.
K
|
asumba mbaya na hatarishi kwa maendeleo ya Taifa la
Tanzania, ni matumizi mabaya ya rasilimali watu. Nchi hii bado imeshindwa
kuweka mikakati mizuri ya kutumia wasomi wake wachache kwa manufaa mapana ya
nchi.
Tuna wasomi wachache lakini tu vinara wa matumizi
mabaya ya wasomi wetu, hatujali sana wasomi wetu wala hatuthamini sana nafasi
za wasomi wetu katika kujiletea maendeleo, matokeo yake nchi inasuasua
kimaendeleo na baadhi ya wasomi kukimbilia kutafuta maslahi nje ya Tanzania.
Fikiri tunawasomi wachache lakini bado wengine wanakimbilia nje ya nchi kwenda
kunufaisha nchi zingine!
Moja wa wosia maarufu wa baba wa Taifa, ni ule
anaosema ili kuweza kujiletea maendelea lazima kutumia kila ulichonacho kwa
kiwango cha juu. Kama nchi ina madini, basi yatumike kwa kiwango cha juu kabisa
katika kulitajirisha Taifa, na kama una watu, wape mafunzo na watumie kiwango
cha juu katika kujiletea maendeleo.
Sekta
inayoongoza kwa kutokujali sana wasomi wetu ni sekta ya elimu, licha ya elimu
yetu kukabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo uhaba wa walimu, miundominu
mibovu ya kufunza na kujifunzia, makazi duni ya walimu na kiwango cha elimu
kuwa cha chini bado serikali haijapanga mikakati mizuri ya kutumia wasomi wake
katika kuboresha elimu.
Kazi nzuri ya kuboresha elimu iliyofanywa na
serikali ya awamu ya tano imetiwa doa na kitendo cha serikali kutoaajiri walimu
mwaka 2017. Kwa kiasi fulani jitihada za serikali ya awamu ya nne kujenga
maabara, serikali ya awamu ya tano kushughulikia tatizo la upungufu wa madawati
na utoaji wa elimu bure haziwezikuleta
manufaa kama shule zinaendelea kukabiliwa na uhaba wa walimu.
Ajenda ya kwanza na kipaumbele cha kwanza cha nchi
maskini kama Tanzania lazima kiwe elimu, na kuboresha elimu kunaanzia kwa kuwa
na walimu wa kutosha, wenye ubora unaokidhi mahitaji pia wenye hali, hamasa na
shauku ya kufanya kazi. Mzizi wa elimu ni walimu.
Tukumbuke hakuna shule bila mwalimu. Tukiwa na
mwalimu popote penye wanafunzi panaweza kuwa darasa au shule hata kama iwe
chini ya mti, lakini bila mwalimu hata jengo lenye thamani kubwa na lililojaa
wanafunzi haliwezi kuwa shule kwa maana ya mahala sahihi pa kujifunzia.
Serikali haijaajiri walimu mpaka sasa kwa hoja yenye
mantiki kabisa ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa watumishi, zoezi ambalo
linaendelea takribani miezi minne sasa kwa mitindo tofauti tofauti. Uhakiki wa
watumishi ni jambo muhimu na halipaswi kupingwa na mtu yeyote mzalendo, lakini
maamuzi yoyote yenye kuleta athari hasi katika uboreshaji wa elimu lazima
yaonywe na yapingwe.
Baadhi ya watu watu, viongozi, wanasiasa na wadau wa
elimu wanafikiri kitendo cha walimu kutoajiriwa kimewaathiri walimu
waliotarajiwa kuajiriwa pekee kwa sababu wamechelewa kupata ajira ambayo
ingeboresha maisha yao. Na wengine wanachukulia uamuzi huu wa serikali
kutoaajiri walimu kuwa hauna athari yoyote mbaya, ndiyo maana sijasikia
wanaojiita wadau wa elimu, wanaharakati wa elimu wala wabunge wa chama chochote
wakizungumzia jinsi suala hili linavyoumiza watoto wa walalahoi wanaosoma
kwenye shule za kata. Naomba kuwasilisha mchanganuo wa athari hasi za kutoajiri
walimu kupitia MR.MWALIMU.BLOGSPOT.COM kama ifuatavyo;
Mfumo wa kuajiri walimu baada ya kuhitimu vyuo bado
una walakini katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu. Serikali ya awamu
ya kwanza ilijiwekea vipaumbele vitatu, kupambana na ujinga, maradhi na
umaskini. Ili kukabiliana na ujinga ilihakikisha inaandaa toa mafunzo ya ualimu
hata kwa watu wenye elimu ya darasa la saba maarufu kama walimu wa UPE. Walimu
hawa waliandaliwa kwa muda mfupi kisha waliajiriwa.
Siku hizi, mara nyingi wanafunzi wa ualimu kwa ngazi
ya astashahada, stashahada na shahada wanahitimu mwezi wa tano,wa sita, wa saba
na wa nane. Baada ya kupata matokeo yao na kufanya mahafali, wahitimu hao ukaa
nyumbani kwa kipindi cha miezi zaidi ya saba. Mathalani mara nyingi serikali
inaajiri walimu mwezi Machi au Aprili wa mwaka unaofuata baada ya ya mwaka wa
kuhitimu.
Kiuhalisia utaratibu huu wa kuajiri una kasoro kubwa
na unalitia Taifa hasara kwa sababu hauoneshi dhamiri ya dhati ya kukabiliana
na hali ya uhaba wa walimu. Ni kama nchi imetosheka na idadi ya walimu waliopo,
ni kama nchi haina uhaba wa wa walimu, ni kama hakuna watoto wetu wanaoumia
kutokana na uhaba wa walimu ,ni kama taifa haliumi kadhalika ni kama serikali
haina shida na walimu ila inaajiri tu kusaidia waajiriwa hivyo inaajiri muda
inaopenda na pale inapojisikia.
Huwezi kueleweka vizuri na watu wenye akili timamu
kama unalalamika njaa wakati shamba lako la mahindi limestawi, mahindi yamezaa
na yamekauka! Kwa hiyo, kwa upungufu wa walimu ambao nchi inao, na jinsi
serikali inavyochelewesha ajira za walimu, ni wazi huu ni ukiritimba na
utendaji wa mazoea usio na tija ya kuliokoa Taifa. Badala ya kurekebisha
kasumba hii ya kuchelwesha ajira za walimu, serikali mwaka huu imechelewesha
zaidi ajira hizo, hii ni kasoro ya wazi ambayo tujitetee tutakavyojitete
itabaki kuwa kasoro, tena kasoro endelevu.
Kutoajiri walimu ni kuitia doa sera ya elimu bure.
Kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa awamu ya tano, Mh. John Magufuli ya
kuhakikisha elimu inakuwa bure ina mwagiwa tope na kucheleweshwa kwa ajira za
walimu. Matokeo moja wapo ya sera ya elimu bure ni kuongezeka kwa idadi ya
wanafunzi wanaojiandikisha elimu ya msingi na hata elimu ya sekondari ya awali.
Mfano nimekuta shule moja ya msingi mkoa wa Geita imeandikisha wanafunzi zaidi
ya miambili wakati takwimu za nyuma wanafunzi waliokuwa wakiandikishwa darasa
la kwanza hawakuwahikufika hamsini!
Kufanikiwa kupata idadi ya wanafunzi wengi
wanaojiunnga na elimu ya msingi na sekondari kutokana na wazazi na walezi
kupunguziwa mzigo wa gharama za kusomesha ni jambo la kumpongeza sana Rais wetu
na watendaji wake wakazi. Kama haitoshi Rais amefanya kazi kubwa kuliondoa
tatizo la ukosefu wa madawati. Ni mambo ambayo usimpomgongeza Rais na serikali
yake ni wazi utakuwa na shida ya kitabia na kiufahamu.
Lakini sasa
nini thamani ya darasa lenye wanafunzi wengi wanaokaa kwenye madawati lakini
hawana mwalimu wa kuwafunza. Ni wazi elimu bure imeongeza wanafunzi mashuleni
lakini serikali haijaongeza walimu ni kama vile jitihada zimefanyika bila
maarifa. Nimejionea Geita wanafunzi wapatao miambili wakifundishwa na mwalimu
mmoja tena kwenye uwanja wa michezo maana hakuna darasa linalowatosha! Bila
walimu matunda ya elimu bure yatakuwa ni yale yale watoto kuhitimu bila kujua
kusoma na kuandika.
Kuna mengi ambayo hayafikiriwi jinsi Taifa
lilivyoumizwa na hali ya walimu kutoajiriwa kwa na pengine yanatia hofu
kuyasema lakini ni hali halisi. Mathalani watumishi wengi wa umma walikuwa na
matumaini makubwa kuwa Rais Magufuli ataongeza mishahara yao mara tu baada
kupitishwa bajeti mpya. Baada ya tarehe moja Juni kupita bila ongezeko zaidi ya
punguzo la kodi mioyo ya wengi ilishuka, lakini wakajipa moyo huenda mwezi
Septemba watapata ongezeko hilo kutokana na uhakiki wa watumishi hewa
kuendelea.
Mshahara wa
mwezi Septemba ulivyotoka bila ongezeko ukatawanya kabisa mioyo ya wafanyakazi
kiasi kwamba hata hamasa ya utendaji ikapungua, huu ni ukweli uliopo japo
unaweza usiwapendeze baadhi ya viongozi wetu, lakini ni vema kuufahamu ili
kuukabili kuliko kuuzuia usisemwe maana utaathiri zaidi Taifa kwa kipindi
kirefu. Kuwakosa walimu wapya kipindi hiki ambacho walimu wengi walio makazini
mioyo ya utendaji imeshushwa na ukosefu wa ongezeko la mshahara ni jambo lenye
kujeruhi Taifa.Walimu wapya wangeweza kupunguza athari za ukosefu wa ongezeko
la nyengeza ya mshahara kwa walimu.
Kutoajiri walimu ni hasara pana. kwa sababu katika
mwaka wa masomo, 2016, kuna walimu wengi wamejiunga na vyuo ili kujiendeleza
katika taaluma ya ualimu.Walimu hawa wameanza safari ya kujiendeleza baada ya
kuruhusiwa na halmashauri zao wanazofanya kazi. Halmashauri ziliwaruhusu
zikitaraji kupata walimu wapya mapema ambao wataziba nafasi za wale walioenda
masomoni.
Kadhalika katika kipindi cha mwaka 2015 na 2016 kuna
walimu wamestaafu, wameaga dunia pia kuna walimu walioathiriwa na zoezi la
uhakiki baada ya kubainika kuwa na mapungufu fulani ya kitaaluma au ya taratibu
za kiutumishi wa umma.
Kutokuajiri walimu ni hasara kwa sababu, walimu
wapya wanavyoajiriwa wanafanya kazi kwa nguvu sana kwa sababu si tu wanakuwa na
hamu ya ajira lakini pia wanakuwa na hamu ya kuifanya kazi yenyewe. Wanakuwa na
upendo wa dhati na kazi tofauti na walimu wenye muda mrefu kazini ambao
hufanyia uzoefu.
Walimu wapya pia huwa chachu mashuleni huja na mbinu
mpya za ufundishaji hivyo kuinua kiwango cha elimu hata kwa kuwapa hamasa mpya
walimu wenye muda mrefu. Kwa kutoajiri walimu wapya tumepoteza haya yote. Leo
walimu wanaongojea kuaajiriwa wana hamu
ya ajira ili wajikimu, hawana hamu ya kufundisha maana kuchelewesha ajira
kumeipa ganzi mioyo yao.
Haihitaji shahada ya utafiti wala shahada ya hesabu
kufahamu kuwa uhaba wa walimu uliokuwepo umeongezeka zaidi kwa sababa nafasi za
walimu waliofariki, walioenda masomoni, waliostaafu na walioathiriwa na zoezi
la uhakiki hazijazibwa. Tunaweza kukadiria athari za pengo waliloliacha walimu
hao ambalo halijazibwa? Tunaweza kufikiri kujifunza kwa watoto kunavyoathiriwa
na hali hii wakati walimu ambao wangeweza kuwasaidia wapo tu mtaani! Tuweke
kando siasa nyepesi na ushabiki, nchi imeumizwa na inaumizwa.
Kasumba ya Taifa hili kufanya mambo kwa mazoea, kwa
nidhamu ya woga, kujipendekeza, mihemuko na hisia bila kuzingatia changamoto
zinazoibuliwa na tafiti za watu binafsi na taasisi mbalimbali, ni miongoni
sababu zinazodumaza elimu yetu na ustawi wa nchi yetu.
Mathalani,
takwimu za mwaka huu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, zinaonyesha
kuwa asilimia 23 ya Watanzania wakiwamo vijana na watu wazima hawajui kusoma na
kuandika. Pia takwimu zinaonyesha kuna wimbi kubwa la wanafunzi wanaohitimu
elimu ya msingi bila kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mapema mwezi Septemba mwaka huu, 2016, Taasisi
ya utafiti ya Twaweza ilitoa matokeo ya utafiti wa uwiano wa walimu na wanafunzi
wenye matokeo ya kuumiza sana. Katika utafiti huo ilionyesha kwamba mikoa mingi
nchini ikiwemo mkoa wa Manyara, uwiano wa mwalimu mmoja ni wanafunzi 100 mpaka
126. Ikumbukwe kitaaluma darasa moja halipaswi kuzidi arobaini na tano! Utafiti
huo uliibua pia hali ya kusitisha ambao wanafunzi wengi hawajui kusoma na
kuandika!
Katika mazingira kama haya ya hali duni ya
elimu nchini, kutokuajiri walimu licha ya kufahamu hali hii mbaya ni kasoro, ni
kama vile nchi inajivunia kuwa na watu wasiojua kusoma na kuandika na ni kama
vile tunajivunia uwiano mbaya wa walimu na wanafunzi katika shule zetu.
Kwa
sababu baada ya tafiti hizi kutoka unawezaje kuthubutu kuwaacha walimu
waranderande mtaani kama kweli kuna nia ya kuinua kiwango cha elimu!
Tunawaachaje walimu,waliohitimu vyuo awamu mbili mtaani huku watoto wanahitimu
bila kujua kusoma na kuandika kwa sababu ya uhaba wa walimu.Walimu waliohitimu
mwaka jana na mwaka huu kama wangekuwa wameajiriwa wangepunguza kiasi fulani
kiwango cha idadi ya wanaohitimu bila kujua kusoma, kuandika na kufanya hesabu.
Kutokuajiri
walimu kuna kinzana na dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuwatetea
wanyonge. Waathirika wa kuu wa hali ya kutoajiri walimu ni
familia za walala hoi, kwa sababu walimu hawa ambao hawajaajiriwa wengi
wengeajiriwa shule za umma na shule za umma ndiyo zina upungufu mkubwa wa walimu.
Shule za binafsi walimu wanagombania vipindi wafundishe, shule za umma watoto
wanajifundisha wenyewe kwa ukosefu wa walimu.
Kwenye shule
za umma watoto wanakodolea macho ubao usio na maandishi, ndoto zao za
kujikwamua kimaisha kupitia elimu ziko matatani, wachache wanathubutu kuwa na
matumaini ya kushinda mitihani, mioyo inalia, serikali inajibu wasubiri walimu
watakuja kesho, kesho siku zinaenda. Walimu ambao serikali imewatelekeza mtaani
baadhi yao wamegeuka lulu na msaada mkubwa kwa shule binafsi ambao wanawatumia
vizuri katika kipindi hiki ambacho wanasubiri kuajiriwa.
Hivyo shule
binafsi zinazidi kujiimarisha kwa walimu hawa hawa ambao wangeweza kunufaisha
watoto wetu katika shule za umma. Ukitazama kwa jicho la tatu utaona jinsi
kutoajiri walimu kunavyoongeza pengo kati ya maskini na matajiri. Watoto katika
shule za umma hawana elimu, lakini wale wa shule za binafsi walimu wapo
wakutosha, ni kama mazingira ya maskini kuzidi kuwa maskini, tajiri kuzidi kuwa
tajiri kupitia uwiano usio sawa katika utoaji wa elimu.
Dhamira ya kuwa komboa wanyonge lazima ianzie kwenye
kuhakikisha wanapata elimu bora na ya uhakika. Kwa sababu katika nchi maskini
kama Tanzania elimu ndiyo silaha ya kwanza ya ukombozi. Pia wengi wa wahitimu
wa fani ya ualimu wanatoka familia maskini na za kati, hivyo kuwaweka mtaani ni
kuwaumiza wanyonge mara mbili. Kuajiri walimu ni kumkomboa myonge kupitia
ajiri, pia ni kumkomboa mnyonge sababu mwalimu mwajiriwa angeokoa kizazi cha
walalahoi kinachoangamia kwa ukosefu wa elimu.
Kutokuajiri walimu ni hasara kwa sababu kama
wangeajiriwa, serikali ingepunguza tatizo la ajira ambalo lina kua kazi ambapo
inakadiriwa kuwa kwa sasa limefikia asilimia 11. Walimu hawa wangeajiriwa
mapema, wangepunguza utegemezi kutoka kwenye famailia zao, ingepunguza uhalifu,
maana ukosefu wa ajira ni jambo la kuweza kuhatarisha usalama wanchi hasa
katika kipindi hiki ambacho vijana wengi wanaoenda vyuo wanakuwa wameshapata
mafunzo ya JKT. Kama wangeajiriwa baaadhi wangejikita kwenye kilimo, biashara
na hata biashara huduma hivyo kujistawisha na kulistawisha taifa.
Naibu waziri wa Tamisemi, Suleman Jafu, aliliambia
Bunge kwamba wizara yake ina mipango wiwili ya kukabiliana na uhaba wa walimu;
kwanza, ni kuwajiri wahitimu wa fani zote za Sayansi kuwa walimu wa masomo ya
Sayansi. Pili, kuchukua idadi ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za
sekondari wakafundishe shule za msingi.
Mipango hii ina kasoro za wazi, kwa sababu walimu wa
elimu ya msingi na sekondari kitaaluma wanaandaliwa tofauti. Mwalimu wa
sekondari kumpeleka kufundisha elimu ya msingi bila kumpa mafunzo si jambo
salama kwa elimu yetu. Mhitimu yeyote wa shahada ya Sayansi kutunukiwa ualimu
na kukabidhiwa darasa bila mafunzo maalumu ya ualimu ni kasoro na si salama kwa
mukstakabali wa elimu.
Mipango hii ya wizara haina mantiki sana wakati huu
ambao tuna wahitimu wa mafunzo ya ualimu awamu mbili, wa mwaka 2016 na 2017
wanaranda randa mtaani. Ni kasoro na kujichanganya kwa wizara kuwa na mipango
ya kuajiri watu kutoka nje ya fani ya ualimu, kuchukua walimu wa msingi
wakafundishe sekondari wakati tuna walimu waliohitimu taaluma hiyo wapo mtaani,
hawana ajira, hawalinufaishi Taifa!
Waziri wa elimu mama Ndalichako, pia ametangaza kuwa
masomo ya sayansi yatakuwa ya lazima kwa wanafunzi wote. Wakati serikali ikinadi
sera ya viwanda ili kuifanya nchi kuwa ya viwanda. Uhalisia wa kuwafanya
wanafunzi wote wasome masomo ya Sayansi una utafanikiwaje kama walimu wa masomo
ya sayansi tumewaacha mtaani, hawa ndiyo walimu ambao wangetia hamasa ya watoto
wetu kusoma masomo ya Sayansi. Nchi itakuwaje ya viwanda bila wazawa wenye
taaluma ya viwanda au ndiyo kuandaa kuwawashangiliaji wa viwanda badala ya
wanufaika wa viwanda?
Walimu ambao wangetengeneza wataalamu wa viwanda
tumewaacha wachome mahindi mtaani huku tunalalamika uhaba wa walimu wa Sayansi,
kama uhaba wa walimu wa Sayansi unatuumiza mioyo, kama tunataka nchi iwe ya
viwanda na kama tumekusudia kufanya masomo ya Sayansi yawe lazima walimu wa
Sayansi wanafanya nini mtaani mpaka sasa badala ya kuwa darasani wakifundisha.
Tumejenga maabara kwa wingi alafu walimu hatuajiri nini maana yake?
Ni
wizara ya Elimu pia ndiyo imetangaza rasmi kuanza kutumiwa kwa viwango vipya
kwa madarasa la ufaulu wa sekondari ya awali,awali daraja C lilianzia alama 41
mpaka 60, daraja B lilianzia 61 mpaka 80 na daraja A lilianzia 81 mpaka 100.
Kwa sasa daraja C linaanzia 45 mpaka 64, B ni 65 mpaka 74 na iwe imeshushwa 75
mpaka 100.
Viwango
vipya vinaathari nzuri lakini vinaathari hasi kwa watoto wa walalahoi wanaosoma
shule za kata zenye changamoto ya mazingira na miundombinu ya kujifunzia. Wengi
wa watoto hawa kufaulu kwao kunaangukia madaraja ya C na D.
Hivyo kuongeza vigezo hivi ni kuwaongezea
ugumu watoto hawa kwani wale walikuwa wanaangukia daraja C wataangukia daraja D
na wale wa waliokuwa wakiangukia daraja B wataangukia daraja C. Kama haitoshi
madaraja ya kujiunga na vyuo vikuu yamepandisha kutoka angalau E mbili kufikia
angalau D mbili yaani alama 4.
Tunaweza
tukatumia nguvu nyingi kukanusha kwamba kutoajiri walimu mpaka sasa kuna umiza
wanyonge na Taifa lakini ukweli huu ni halisia. Mathalani tutafakari kwa kina
athari za kupandisha madaraja ya ufaulu katikati ya uhaba wa walimu na bila
kuajiri walimu wapya.
Tumepandisha
madaraja ili kuboresha elimu ni jambo jema lakini nani atakwenda kuinua ufaulu
wa wanafunzi kadiri ya madaraja mapya ikiwa walimu tumewaacha mtaani? Ni kama
dhuluma fulani kuwapandishia wanafunzi madaraja ya ufaula bila kuwapatia
kuwaajiria walimu wa kuwasadia.
Ningependa mfumo unaotumika kuajiri askari,
utumike pia kwa walimu hasa kutokana na hali ya uhaba wa walimu tulionao.
Askari ambao pia ni matunda ya walimu wakihitimu tu mafunzo wanapangiwa vituo
vya kazi, kwa kuwa kuna upungufu wa askari nchi, kadhalika unyeti wa kazi yao.
Na fikiri ndiyo tungefanya kwa walimu, maana hakuna sababu ya walimu kukaa
mataani wakati nchi inaupungufu wa walimu.
Mimi ni hitimishe tu kwa kusema Taifa hili ni
maskini na linahitaji uwekezaji wakina katika elimu. Maendeleo katika
mawasiliano, uchukuzi na viwanda
tunayoyapigania hayatakuwa na maana kama nchi ina watu wengi wasio na
elimu. Haitapendeza nchi kuwa na ndege nzuri, reli ya kimataifa, madaraja
makubwa na barabara za lami kila uchochoro huku watu wan chi hii ni wajinga.
“Tutaendelea kuwa maskini tusipowekeza kwenye elimu” Ni
kauli nzito aliyoitoa Dr. Binilith Satano Mahenge, mkuu wa mkoa wa
Ruvuma katika maadhimisho ya siku ya mwalimu ambapo kimkoa wa Ruvuma
yalifanyika wilaya ya Tunduru. Hotuba yake fupi iliyojaa tafakari pana na
uhalisia wa tulipo na tuendako kama haututa wekeza katika elimu haipaswi
kuchukuliwa kawaida japo mimi nimechukua maneno hayo machache tuu. Elimu kwanza.
0 Comment to "SITISHO LA AJIRA ZA WALIMU LINAUMIZA NCHI NA WALALAHOI"
Post a Comment
Post a Comment
1410