama nilivyosema,
nilijisikia vibaya kuona kazi nzuri tuliyoifanya chini ya uongozi wa Rais
(Benjamin) Mkapa inabomolewa katika mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya
Nne,” alisema Mungai alipoulizwa alijisikiaje wakati anaona Baraza la Mawaziri
linabadilisha uamuzi ambao waliufanya wakati akiwa Waziri wa Elimu.
“Nilisononeka
sana. Pamoja na utu uzima wangu, sikusikilizwa. Niliwatahadharisha wahusika
kuwa matokeo mabaya ya uamuzi huo watayaona baada ya miaka kadhaa. Matokeo
yakawa kama nilivyosema. Baada ya mwaka 2007, matokeo ya mitihani ya darasa la
saba na kidato cha nne yalianza kushuka mwaka hadi mwaka.”
Mungai alisema
katika kipindi hicho idadi ya wahitimu wanaofeli iliongezeka mwaka hadi mwaka
na kufikia kiwango cha juu mwaka 2012 wakati idadi ya waliofeli ilipofikia
asilimia 60.
Alisema hata vyuo
vikuu viliendelea na vinaendelea hadi sasa kupokea wanafunzi wasiojua vizuri
Kiingereza kutokana na kufuta hata somo walilolianzisha la muundo wa Kiingereza
kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu ya sekondari ili kuwaandaa na masomo ya chuo
kikuu.
Mungai hakutaka
kumlaumu mtu yeyote aliyeshika wizara hiyo, akisema katika kipindi cha miaka
55, takriban mawaziri 23 wameiongoza, ikiwa ni wastani wa miaka miwili kwa kila
waziri na hivyo hakuna aliyepata muda wa kutosha.
Akizungumzia
uamuzi ambao uongozi wake ulifanya wakati huo, Mungai alisema ni kubuni na
kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2004 - 2009
uliopanua elimu ya sekondari kuwafikia angalau nusu ya rika lengwa la miaka
14-18.
“Tulianzisha vyuo
vikuu vishiriki vya elimu vya Chang’ombe na Mkwawa kwa lengo la kufundisha
walimu kwa ajili ya utekelezaji wa MMES. Upanuaji wa elimu ya sekondari
ulipangwa kuendana na upanuaji wa mafunzo ya walimu wa sekondari,” alisema.
“Najivunia kufuta
ada na kuifanya elimu ya msingi kuwa ya bila malipo na ya lazima kwa kila mtoto
wa miaka saba hadi 13. Mzazi alibakia na wajibu wa kumpa mtoto wake malazi, mlo
na mavazi. Nilipiga marufuku michango yote ya wanafunzi na wazazi wao. Michango
ya ujenzi wa shule ni jukumu la wote wenye uwezo wa kufanya kazi; na siyo
wazazi wa wanafunzi peke yao.”
Alisema wakati huo
Serikali ilitoa ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi ya Sh10,000 kwa kila
mwanafunzi, kutenga fedha kwa ajili ya michezo baada ya kufuta mchango wa
Sh1,000 kwa ajili mashindano ya shule.
Mbali ya MMES, pia
aliandaa na kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) 2002 -
2006 iliyotoa ruzuku za maendeleo na uendeshaji kwa wananchi wanaojenga na
kuendesha shule. Kadhalika, alisimamia kupunguzwa kwa ada ya shule za sekondari
za Serikali za kutwa kwa aslimia 50 kutoka Sh40,000 mpaka Sh20,000 na kuongeza
ruzuku maradufu ya kuwasomesha sekondari bila ada, watoto wa familia zisizo na
uwezo.
Alisema anajivunia
pia kuanzisha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), katika
vyuo vyote vya ualimu, kusimamia marekebisho na kuanza kutekeleza mtalaa mpya
wa sekondari uliounganisha masomo ya michepuo (ufundi, kilimo, biashara na
sayansi kimu) na masomo ya kawaida uliotokana na mapendekezo ya Taarifa ya
Mfumo wa Elimu ya Tanzania unaofaa kwa Karne ya 21 (The Tanzania Education
System for the 21st Century).
Alipoulizwa kitu
ambacho angetamani kuendelea kukisimamia wakati Serikali ya Awamu ya Nne
ikiingia madarakani, Mungai alitaja maboresho ya elimu kwa kutekeleza mtalaa
mpya.
“Lakini Rais
Kikwete aliniteua kuwa Waziri wa Kilimo na baadaye kidogo Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Niligundua baadaye
kuwa lilikuwapo shinikizo la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) nisiteuliwe kuwa
Waziri wa Elimu. Sikupendwa na walimu kwa sababu niliwabana mno,” alisema.
“Wakajibu mapigo
kwa kumwambia mgombea urais wa CCM mwaka 2005 (Kikwete) kuwa wanamuunga mkono,
lakini Mungai asiwe tena Waziri wa Elimu. Rais Kikwete akaamua kuwafurahisha
zaidi walimu kwa kumteua aliyekuwaRrais wa Chama cha Walimu, Mheshimiwa
Margareth Sitta kuwa Waziri wa Elimu baada yangu. Hivyo ndivyo siasa ilivyo.”
0 Comment to "Mungai; Kikwete alinitosa ili kuwafurahisha walimu"
Post a Comment
Post a Comment
1410