“Mungu akitaka jambo huwa hata kama watu hawalitaki. Mungu asipolitaka jambo haliwi hata kama watu wakalitaka kiasi gani”.Nina furaha kuchukua fursa hii kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kuniweza kuanza kwa Blog hii ambayo nina hakika itachangia sana maendeleo ya sekta elimu nchini Tanzania. Maendeleo ya elimu yatakuwa mbegu na chachu ya ustawi wa mtu mmoja mmoja , familia, jamii na hata Taifa kwa ujumla.
Nina mshukuru kwa sababu bila
yeye mimi sina ninachoweza, wala siwezi kufikiria jambo lolote jema lenye
manufaa, hata nikifikiri jambo jema sina maarifa na nguvu ya kulitekeleza.Bila
yeye mimi ni dhaifu na dhoofuli hali. Bila yeye mimi nisingekuwepo, wewe
usingekuwepo. Nini yeye ametupa ufahamu timamu, ametuwezesha kuona, kusikia na
hata kusema.
Nawashukuru pia watu walio nitia
moyo na kuniombea katika kufanikisha adhima yangu ya kuwa na blog. Kwa pekee
kabisa namshukuru ndugu George Akilimali ambaye ameshiriki kusanifu Blog hii na
wote waliochangia mawazo kwa namna moja au nyingine akiwemo ndugu Athur Davie
,raia wa Austria ambaye kwa sasa anaishi nchini, aliyenisaidia kuanza blog ya
kwanza mwaka 2014, japo haijadumu lakini ilifungua ufahamu na kuniongezea
shauku ya kuunda blog hii.
Lengo la Blog hii ya Mr Mwalimu
Blogspot.com ni kuwa jukwa huru la kujadili changamoto za kielimu katika hali
ya kujenga. Iko wazi sekta ya elimu ndiyo sekta mama lakini kwa miaka mingi
mambo hayaendi vizuri katika sekta hiyo. Kama inavyofahamika kudumaa kwa elimu
ni kuduma kwa kila maendeleo hivyo lazima zifanyike jitihada za kusisimua elimu
yetu.
Jukwa hili huru la kujadili
changamoto, litakuwa pia sehemu ya kuwasilisha hoja za msingi na zenye tija
katika sekta ya elimu. Ni sehemu pia ya kutoa ushauri wowote ambao utawezesha
kuleta chachu ya maendeleo ya kielimu.
Ukosoaji wenye tija katika elimu
na wenye ukweli na si wenye kuzaliwa kwenye hisia za juju juu utapewa nafasi.
Kuna mengi ya ya kuibua na kukosa ili Taifa listawi. Bila dhamira mbaya
tutakosoa sera, mikakati, uendeshaji na utawala wowote wa kielimu ambao hauna
tija kwa nchi.
Kwa kuwa Blog hii ni jukwaa huru,
msomaji yeyote, mdau wa elimu yeyote, mwalimu, mwanafunzi, mzazi au mlezi
yeyote ataruhusiwa kutoa hoja yake aliyonayo. Mtu mwenye andiko lenye tija atawasiliana
nami kipitia namba tajwa hapo juu au email tajwa.
Atatuma andiko lake na baada ya kuhaririwa
litachapishwa likiwa na jina la mwandishi husika. Hivyo ni sehemu pia ya
kuendeleza vipaji vya uandishi kwa watu walionavyo. Ukiwa na chochote chenye
kujenga elimu, usisite kuwasiliana nami.
Jukwa hili litakuwa sehemu ya
kujifunza, kushauri, kuonya, kukosoa na kuibua mijadala ya kielimu, wakati huo
huo itakuwa sehemu ya kufurahi kupitia kategoria ya kihoja. Hapo vitapatika
vihoja mbali mbali vilivyotokea katika mazingira ya utoaji elimu. Jukwaa hili
litakuwa pia mahala pa kubadilishana uzoefu kwa wadau wote wa elimu na
kujipatia taarifa za kielimu.
Kwa kuwa suala la uhamisho kwa
walimu ni moja ya changamoto kubwa, mwalimu mwenye kutaka kuweka tangazo lake
katika Blog hii ataruhusiwa, lakini atalipia shilingi elfu tano, 5000/,Blog
itamtengenezea tangazo na kuliweka katika kategoria ya Uhamisho.
Naomba nimalize kwa kunukuu kauli
aliyotoa mkuu wa mkoa wa Ruvuma, katika sherehe za siku ya walimu duniani,
ndugu Briliant Mahenge ,alisema “Tutaendelea kuwa maskini kama hatutawekeza
kwenye elimu”.
Kipaumbele cha kwanza kwa nchi
maskini ni utoaji wa elimu bora, ni kuelimisha watu wake na si vinginevyo.
Hivyo kwa kauli moja Blog hii ni jukwa la kutetea elimu ipewe kipaumbele cha
kwanza.
Uwekezaji wa kwanza kwenye elimu
ni kutoa mawazo yenye kujenga ambayo yataamsha hamasa ya viongozi wanchi katika
kuboresha elimu. Hiyo ndiyo haswa kazi ya Blog hii kuisemea sekta ya elimu bila
woga wala kujipendekeza kwa yoyote. Elimu
Kwanza.
0 Comment to "MR.MWALIMU.BLOGSPOT.COM NI ELIMU KWANZA"
Post a Comment
Post a Comment
1410